MAMBO 20 NILIYOJIFUNZA KWENYE KITABU EAT MOVE SLEEP.
Maisha yetu yanatokana na maamuzi tunayofanya kila siku kwenye maeneo haya matatu muhimu kwenye maisha,
UNAKULA NINI,
UNALALA VIPI
UNAFANYA MAZOEZI KIASI GANI.
1. Unachokula ndio kinakujenga au kukubomoa. Magonjwa mengi yanayotusumbua sasa yanatokana na vyakula tunavyokula kila siku. Kuwa mwangalifu sana na vyakula unavyokuka, vinaweza kuwa sumu kubwa sana kwako.
2. Unahitaji muda wa kutosha wa kulala. Usingizi ni muhimu sana kwa afya yako na hata uzalishaji wako kwenye kazi. Kukosa muda wa kupumzika ni chanzo kikubwa cha matatizo mengi ya kiafya na hata uzalishaji mdogo.
3. Je mwili wako unapata mazoezi ya kutosha? Mazoezi ni muhimu sana kwa afya yako na hata uzalishaji wako. Unapofanya mazoezi unatumia vyakula ulivyokula na hivyo kupunguza matatizo ya kiafya. Pia unakuwa na nguvu nzuri ya kuweza kufanya kazi vizuri na pia utapata usingizi mzuri.
4. Kuvuruga kitu kimoja kati ya hivi vitatu kunaleta mvurugano kwenye vingine vyote.
Kwa mfano kula vyakula visivyo vya afya kunafanya mwili wako kuchoka na hivyo kushindwa kufanya kazi zako, kukosa usingizi na hata kushindwa kufanya mazoezi.
Kukosa usingizi kunakufanya uamke umechoka, kushindwa kufanya mazoezi na kujikuta unakula hovyo.
Usipofanya mazoezi vyakula unavyokula havitumiki na hivyo kuwa ha afya mbovu.
Nenda na vitu hivi vitatu kwa uwiano.
KULA VIZURI,
PATA USINGIZI WA KUTOSHA,
FANYA MAZOEZI.
5. Haijalishi afya uliyonayo leo bado unaweza kufanya maamuzi ambayo yatapelekea wewe kuwa na nguvu za kutosha na kuweza kuishi umri mrefu.
Haijalishi umri wako ni kiasi gani, unaweza kuchukua hatua ndogo ndogo kwa jinsi unavyokula, jinsi unavyolala na jinsi unavyofanya mazoezi na maisha yako yakawa bora na marefu.
Chukua hatua leo, huhitaji kufanya mambo makubwa mara moja, bali mambo madogo madogo kila siku.
6. Kuianza siku yako kwa kupata kifungua kinywa kizuri, kunaifanya siku yako kuwa nzuri na kuwa na nguvu kwenye masaa yanayofuata. Hii itakuwezesha kula vizuri pia mchana na jioni ja hivyo kuwa na usingizi mzuri. Unapolala vizuri unaamka ukiwa na nguvu mpya na kuianza siku nyingine vizuri pia.
Ila ukiianza siku vibaya au kwa kula hovyo, unaharibu kila kitu.
7. Kama unataka kubadili afya yako kwa kubadili chakula, labda unataka kupunguza uzito, unapoanza kula tofuti, unahitaji muda mrefu ndio uone majibu unayotarajia. Kama utakata tamaa haraka kwa sababu huoni mabadiliko, utajaribu vyakula vingi sana na afya yako itabaki pale pale.
Unahitaji muda kurekebisha mwili wako.
Mtu akikuambia njoo nikupe dawa ya kupunguza unene ndani ya mwezi mmoja, kimbia haraka, maana anataka kukutapeli.
8. Kufanya mazoezi kwa wakati fulani tu haitoshi. Kufanya mazoezi mara moja kwa siku ni kujidanganya. Kama utafanya mazoezi saa moja halafu unakaa na kulala masaa 23 bado afya yako ipo hatarini.
Unachohitaji ni mwili wako kuwa na mazoezi siku nzima. Usikae sehemu moja kwa muda mrefu, ushughulishe mwili wako.
9. Kwa wastani, watu wengi tunatumia muda mwingi kukaa kuliko hata kulala.
Unaamka asubuhi, unaenda kazini, umekaa kwenge gari, ukifika unakaa kwenye kiti karibu siku nzima, unakaa tena kwenye gari kurudi nyumbani, ukifika unakaa tena kwenye kochi kuangalia tv.
Mwili wa mwanadamu haujajengwa kwa aina hii ya maisha, unahitaji kushughulisha sana mwili wako. Kufanya mazoezi kwa nusu saa au saa moja hakutoshi kukabiliana na muda huu mwingi unaokaa.
10. Kubakikisha mwili wako u apata mazoezi ya kutosha, usikae sehemu moja kwa muda mrefu. Kila baada ya muda, simama na zunguka kidogo kisha urudi. Kama kazi imekubana sana na unaweza kusahau, kunywa maji mengi, utabanwa na mkojo mara kwa mara ma hivyo utahitaji kwenda kukojoa, haya yatakuwa mazoezi pia.
11. Kupunguza saa moja ya kulala sio sawa na kuongeza saa moja ya uzalishaji. Badala yake ni kinyume. Kupunguza saa moja ya kulala, ukifikiri unafanya kazi, unakuwa umepunguza muda wa wewe kuwa na uzalishaji mzuri.
Kukosa usingizi kunapunguza umakini wako kwenye kazi na unaweza kufanya makosa mengi.
12. Kama unataka kuongeza saa yako moja ya uzalishaji, ongeza saa moja ya kulala. Usifanye kazi moja kwa muda mrefu, igawe kwenye makundi madogo madogo na ifanye kwa kipindi kifupi. Pata muda wa kupumzika na kuzungusha mwili wako pia.
13. Kukaa ni hatari kubwa sana kwa magonjwa kwenye ulimwengu wa sasa.
Kukaa ni hatari kuliko hata kuvuta sigara, inasemekana kukaa ndio sigara ya karne hii, maana wengi wanapata magonjwa ya presha, kensa na kisukari kutokana na kukaa muda mrefu.
Kukaa masaa sita mfululizo kila siku kutakupelekea kufa kabla ya muda wako.
14. Kama kazi yako ni ya kukaa siku nzima kama kazi za ofisi basi unahitaji kufanya mabadiliko ili ujiepushe na kifo unachojitengenezea.
Moja ya mabadiliko unayoweza kufanya ni kufanya kazi ukiwa umesimama. Unaweza kununua madawati ya kusimama na kufanyia kazi zako pale. Kusimama ni bora kuliko kukaa.
Pia unaweza kuwa na mapumziko ya mara kwa mara kwenye kazi yako ili kuepuka kukaa muda mrefu.
15. Kula mlo utakaoendana na maisha yako. Kama unafanya kazi za ofisini ambapo hutumii nguvu epuka sana mafuta na sukari. Kula protini kwa wingi.
Vyakula vya wanga, sukari na mafuta visipotumika mwilini vinageuzwa kuwa mafuta ambayo yanahifadhiwa kwenye mwili na hivyo uzito kuongezeka. Hii inakuletea hatari ya kupata kisukari, ugonjwa wa moyo na kansa.
16. Sukari ni sumu kwenye mwili wako.
Sukari inachochea kisukari,
Sukari inaharakisha kansa,
Na sukari inaleta magonjwa ya moyo.
Sukari inaua watu wengi kuliko hata madawa ya kulevya,
17. Kadiri unavyokula sukari kwa wingi unaupa mwili wako nguvu ya kufanya mashambulizi na hii inapelekea wewe kuzeeka haraka.
Hakuna sababu ya kuongeza sukari ya ziada zaidi ya ile inayopatikana kwenye vyakula vya asili.
18. Epuka sana vyakula vinavyotengenezwa viwandani. Vina vitu vingi ambavyo sio vizuri kwa afya yako.
Kula vyakula vya asili kunaufanya mwili wako kuwa na kinga nzuri ya kupambana na magonjwa na pia sio rahisi kuongezeka uzito.
19. Tembea angalau hatua elfu kumi kwa siku. Wengi wetu tunatembea chini ya hatua elfu tano ambayo sio nzuri kiafya. Hakikisha unatembea angalau hatua elfu kumi. Kama una simu janja(smartphone) weka aplication inayoweza kupima ni hatua ngapi umetembea kwa siku. Na kazana kuziongeza kila inapobidi.
Kwa mfano panda ngazi badala ya lift.
20. Kukosa muda wa kulala kunaufanya mwili kushindwa kutengeneza kinga, na hivyo mwili unakuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa kama kansa na pia mwili unakuwa hivyo hivyo kujikuta unakula hovyo na kuongezeka uzito.
Hakikisha unapata usingizi wa kutosha na mwili wako unaamka ukiwa na nguvu.
HITIMISHO;
Maamuzi madogo madogo unayofanya kwenye afya yako kila siku ndio yanayopima maisha yako yatakuwa wapi miaka ijayo.
Fanya maamuzi sahihi kwenye KULA, KULALA NA KUFANYA MAZOEZI na utakuwa na maisha bora, yenye mafanikio na utaishi muda mrefu.