Sehemu kubwa sana ya vikwazo vinavyokuzuia wewe kuishi yale maisha unayotaka vinatoka ndani yako mwenyewe. Hakuna mtu mwingine anayevisababisha ila wewe mwenyewe.

Umekuwa unapanga vizuri kabisa ya kwamba utafanya kitu fulani, lakini unakuja na lakini ambazo unaweza kujishawishi vizuri sana. Unajishawishi ya kwamba kwa sasa hutaweza kwa sababu fulani na fulani unazojipa wewe mwenyewe. Zinaweza kuwa sababu makini kabisa au zikawa sababu zisizo makini. Kikubwa ni kwamba wewe ndio unaweka vikwazo hivyo.
Ubaya wa kujiwekea vikwazo wewe mwenyewe ni kwamba inaua kabisa juhudi zako na hata ubunifu wako. Unapokuja na sababu tu basi, hutaendelea kujaribu tena. Utaacha kufanyia kitu kazi na hatimaye huwezi kuona mabadiliko uliyotarajia kwenye maisha yako.
Na unapokuwa mtu wa sababu, kujiwekea vikwazo, kila mara utapata sababu ya kwa nini haiwezekani kwa wewe kufikia kiwango fulani au kufanya kitu fulani. Hata kama watu watakusisitiza vipi, bado utaamini ya kwamba wewe kwa sasa huwezi kwa sababu ambazo umejipa wewe mwenyewe.
SOMA; UKURASA WA 114; Tumia Vikwazo Ulivyonavyo Kufikia Mafanikio.
Acha sasa kuendelea kujiwekea vikwazo. Unapofikiri kufanya kitu, usianze tena kufikiria kwa nini haitawezekana au umekosa nini kwa sasa. Bali peleka akili yako yote kufikiria ni jinsi gani itawezekana kufanya au kufikia unachotaka. Unapofikiri ni jinsi gani itawezekana utapata njia nyingi sana za kuweza kufanya. Unaposema kwamba haiwezekani, utapata kila sababu kwa nini haiwezekani au kwa nini wewe hutaweza kwa sasa.
Hebu kwa mara ya kwanza kwenye maisha yako fikiria kwamba kitu kinawezekana, ondoa kabisa vikwazo unavyojiwekea mwenyewe. Acha kabisa kusikiliza wengine wanasema nini na ifikirishe akili yako ni jinsi gani unaweza kufikia kile unachotaka. Akili yako ina uwezo wa ajabu sana. Utashangaa itakuletea njia nyingi ambazo hukuwahi hata kufikiri.
Yote haya yanaanza pale ambapo unaacha kujiwekea vikwazo wewe mwenyewe.
TAMKO LA LEO;
Najua nimekuwa najiwekea vikwazo mimi mwenyewe, mambo mengi niliyokwama kukamilisha ni kutokana na vikwazo nilivyojiwekea. Nimekuwa naweka mipango mizuri sana, lakini baada ya hapo nimekuwa nakuja na sababu kwa nini sitaweza kwa sasa au ni vitu gani vinanizuia. Kuanzia sasa naachana na sababu hizi. Wakati wowote ambao nitapanga kufanya kitu, nitaondokana na fikra za vikwazo na nitafikiria ni njia gani ninazoweza kutumia ili kufikia kile ninachotaka. Najua akili yangu itanipa majibu mengi sana.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.