Tukiweka unafiki pembeni, mambo mengi tunayofanya kwenye maisha yetu tunayafanya tukiwa na ajenda fulani. Mara nyingi umekuwa unafanya kitu au kukubali kitu kwa sababu unajua matokeo yatakayotokea baada ya hapo yatakunufaisha kwa kiasi fulani.

Vizuri sana kama una hisia hizi, kwa sababu umedhibitisha kwamba ni binadamu. Ila unakuwa binadamu wa kawaida. Na leo nataka nikupe mbinu ambayo itakufanya uache kuwa wa kawaida na uwe wa kipekee, uwe tofauti na uweze kufanya makubwa.
Siri hiyo ni kwamba fanya chochote unachofanya bila ya kuwa na ajenda yoyote. Fanya kwa sababu ndio unachotaka kufanya, hata kama hakuna anayekuangalia bado ungefanya, hata kama kila mtu angekupiga bado ungefanya na hata kama hupati fedha bado ungefanya.
Kama tulivyokubaliana kwamba tunafanya mambo yetu tukiwa na ajenda, na ninaamini kwamba unakubaliana na mimi kwamba sisi wote sio watabiri wazuri wa kesho. Kama hukubaliani na hilo soma hapa kwanza; wewe sio mtabiri mzuri, acha kujiumiza.
Sasa kinachotokea ni kwamba, ile ajenda uliyokuwa nayo, maana yake ulitabiri kesho itakuwa hivi. Na kwa kuwa wewe sio mtabiri mzuri haitokei kama ulivyopanga ingetokea. Kinachotokea ni nini? Unaumizwa moyo, unakata tamaa, unaona maisha ni magumu na mengine mengi.
Ulifikiri kwa kuoa/kuolewa na mtu fulani kungeleta maisha ya furaha unapata kinyume chake. Ulifikiri kwa kuonekana unamkubali sana mtu mwenye nafasi fulani atakusaidia na wewe kufika mbali, anakusahau. Ulifikiri kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kuliko wengine utapandishwa cheo, unashangaa mtu aliyekuwa mzembe ndio anapandishwa cheo. Na mengine mengi ya maisha.
Vipi kama usingekuwa na ajenda? Unaoa au kuolewa kwa sababu umepata mtu mnayependana na mtaheshimiana mkiwa pamoja? Vipi kama utakuwa karibu na mtu sio kwa sababu atakusaidia bali wewe unafurahi kuwa sehemu ya msaada kwake? Vipi kama kufanya kwako kazi kwa juhudi na maarifa, sio kwa sababu utapandishwa cheo, ila kwa sababu ndio kinakufanya uone umetoa mchango wako hapa duniani?
Maisha yako yangekuwa bora sana, na mafanikio yangefuata bila hata ya kujiumiza na hali za kukatisha tamaa.
Lakini sisi ni binadamu, ni vigumu kutokuwa na ajenda kabisa, na hivyo kujiandalia huzuni na kukatishwa tamaa hapo mbeleni.
Ila ukiacha na mawazo hayo hapo juu, na ukakazana kufanya mabadiliko kidogo kwenye maisha yako, utapunguza kuwa na ajenda nyingi.
Kama mimi nilivyopunguza na kuandika makala hii bila ajenda yoyote, sitegemei kwamba utajiunga na KISIMA CHA MAARIFA kwa sababu umesoma hapa. Sitegemei kwamba utanunua vitabu vyangu kwa sababu umesoma hapa. Ila kama hilo litatokea, itakuwa ni sehemu ya ujumbe huu kumfikia mlengwa.
Naamini kwa kusoma hapa kuna kitu kimeongezeka kwako, na utapunguza maumivu ya maisha yako, na utaongeza uzalishaji wako, na utakuza uchumi wa nchi, halafu wote tutafaidika. Hiyo nayo ni ajenda eh! Kila la kheri.
TAMKO LA LEO;
Najua kufanya mambo kwa ajenda ndio kumekuwa kunaniletea maumivu na kukata tamaa. Najua kufanya mambo kwa ajenda ndio kumenikosesha mafanikio. Kuanzia leo naamua kufanya jambo kwa sababu ndio kitu nilichotayari kufanya, iwe kuna kitu napata au la.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.