Watu huwa wanalalamika kwamba kuleta mabadiliko kwenye maisha yao ni vigumu sana. Lakini sio kweli.

Sio kwamba ni vigumu kuleta mabadiliko, ila mpango wetu wa mabadiliko ndio unakuwa mgumu.

BADILI KITU KIDOGO KILA SIKU, BAADA YA MUDA MAISHA YAKO YOTE YATAKUWA YAMEBADILIKA.
BADILI KITU KIDOGO KILA SIKU, BAADA YA MUDA MAISHA YAKO YOTE YATAKUWA YAMEBADILIKA.

Kwa mfano mtu anapanga kubadili milo yake ili awe na afya bora. Anaanza kula vizuri leo halafu anategemea kesho awe na afya bora, hiki ni kitu ambacho hakiwezi kutokea.

Au mtu anapanga kufanya mazoezi, halafu anataka siku moja aweze kukimbia sana au kufanya mazoezi makubwa siku ya kwanza na kila siku.

Au mtu anaamua kujijengea tabia ya kusoma na siku ya kwanza anataka asome nusu ya kitabu, au kitabu kizima kabisa.

Kwa mtizamo huu, itakuwa vigumu sana kufanya mabadiliko yoyote kwenye maisha yako.

Lakini unapokuwa na mtizamo kwamba unahitaji kufanya badiliko dogo sana kila siku, baada ya siku nyingi utakuwa mbali sana.

Kama umeamua kubadili mlo wako badili kitu kidogo kila siku na usikate tamaa.

Kama umeamua kujisomea, anza kwa kusoma ukurasa mmoja kila siku, au kurasa tano tu kila siku, ukifanya hivi kwa mwaka mzima utakuwa umesoma kurasa zaidi ya 1800, hii ni zaidi ya vitabu vitatu, asilimia 98 ya watu hawasomi zaidi ya kitabu kimoja kwa mwaka.

Kama umepanga kuanza mazoezi anza kwa kutembea hatua chache siku ya kwanza na kila siku ongeza hatua moja tu.

Kikubwa hapa ni wewe kuhakikisha kila siku unafanya kitu kidogo kinachokupeleka kwenye yale mabadiliko unayotaka.

Na unahitaji nidhamu kubwa kwa sababu kama utaikosa hiyo, hakuna utakachoweza kubadili kwenye maisha yako.

TAMKO LA LEO;

Najua ya kwamba mabadiliko hayatokei mara moja kwenye maisha yangu. Mabadiliko ni kitu ambacho nahitaji kufanya kila siku. Kuanzia sasa nitakuwa nafanya vitu vidogo vodogo kila siku bila ya kukata tamaa mpaka pale maisha yangu yatakapokuwa bora. Kujenga tabia ya kufanya kila siku ndio msingi wa mabadiliko. Nitahakikisha naimarisha nidhamu yangu ili niweze kuwa na maisha bora.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.