Kuna neno zuri sana na lenye manufaa tunaloweza kulitumia kwenye maisha yetu ya kila siku na likatuwezesha kufikia mafanikio makubwa.
Neno hilo linatuokolea muda wetu, linatunza fedha zetu, linatuweka karibu na wale tunaowapenda na linatuma nafasi ya kukaa na sisi wenyewe kwa muda mrefu.
Neno hili linatuwezesha sisi kupata muda wa kutafakari maisha yetu zaidi na kujua ni hatua gani za kuchukua.

Neno hilo sio jingine bali ni neno HAPANA. Hapana ni neno zuri sana, ni neno ambalo ukiweza kulisema litakuletea uhuru mkubwa sana.
Lakini sisi ni watu, hatupendi kuwaumiza wengine, hatupendi kuonekana hatujali, hivyo ni vigumu kusema HAPANA, ni bora tukasema NDIO, ili tujenge mahusiano mazuri na wenzetu.
Hivyo marafiki zako wanapokupigia na kutaka mkapate moja baridi na moja moto wakati wewe una kazi yako ya pembeni unaifanyia kazi sio vizuri kuwaambia HAPANA, ni bora kuwaambia NDIO kwa sababu hii kazi unaweza kuifanya baadae tu. Na unaendelea kulalamika kwa nini huwezi kufanya kitu cha tofauti.
Unapokuwa na fedha na ukaona nguo nzuri au kitu chochote kizuri na ukapenda kukinunua, kusema HAPANA ni kujiumiza, kwani hela unazitafuta za nini, na hivyo unasema NDIO, unanunua, halafu baadaye unalalamika kwa nini unafanya kazi lakini huna akiba yoyote.
Ukweli ni kwamba unaposema NDIO jua kwamba kuna kitu kingine umesema HAPANA. Umesema ndio kwa muda wa kupumzika na marafiki zako bila ya kujua kwamba umesema hapana kwa kufanya kazi yako ya pembeni. Umesema ndio kwa kitu unachotaka kununua bila ya kujua kwamba umesema hapana kwenye kuweka akiba na kuwekeza zaidi.
Kila NDIO unayosema ina HAPANA ndani yake, na kila HAPANA unayosema ina NDIO ndani yake. Amua ni kitu gani unataka kwenye maisha yako, kusema ndio ili uwaridhishe wengine au kusema hapana ili uboreshe maisha yako.
Maisha ni yako chaguo ni lako.
TAMKO LA LEO;
Najua kila NDIO ninayosema kuna vitu vingi sana nimesema HAPANA. Najua nimekuwa naogopa kusema hapana kwa sababu naogopa kuwaumiza wengine, ila kumbe nimekuwa najiumiza mimi mwenyewe zaidi. Kuanzia sasa nitatumia HAPANA mara nyingi, kwa sababu kwenye HAPANA ndipo uhuru wangu ulipo.
Tukutane kwenye ukurasa wa 208 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.