Wajasiriamali na wafanyabiashara wote tunajua ni jinsi gani ilivyo changamoto kuendesha biashara. Japokuwa wengi hufikiri kuendesha biashara ni kuwa na uhuru mkubwa, bado changamoto ni nyingi sana. Ni changamoto hizi ndio zinazuia wafanyabiashara wengi kukua na kusababisha wengine kushindwa kabisa.
Changamoto za kibiashara zinaweza kusababishwa na mambo mengi sana, matatizo ya wafanyakazi, matatizo ya wateja, matatizo ya wasambazaji, matatizo ya kiuchumi na mengine mengi. Lakini mengi ya matatizo haya huchimbuka kwenye eneo moja muhimu sana ambao wengi huwa hawalifanyii kazi. Eneo hili ni matumizi ya muda.
Wajasiriamali wengi ambao wameweza kuwepo kwenye biashara kwa muda sasa, wanaweza kupanga bajeti nzuri sana ya fedha zao. Wananua vizuri mzunguko wao wa fedha ukoje na wanaweza kuusimamia. Ila wanashindwa kupanga bajeti ya kitu kimoja muhimu sana, tena kuliko hata fedha. Kitu hiki ni muda.
Wajasiriamali wengi wamekuwa wakishindwa kupangilia muda wao vizuri na hivyo kujikuta wakifanya kazi kwa muda mrefu, wakikosa muda wa kupumzika na kuchoshwa sana na biashara wanazofanya. Japo wengi hufikiri kwa kuweka muda mwingi kwenye biashara zao ndio wanazikuza, lakini ukweli ni kwamba kama mjasiriamali unakosa muda wa kupumzika na kuwa na watu muhimu kwenye maisha yako, husaidii biashara yako bali unaiumiza. Kuendesha biashara huku umechoka ni vigumu kuweza kutoa huduma nzuri kwa wateja, kushirikiana na wengine vizuri na pia inapelekea kufanya maamuzi ambayo yanaweza kukuletea hasara.
Hivyo ni muhimu sana kwa kila mjasiriamali kuwa na bajeti ya muda wake, ajue anatumiaje muda wake wa siku na hata wa wiki nzima.
Kupanga bajeti ya matumizi ya muda ni muhimu sana kwa mjasiriamali kwa sababu itaongeza ufanisi na hata uzalishaji wake kwenye biashara. Katika wakati wowote ule unajiona kama huna muda wa kutosha, unaona una mambo mengi ya kufanya kuliko muda ulionao. Hapa ndipo unahitaji kuweka bajeti ya muda ambayo itakusaidia wewe kufanya vile ambavyo ni muhimu kwa ukuaji wa biashara yako.
Unawezaje kupanga bajeti ya muda wako ili kuongeza ufanisi kwenye biashara yako?
Kama ilivyo kwenye kupanga bajeti ya fedha, lazima ujue mapato na matumizi. Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye kupanga bajeti ya muda. Unahitaji kujua mapato na matumizi. Na changamoto ya muda ni kwamba mapato hayabadiliki ni yale yale, ila matumizi ndio yanabadilika. Hivyo kikubwa tutakachopanga hapa ni matumizi.
Unapopanga bajeti ya matumizi ya muda wako, panga bajeti mbili. Bajeti ya kwanza ni bajeti ya wiki. Wiki ina siku saba na siku ina masaa 24, hivyo kwa wiki unakuwa na masaa 168. Kwa kuyaangalia hivi unaweza kuona ni mengi la wiki inavyoanza na kuisha unaweza usijue muda huo umepotelea wapi.
Katika kupanga bajeti ya wiki, tenga muda siku moja kwenye wiki, hasa mwisho wa wiki na weka mipango ambayo utahitaji kwenda kukamilisha kwenye wiki inayofuata. Unaweza kufanya hivi siku ya jumapili jioni. Panga mambo makubwa mambayo unataka wiki inayokuja uweze kuyafanya kwenye biashara yako na hata maisha yako pia. Kisha weka na siku ambayo kila jambo ulilopanga litakuwa limekamilika.
Katika kupanga bajeti ya siku, hapa ndipo unapoyagawa vizuri masaa yako. Siku ina masaa 24, katika masaa haya unahitaji kufanya biashara, unahitaji kupumzika, unahitaji kuwa na watu wa karibu kwako (familia ndugu na marafiki.). Ni muhimu sana kupangilia muda huu kabla ya kuianza siku ili kuhakikisha hakuna unachoacha nyuma katika hivyo ambavyo ni muhimu kwako.
Anza kwa kupanga muda ambao utalala kila siku, wengi tunahitaji masaa 7 mpaka 8 ya kulala kwa siku. Hakikisha una tenga masaa haya ili upate muda w akutosha wa kupumzika. Baada ya kujua muda unaolala, jua ni muda kiasi gani utakaohitaji kwa siku kwenye mapumziko na hata kupata chakula. Hapa unaweza kutenga masaa mengine mawili kuanzia chai mpaka chakula cha jioni. Baada ya hapa unahitaji kutenga muda wa kuwa na familia yako au watu wako wa karibu, unaweza kutenga masaa mengine mawili kwa siku. Kwa muda wa kulala, wa kula na kuwa na watu wa karibu utakuwa umeshaondoa kama mawaa 12, na unabaki na masaa mengine 12. Sasa haya yagawe vizuri kwenye kazi za biashara yako, kwanza unahitaji muda wako binafsi wa kuweka mipango yako ya kibiashara, usipungue nusu saa kwa siku, saa moja ni vizuri zaidi. Pia unahitaji muda mwingine wa kujifunza kuhusu biashara, kwa kujisomea vitabu, nao usipungue nusu saa, saa moja ni bora zaidi.
Kwa mpangilio huu utabaki na masaa 10 kila siku ambayo unaweza kuyatumia kwa shughuli zako za kibiashara. Kama utatumia muda huu vizuri kila siku, utaweza kutekeleza majukumu yako mengi ya kibiashara. Wiki ijayo tutachambua unavyoweza kupanga vipaumbele vya biashara yako kwenye masaa haya kumi ya kibiashara kila siku.
Anza sasa kuweka bajeti ya muda wako, sio lazima ifanane na hiyo niliyotoa hapo juu, unaweza kuwa na mahitaji tofauti, muhimu ni uwe na bajeti na sio kutumia tu muda kama kitu ambacho hakina thamani.
TUPO PAMOJA.