Habari za leo mpenzi msomaji?
Karibu kwenye mfululizo huu wa makala za FALSAFA MPYA YA MAISHA. Kupitia makala hizi utapata kujifunza na kujijengea falsafa ya maisha yako ambayo itakuwezesha wewe kuwa na maisha ya furaha na yenye mafanikio.
Lakini kabla hatujaingia ndani na kujifunza kutengeneza falsafa ambayo tutaishi nayo, ni vyema ukajua kwa nini unahitaji falsafa mpya kwenye maisha yako.
Kabla ya yote inaweza kuwa vyama kama utajua falsafa ni nini.
Kwa kuwa hapa hatujifunzi kwa lengo la kujibu mtihani, au kuonesha wengine kwamba tunajua sana, basi nitakushirikisha maana rahisi sana ya falsafa, ambayo kama ukiijua basi inakuwa rahisi kuifanyia kazi.
Falsafa ni aina au njia ya maisha ambayo mtu anachagua kuishi. Njia hii ya maisha inaweza kutokana na yeye binafsi au anaweza kuwa ameichukua kutoka kwa jamii inayomzunguka. Falsafa inahusisha imani ambayo mtu anaisimamia kwenye maisha yake, aina ya maisha ambayo mtu anaishi na hata jinsi anavyohusiana na wengine kwenye jamii.
Falsafa ambayo mtu anaiishi ina mchango mkubwa sana kwenye furaha ya maisha yake na hata mafanikio.
Je hapo ulipo una falsafa?
Ndio, kila mmoja wetu ana falsafa anayoiishi, iwe anajua hivyo au la. Kuna jinsi ambavyo unayaendesha maisha yako, kuna jinsi ambavyo unajua kipi ni sahihi na kipi sio sahihi. Kuna vitu ambavyo unaamini kwenye maisha yako.
Pamoja na kwamba kila mtu anaishi falsafa, lakini ni wachache sana ambao wanaijua kiundani ile falsafa wanayoishi. Wengi hujikuta wakiishi falsafa kwa sababu ndivyo jamii inavyoishi. Mambo mengi ambayo umekuwa unafanya, huwezi kuyaelezea au kuyatetea mbele za watu kwa sababu hujui kwa nini unafanya hivyo. Umekuta watu wanafanya na wewe umeendelea kufanya.
Kwa nini ni muhimu kuwa na falsafa mpya?
Kama tulivyoona hapo juu, kila mtu kuna falsafa anayoishi, lakini sehemu kubwa ya watu hatujui ni falsafa gani tunaishi. Hivyo ni muhimu sasa kuwa na falsafa mpya ambayo tutafanya vitu sio kwa sababu tumezoea kufanya, bali kwa sababu tunajua kwa nini tunafanya. Kufanya vitu kwa sababu umezoea hakuwezi kukuletea maisha ya tofauti, maisha ambayo ni bora kwako na yanya maana.
Pia ni muhimu sana kuwa na falsafa mpya kwa sababu falsafa ndio inatuletea furaha kwenye maisha na hata mafanikio. Kuna watu wengi ambao wanafanya kazi kwa juhudi sana lakini maisha yao yako hovyo, hawana furaha na pia hawana mafanikio. Hii inatokana na kwamba wana kila kitu ila wamekosa falsafa sahihi ya kuwafikisha kwenye maisha ambayo ni bora sana kwao. Kwa kuwa na falsafa mpya kutamwezesha kila mtu kufurahia maisha yake kwa kuwa na furaha na mafanikio makubwa kupitia kile ambacho anafanya.
Ni muhimu sana wewe kuwa na falsafa mpya ya maisha yako kwa sababu umekuwa ukilishwa falsafa ya uongo, falsafa ambayo haiwezi kukufikisha kule ambapo unataka kwenda. Ukichunguza maisha yetu ya kitanzania kwa undani, utagundua kwamba kuna falsafa ambazo sio rasmi lakini watu wanaziishi kila siku. Kwa kuishi falsafa hizi imekuwa kikwazo kwa watu wengi kuwa na maisha bora. Kwa mfano;
- Wizi, rushwa na ufisadi imekuwa kama ni maisha ya kawaida. Mtu haoni aibu wala roho yake haimsuti pale anapojihusisha kwenye mambo hayo. Kuna mtu anadai rushwa kama vile ni haki yake ya msingi. Hii sio falsafa nzuri ya kuendelea kuishi nayo.
- Falsafa ya kazi nayo imekuwa ni ya hovyo sana. Kila mtu anatafuta njia rahisi ya kupata mafanikio. Watu wengi wanafanya kiwango kidogo sana cha kazi ili waonekane tu ya kwamba wanafanya kazi, lakini uzalishaji wao ni mdogo sana ukilinganisha na uwezo ambao wanao. Bila ya falsafa mpya, itakuwa vigumu sana kwako kuweza kutoa mchango mkubwa kwenye kazi unayofanya.
- Uaminifu umekuwa kitu ambacho hakina thamani kabisa. Tunaishi kwenye jamii ambayo mtu anaweza kuahidi kitu chochote na asikifanye kwa sababu kuahidi hakuna uhusiano wowote na kutekeleza. Hii imeshakuwa kama ni kawaida na kila mtu anaona kudanganya ni maisha ya kawaida ya kila mtu. Wanasiasa wapo tayari kuahidi kitu ambacho hawawezi kutekeleza. Sasa sumu hii imesambaa mpaka kwenye kazi na biashara. Kila mtu anahidi lakini hakuna utekelezaji. Na vibaya zaidi sumu hii imekwenda mpaka kwenye familia na inaharibu familia nyingi sana. Mtu anaahidi wakati wa ndoa kwamba nitakuwa mwaminifu kwako mpaka siku ya kifo, lakini siku sio nyingi anavunja uaminifu huo. Ni kutokana na falsafa yetu mbovu leo hii neno mchepuko linaonekana ni kitu cha kawaida kwenye jamii yetu. Unahitaji falsafa mpya kuweza kuondoka kwenye maisha ya aina haya.
- Kuna mambo mengi sana ambayo ni ya hovyo lakini tunaendelea kuyaishi na kuyafanya kwa sababu tumeyapokea kutoka kwenye falsafa tunayoishi. Mambo kama kutokujiamini, kutokupenda kujifunza, kupenda kupata zaidi ya kile tunachotoa na kadhalika.
Kupitia falsafa hii mpya utapata nini?
Utapata nafasi ya kujifunza kuhusu maisha ya furaha na yenye mafanikio na jinsi unavyoweza kuishi maisha haya.
Utaweza kutengeneza na kuishi falsafa mpya ambayo lazima itakupeleka kwenye maisha bora.
Na pia utapata nafasi ya kujitathmini ili kujua kama unakoelekea ni kuzuri au kubaya kulingana na falsafa unayoishi.
ANGALIZO;
Falsafa hii mpya itakuletea mambo mengi ambayo hutayapenda, kwa sababu umekuwa unaishi maisha ya mazoea, unaweza ukashindwa kuelewa pale unapoona kabisa ya kwamba unachofanya umekuwa unapoteza maisha yako bure. Kuna wakati unaweza kufika na kuona miaka yako mingi uliyoishi ni kama ulikuwa hujui ni nini unafanya. Kama utachukia hali kama hizo napenda nikuambie mapema kabisa usiendelee kusoma mfululizo huu wa makala. Utaumia utakasirika kwa sababu ukweli huwa unauma. Lakini kama upo tayari kubadilika, kama upo tayari kuboresha maisha yako, basi upo sehemu sahihi kabisa.
Falsafa hii haitaingilia imani yako ya kidini. Imani ya kidini ni muhimu sana kwa kila mtu. Kupitia falsafa hii utaongeza mambo muhimu ambayo huenda huyapati kupitia imani ya kidini uliyonayo. Hivyo usihofu kwamba utatakiwa kubadili kile ambacho unaamini, badala yake utakiamini kwa ubora zaidi. Kwa sababu hata imani zetu, wengi hatujui kwa nini tunaamini hivyo, tulizaliwa kwenye imani hiyo, tumekulia huko na tunaendelea kuwa huko. Kupitia falsafa hii mpya ya maisha utaweza kutafakari umuhimu wa imani uliyonayo. Na kupitia falsafa hii mpya, hakuna imani bora zaidi ya nyingine, kwa sababu imani inamhusu sana yule anayeamini.
Karibu sana kwenye falsafa hii mpya ya maisha ili uweze kujenga maisha yenye furaha na mafanikio. Hakuna jambo lolote ambalo linashindikana kama kweli utaamua kulifanyia kazi.
Twende pamoja kwenye safari hii, utajifunza mengi na kuboresha maisha yako.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,