Kila mmoja wetu kuna vitu amekusudiwa kufanya hapa duniani.

Tuna uwezo na vipaji tofauti tofauti na hivyo kuweza kufanya vitu tofauti.

Mafanikio makubwa yanakuja pale mtu anapofanya kile ambacho amekusudiwa kufanya, kile ambacho kinaendana na uwezo wake na hata vipaji vyake.

Lakini kwa bahati mbaya sana, huwa hatuzaliwi na karatasi ya maelezo, kwamba mtu huyu anatakiwa kufanya kitu fulani na fulani.

JE KILE UNACHOFANYA NDIO KINAKUPA HAMASA, FURAHA NA AMANI YA MOYO? KAMA NDIO UMESHAJUA ULICHOKUSUDIWA KUFANYA, KAMA BADO ENDELEA KUTAFUTA.
JE KILE UNACHOFANYA NDIO KINAKUPA HAMASA, FURAHA NA AMANI YA MOYO? KAMA NDIO UMESHAJUA ULICHOKUSUDIWA KUFANYA, KAMA BADO ENDELEA KUTAFUTA.

Hivyo kujua ni kitu gani cha kufanya linabaki kuwa jukumu letu wenyewe.

Kwa bahati mbaya tena tumekuwa tunaruhusu jamii ituambie ni kitu gani tunaweza kufanya au kipi hatuwezi kufanya. Lakini ukweli ni kwamba sisi wenyewe ndio tunaoweza kuamua jambo hilo.

Sasa je unawezaje kujua kama hiko unachofanya sasa ndio ulichokusudiwa kufanya?

Kuna njia rahisi sana ya kujua hilo, na njia hiyo ni kupima kiwango cha furaha na hamasa uliyonayo wakati unafanya kitu hiko.

Kama unapata furaha kubwa unapofanya kile unachofanya basi ndio ulichokusudiwa kufanya. Kama unakuwa na hamasa kubwa ya kukifanya kwa ubora mkubwa ndio kitu unachotakiwa kufanya hiko. Na kama unajisikia amani kwa kufanya kitu hiko basi upo kwenye njia nzuri.

Lakini kama kile unachofanya hakikupi furaha, hamasa na amani ya moyo, sio ulichokusudiwa kufanya.

Na kama kile unachofanya sio ulichokusudiwa kufanya usikasirike, bado unao muda w akutosha wa kuweza kujua ni kipi umekusudiwa kufanya. Kaa chini na kufikiria ni vitu gani unapenda kufanya, ni vitu gani ungependa kuona viko bora.

Lakini nahitaji kupata fedha za kuendesha maisha, ndio kila mtu anajua hilo. Hivyo ukishajua kile ulichokusudiwa kufanya, fikiria ni kwa njia gani watu wanaweza kukulipa kwa wewe kufanya kitu hiko. Sio lazima uache kila unachofanya sasa ili kuanza kufanya kitu hiko, bali anza kidogo kidogo kama kitu cha pembeni. Na kadiri siku zinavyokwenda endelea kuboresha jinsi unavyofanya na kuangalia njia za kuweza kulipwa kwa kile unachofanya.

TAMKO LA LEO;

Najua kuna kitu ambacho nimekusudiwa kufanya. Kwa uwezo wangu wa kipekee na vipaji nilivyonavyo kuna vitu ambavyo naweza kuvifanya vizuri sana. Kujua kama ninachofanya ndio nilichokusudiwa kufanya nitaangalia furaha ninayoipata pale ninapofanya kile ninachofanya. Kama sio nilichokusudiwa, nitatenga muda wa kuendelea kutafuta kile nilichokusudiwa kufanya na kuangalia ni jinsi gani ambavyo watu wanaweza kunilipa kwa kufanya kitu hiko.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.