Kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo mazingira ya kuendesha biashara yanavyozidi kuwa mazuri na rahisi. Miaka kumi iliyopita ili upate mkopo wa biashara ingekuchukua muda mrefu sana na kuupata tu unashukuru maana sio wote waliokuwa wanaomba walipata. Lakini sasa hivi kama una vigezo unaweza kupata mkopo ndani ya siku moja. Sasa hivi sio wewe mfanyabiashara unayeenda kutafuta wapi pa kukopa, bali taasisi za kifedha zinajinadi kila kona kwamba wanatoa mikopo rahisi.

Lakini pia urahisi huu wa upatikanaji wa mikopo haujaja peke yake. Umekuja na matatizo mengi pia. Kuna wafanyabiashara wengi ambao wameshuhudia biashara zao zinakufa kutokana na kuingia kwenye mikopo. Kuna mtu mmoja aliwahi kuniandikia akitaka ushauri aliniambia hatokuja kuchukua tena mkopo kwenye maisha yake, kitu ambacho mkopo umemfanyia hatakuja kusahau. Baadae tulikutana na kujadili na alikuja kuona makosa makubwa aliyofanya wakati anachukua na kutumia mkopo wake.
Najua kuna wafanyabiashara wengi ambao wanapitia kwenye hali hii. Labda una mkopo na unakusumbua sana au uliingia kwenye mkopo na biashara yako ikafilisiwa au mali zako binafsi zikafilisiwa. Leo hapa kwenye KONA YA MJASIRIAMALI tutajadili kuhusiana na wakati sahihi kuchukua mkopo kwenye biashara yako.
Kwanza kabisa naomba nikuambie na kukuhakikishia kwamba tatizo la wewe kuchukua mkopo na ukakuingiza kwenye matatizo sio tatizo la mkopo bali ni tatizo lako wewe binafsi. Kama mkopo utachukuliwa kwa wakati sahihi na ukatumika kwa matumizi sahihi basi mkopo huo utakusukuma sana wewe na biashara yako itakua kwa kiasi kikubwa.
Je ni wakati gani sahihi wa wewe kuchukua mkopo wa kibiashara?
Wakati sahihi kwako wewe mfanyabiashara kuchukua mkopo wa kibiashara ni pale ambapo biashara yako inafanya vizuri na unataka kuikuza zaidi. Elewa vizuri hapo, biashara inafanya vizuri maana yake inajiendesha kwa faida na sasa umeshakuwa tayari kuikuza zaidi. Huu ndio wakati ambapo unaweza kuchukua mkopo, ukausimamia vizuri kwenye biashara yako na ukafanikiwa.
Lakini wafanyabiashara wengi wamekuwa wakijidanganya au kudanganyika na kuchukua mkopo kwa sababu tu ana sifa za kupata mkopo au anakopesheka. Taasisi ya fedha inaweza kukuambia kwamba wewe unakopesheka, au ukaona tangazo linalovutia kwamba kuna mikopo ya biashara inatolewa. Usikimbilie haraka na kuchukua mkopo, kuambiwa kwamba unakopesheka maana yake taasisi ya fedha ina uhakika wa kupata fedha yao hata kama biashara yako haitafanikiwa. Matangazo ya upatikanaji rahisi wa mkopo yasikufanye wewe ufikiri kwamba mkopo ndio utakaoiwezesha biashara yako kukua. Ni vyema ukatengeneza biashara inayojiendesha kwa faida kwanza kisha ukichukua mkopo utajua ni eneo gani zuri kuuweka ili uendelee kupata faida zaidi, ulipe mkopo na biashara yako ikue.
Wafanyabiashara wengine wamekuwa wakichukua mkopo ili kufufua biashara inayofanya vibaya. Kosa kubwa sana. Kama biashara inajiendesha kwa hasara, kuchukua mkopo sio dawa ya hasara, ila ndio utaongeza hasara zaidi. Kama ndoo inavuja, kuweka maji mengi kutaifanya ivuje zaidi. Hivyo kama biashara yako inafanya vibaya, usikimbilie kuchukua mkopo. Jua kwanza ni tatizo gani linaendelea kwenye biashara yako, litatue, hakikisha biashara haiendi kwa hasara na hapa unaweza kuchukua mkopo na kuirudisha biashara kwenye mstari mzuri. Lakini kukimbilia kuchukua mkopo bila kwanza ya kutatua tatizo ni kujiingiza kwenye matatizo zaidi.
Hakikisha biashara yako inajiendesha kwa faida kabla hujaingia kwenye mkopo na pia jua mkopo unaochukua unauweka kwenye sehemu ipi ya biashara yako ili uweze kutengeneza faida vizuri na kurudisha mkopo huku biashara yako inakua. Kumbuka kwamba mkopo unachukua na unatakiwa kulipa kwa riba. Hivyo chochote unachofanya na mkopo unaochukua hakikisha kinaleta faida kubwa zaidi ya mkopo wenyewe kujumlisha na riba.
Mkopo hauui biashara, ila wewe mwenyewe ndio unaua biashara yako. Kama utachukua mkopo kwa wakati sahihi na ukautumia kwa lengo lile ulilochukulia basi biashara yako itakwenda vizuri. Na hata kama kuna matatizo yaliyoko nje ya uwezo wako yatakayotokea, kama biashara yako inafanya vizuri bado utaweza kulipa mkopo uliochukua.
Mkopo ni mzuri kwa biashara yako, kama utauchukua kwa wakati sahihi na kuutumia kwa matumizi sahihi, kinyume na hapo mkopo utakuwa sumu kwa biashara yako.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA.