Kwanza kabisa naomba nikiri ya kwamba mimi ni mwinjilisti mzuri wa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Naamini kwenye kazi kama ndio msingi mkuu wa maendeleo na mafanikio. Naamini ni kupitia kazi bora ndio tunaweza kujenga jamii bora na yenye maendeleo. Naamini ya kwamba ni kazi ndio inaleta maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla. Naamini bila ya kuyumbishwa kwamba sio kazi tu, bali kazi ya kipekee ndio inayoleta mafanikio makubwa kwa mtu yeyote anayeifanya.
Siamini kwamba kuna njia ya mkato ya kufikia mafanikio ya kudumu ambayo haihusishi kazi. Siamini kwamba misaada inaweza kumletea mtu mafanikio kama mtu huyo hayupo tayari kufanya kazi. Na pia siamini kwamba kufanya kazi kwa kawaida kunaweza kumletea mtu mafanikio makubwa.

WEKA TIJA KWENYE KAZI UNAYOFANYA.

 
Pamoja na haya yote ambayo tunayajua kuhusu kazi, kuna watu ambao wanafanya kazi sana, lakini bado maisha yao ni magumu. Kuna watu wapo kwenye kazi kwa miaka kumi, wengine ishirini na wengine zaidi ya hapo, lakini hakuna kitu kikubwa wanachoweza kuonesha kutoka kwenye kazi hiyo. Tatizo ni nini kwenye hali hii? Au kazi inaleta mafanikio kwa wengine na haileti kwa wengine?
SOMA; Kitu Kimoja Kitakachoongeza Wasifu Wako(Cv) Na Kukuongezea Kipato Pia.
Hapa tutajadili baadhi ya tabia zetu na fikra zetu ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio japo tunafanya kazi sana.
1. Kufikiri unafanya kazi kwa akili na sio nguvu.
Kuna usemi maarufu wa kiingereza unasema kwamba work smart not hard. Ukimaanisha fanya kazi kwa akili na sio nguvu. Usemi huu umewapotosha watu wengi sana na kuamini ya kwamba ukishakuwa na akili, au ukishakuwa mtaalamu basi huhitaji tena kutumia nguvu kufanya kazi. Usemi hii na semi nyingine kama hizi zinawafanya watu wenye elimu kubwa kuona ya kwamba elimu yao pekee ndio inayohitajika kwenye kazi na hivyo kukwepa kazi zote ambazo zinatumia nguvu.
Ukweli ni kwamba hakuna kazi ambayo haitumii nguvu. Hata kama ungekuwa unatumia akili nyingi kiasi gani, ni lazima utumie nguvu pia. Hata kama wewe ndio msimamizi wa kazi, bado kazi haiwezi kwenda kwa sababu wewe ndio unatoa mawazo na kukaa ofisini kwako. Ni lazima uwepo eneo la kazi, ni lazima uoneshe kwa mfano ni kitu gani ambacho unataka kifanyike.
Mtazamo huu wa kufanya kazi kwa akili umewafanya wengi kushindwa kufikia mafanikio hasa kwenye kazi zao binafsi. Watu wanaoanzisha biashara kwa mtazamo huu wamekuwa wanajikuta kwenye wakati mgumu sana na hivyo kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea.
Badala ya kuamini kwamba unahitaji kufanya kazi kwa akili tu na sio nguvu, leo nakushauri uamini kwamba unahitaji kutumia vyote akili na nguvu. Kwa kiingereza tuseme work hard and smart, yaani fanya kazi kwa nguvu na akili(mimi napenda kutumia fanya kazi kwa juhudi na maarifa.) akili ni muhimu sana ili usije kutumia nguvu nyingi kwenye kitu ambacho hukutakiwa hata kukifanya, au kitu ambacho ungeweza kutumia nguvu kidogo.
JUHUDI NA MAARIFA ni muhimu sana kwenye kazi yoyote unayofanya, ukiacha kimoja kati ya hivyo unajiandaa kushindwa kwenye kazi hiyo.
SOMA; Njia Tatu Za Kuongeza Ufanisi Wako Eneo La Kazi Na Kuepuka Kupoteza Muda Kwa Hadithi Zisizo Na Msaada Kwako.
2. Kufanya kazi kwa mazoea.
Hakuna kikwazo kikubwa cha mafanikio makubwa kwenye kazi kama kufanya kazi kwa mazoea. Watu wengi waliokaa kwenye kazi muda mrefu, hushangaa kwa nini vijana wanaoingia kwenye kazi hizo wanawazidi wao kwa ufanyaji wa kazi. Wao hujua ya kwamba ni wazoefu na wanajua kila kitu. Lakini wanasahau kwamba vijana wanaokuja wanakuwa na ubunifu na njia tofauti za kufanya kazi hiyo. Wakati wao wanaendelea kufanya kwa mazoea.
Kufanya kazi kwa mazoea ndio chanzo namba moja cha watu kutopenda kazi zao na kutopenda kazi ndio chanzo namba moja cha kushindwa kufikia mafanikio. Unapofanya kazi ile ile kila siku, na kwa mtindo ule ule, inachosha na kukera. Kwa sababu unajua kabisa hapa unafanya hiki na baada ya hiki kinakuja kile. Unaona kama maisha yako hayana kitu kipya zaidi ya kazi hiyo unayofanya kila siku. Hii inapelekea mtu kuchukia kazi anayoifanya na hivyo kukufanya usifikie mafanikio makubwa.
Unapoleta ubunifu na utofauti kwenye kazi yako unaleta hamasa mpya kwenye kazi hiyo na mara zote utakuwa na shauku ya kufanya kazi ili uendelee kuweka juhudi kubwa zaidi. Utakuwa na shauku ya kujaribu vitu vipya na vitu hivi vipya ndio vitakavyokuwezesha wewe kufikia mafanikio makubwa.
Kama umekuwa unafanya kazi yako kwa mazoea, hebu anza leo kuleta ubunifu na utofauti kwenye kazi hiyo, hebu tafuta njia ambazo unaweza kuigeuza kazi hiyo kuwa kama mchezo. Kwa sababu michezo huwa inakuwa na hamasa kubwa sana, hakuna mtu ambaye amezoea mchezo wowote, hii ni kwa sababu kuna mambo mengi mapya yanaweza kutokea kwenye mchezo. Jaribu vitu ambavyo vitakufanya wewe ufikiri tofauti, weka malengo ambayo yatakusukuma zaidi na pia jiulize kila siku ni kitu gani unachoweza kuboresha zaidi kwenye kazi unayofanya, hata kama ni kidogo, kifanyie kazi.
SOMA; Tabia Tano(5) Za Wafanyakazi Ambao Ni Sumu Kwenye Eneo La Kazi Na Jinsi Ya Kuepuka Kuwa Mmoja Wao.
3. Kufanya kazi kusiko na tija.
Kuna usemi unasema kwamba kama kufanya kazi kwa nguvu kungekuwa ndio mafanikio basi punda wangekuwa mbali sana.
Usemi mwingine unaenda na picha inayomwonesha mwanamke wa kiafrika akiwa na mizigo kichwani na mtoto mgongoni halafu usemi unakwenda, kama kufanya kazi kwa nguvu ingekuwa ndio mafanikio basi wanawake wote wa kiafrika wangekuwa mabilionea.
Huwa naishia kucheka tu kwa semi hizi kwa sababu yeyote anayeziamini atakuwa ni mtu mvivu, hata wa kufikiri tu. Mifano yote miwili ambayo imetolewa hapo juu inaonesha ufanyaji kazi usio na tija.
Punda anafanya kazi sana, lakini kazi hiyo haina tija yoyote. Punda atabeba mzigo sio kwa sababu anajua mzigo huo una manufaa gani kwake, bali kwa sababu amebebeshwa mzigo huo. Kuna watu wengi sana wanaofanya kazi zao kama punda. Mtu anafanya kitu hajui ni kwa sababu gani anafanya, ila anafanya tu kwa vile ndio kila mtu anafanya au ndio majukumu yake ya kazi. Katika kazi yoyote ile unayofanya, kama unataka iwe ya tija, jua ni kwa nini unaifanya. Unapokuwa na sababu ya kufanya kazi yoyote unayofanya inakuwa rahisi kwako kuiboresha zaidi ili kufikia lile lengo.
SOMA; Sehemu Kubwa Ya Watanzania Hatufanyi Kazi, Na Hili Ni Tatizo Kubwa Kwa Maendeleo.
Tukienda kwenye mfano wa mwanamke wa kiafrika ambaye ana majukumu mengi sana lakini bado ni masikini, bado tunaona kitu kile kile, ukosefu wa tija. Ni kweli utawaona wakifanya kazi nyingi sana na kutumia nguvu nyingi, lakini sio kwa sababu wamepanga kufanya hivyo bali kwa sababu wamezoea kufanya hivyo. Ni wachache sana wanaokaa chini na kufikiria njia za kuboresha maisha yao, au jinsi ya kufanyia kazi majukumu yao kwa kupunguza yale ambayo sio ya msingi kwa wakati huo. Wao hufanya kile ambacho wamezoea kufanya hata kama wangeweza kubadili na kuboresha zaidi.
Mambo hayo matatu yamekuwa yanakuzuia wewe kufikia mafanikio licha ya kuweka nguvu kubwa kwenye kazi unayofanya. Anza sasa kuleta mabadiliko kwenye kazi zako na uzifanye kwa juhudi na maarifa, uweke ubunifu na ziwe na tija. Hii itakuwezesha wewe kufikia lengo lolote kubwa ambalo utajiwekea kwenye kazi utakayokuwa unafanya.
Fanya kazi, maana kazi ndio mkombozi pekee kwenye dunia tunayoishi sasa.
Nakutakia kila la kheri kwenye utekelezaji wa haya uliyojifunza hapa.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
0717396253