Daima namshukuru mungu kwa namna ya pekee kwa kadri anavyozidi kutubariki na hata kupata wasaa huu wa kuelimishana na watanzania wenzangu. Pia nawashukuru wasomaji wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa namna ambavyo wamepata mwamko huu wa kutaka kupata ufahamu zaidi kuhusu uwekezaji wa amali za majengo hapa nchini. Nina mengi ya kukushirikisha lakini Leo nataka ufahamu mambo muhimu yanayoathiri gharama za ujenzi na namna ya kupanga mipango bora kabla hujajenga unachotaka kujenga. Mambo haya yatakusaidia kufanya tathmini za gharama na hatimaye kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji kwa kuzingatia muda na mzunguko wako wa fedha.
SOMA; Ili Upate Mafanikio Ya Kudumu, Wekeza Kwenye Ardhi Na Majengo.1. Hali ya uchumi
Hali ya uchumi wa nchi ni jambo lenye athari kubwa hasa kwa mwananchi wa kawaida katika kuendesha maisha yake. Gharama za ujenzi wa nyumba hutegemea sana hali ya uchumi wa nchi kutokana na matumizi mengi ya rasilimali na uzalishaji mvutano. Pia mfumuko au kudorora kwa uchumi ni hali inayoathiri thamani ya fedha ya ndani ukilinganisha na fedha za nchi za kibiashara ambazo kwa kiasi kikubwa tunategemea malighafi kutoka nchi hizo. Endapo uchumi utaimarika gharama zitapungua kutokana na ukuaji wa uzalishaji wa malighafi za ujenzi na huduma za jamii kama vile umeme na maji. Hivyo upatikanaji rahisi wa malighafi za ujenzi hupunguza gharama za ujenzi. Pia ndani ya uchumi imara hata mzunguko wa fedha huwa mkubwa hasa kwa wale walio ndani ya mfumo wa biashara hatimaye kila mtu anakuwa na uhakika wa mapato, matumizi na uwekezaji.
2. Upatikanaji wa malighafi za ujenzi
Mara nyingi uhaba wa malighafi za ujenzi husababisha gharama kuwa juu zaidi. Ni vema kufanya maandalizi kabla ya ujenzi kuhakikisha kuwa malighafi za ujenzi zipo kiasi Fulani kutoka mahali Fulani na kwa gharama kadhaa. Pia ni vema kupangilia manunuzi ya malighafi ili kudhibiti gharama za usafirishaji. Gharama zako zitakuwa chini endapo utakuwa umeweka mipango na makadirio makini ili kudhibiti matumizi mabaya ya malighafi na wizi ambao hufanywa na wajenzi wasio waaminifu.
3. Mfumo wa ujenzi na Ukubwa wa nyumba husika
Ukubwa wa nyumba huathiri gharama za ujenzi, nyumba kubwa huwa na gharama kubwa zaidi, pia mfumo wa ujenzi, mpangilio wa vyumba na njia au dhana zitakazotumika kwenye ujenzi hufanya gharama kuwa juu au chini. Hivyo ni muhimu sana kuwa na mipango madhubuti kabla na wakati wa ujenzi ili upate nyumba bora na kwa gharama nafuu zaidi. Zungumza na wataalamu kuhusu mpango wako wa ujenzi na namna ambavyo unatarajia kupata nyumba itakayokidhi matakwa yako.
SOMA; Kama Unataka Kufanikiwa Achana Na Demokrasia Na Kuwa Dikteta.
4. Mandhari ya mazingira husika.
Mazingira husika ya ujenzi wa nyumba huathiri gharama katika ujenzi wa nyumba kutokana na kulazimisha baadhi ya ubunifu kufanyika ili nyumba iweze kuhimili mapambano ya mandhari husika. Ujenzi huzingatia sana mazingira ambayo husababisha utofauti katika ubunifu wa nyumba, malighafi na dhana utakazotumia wakati wa ujenzi. Mfano maeneo ya mabondeni na milimani huhitaji msingi mzito wenye usawazo tofauti na eneo tambarare, pia maeneo yenye chemchemu huhitaji malighafi zaidi ili kuzuia maji yasiathiri nyumba husika. Pia mpangilio na namna ya ukwepaji wa miundombinu husika huongeza gharama za ujenzi. Hivyo ni muhimu sana ukalitambua hili, wengi wamelalamika wakisema ‘’ramani ya nyumba ni moja kwa nini gharama ni tofauti ikiwa wajenzi ni walewale’’ tofauti za gharama hutokana na mambo yote niliyo orodhesha katika makala hii.
5. Muda utakaotumika
Ujenzi wa nyumba ni sawa na uzalishaji wa bidhaa kwenye viwanda, hata kwenye ujenzi muda ni rasilimali inayozingatiwa sana katika kuongeza au kupunguza gharama husika. Endapo nyumba itachukua muda mrefu kukamilika italazimu wajenzi kulipwa zaidi na kupata huduma zaidi kama vile chakula na malazi au usafiri kutokana na muda watakaokuwepo wakati wa ujenzi. Hata dhana utakazotumia wakati wa ujenzi huathiriwa sana na muda ili kukidhi ubora unaotakiwa, pia endapo utatumia mashine za kutumia nishati ya umeme au mafuta gharama huwa juu tofauti na kutumia kwa muda mfupi. Hivyo ni muhimu sana kujipanga kwa kila hatua ya ujenzi kwa kuzingatia makadirio ya fedha na upatikanaji wa malighafi kwa kuzingatia muda husika ili kupunguza gharama zisizo na ulazima. Ujenzi huhitaji mipango na mikakati madhubuti katika kufikia malengo.
Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888, Email: kimbenickas@yahoo.com

Kuhakikisha unapata makala za AMKA MTANZANIA moja kwa moja kwenye email yako kila zinapotoka BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UWEKE EMAIL YAKO.