Karibu kwenye falsafa yetu mpya ya maisha.

Kumbuka kama tulivyokubaliana, maisha bila ya falsafa ni maisha ambayo hayana thamani ya kuishi. Kama huna falsafa inayokuongoza kwenye maisha, utajikuta unafanya vitu ambavyo havina msaada kwenye maisha yako.

Na hapa tunatengeneza falsafa mpya kwa sababu falsafa tunazoishi sasa ndio zimekuwa chanzo kikubwa cha matatizo kwenye maisha yetu. Kwanza kabisa hatuzijui falsafa hizi vizuri hivyo tunaziishi kwa kuiga tu. Kwa kuangalia watu wanafanya nini na wewe ukafanya.

Kupitia falsafa hii mpya ya maisha utafanya kitu kwa sababu unataka kufanya na unajua kwa nini unafanya na sio kwa sababu kila mtu anafanya. Haya ndio maisha bora sana kwako kuishi na yatakuwa na furaha na mafanikio makubwa, bila ya kujali unaanzia wapi.

Kwenye maisha yetu ya kila siku, tumekuwa tunashuhudia watu wakiondoka kwenye eneo moja na kwenda eneo jingine wakiamini kwamba kule walikotoka ni kubaya na wanakokwenda ndio bora. Lakini haiwachukui muda kabla hawajafika kule na kukuta nako kuna matatizo, tena wakati mwingine makubwa kuliko kule ambako wametoka.

Kwa mfano mtu anaondoka kwenye kazi moja, na kuisema vibaya kwamba kazi ile ilikuwa sio nzuri, matatizo mengi, malipo kidogo. Anapokwenda kwenye kazi nyingine ana kuwa na imani kazi itakuwa bora, malipo mazuri na vingine vingi. Lakini anapofika kule anakuta kuna mambo magumu zaidi ya kule ambapo ametoka.

Mfano mwingine ni mtu anayeachana na mwenza wake, mwanandoa au hata mchumba. Mtu anaweza kuondoka akiwa na mambo mengi ambayo hakuyapenda kwenye mahusiano yale. Na akapata mtu mwingine wa kuanza naye mahusiano, na akawa na mategemeo makubwa. Lakini kadiri mahusiano haya yanavyokwenda, anagundua kuna changamoto nyingi zaidi wakati mwingine kuliko hata kule alipotoka.

Na pia tumekuwa tunaona kila siku wanasiasa wakihama vyama vyao na kuvisema vibaya sana. Wanapoingia chama kipya wanakuwa na matarajio makubwa lakini nako wanakutana na changamoto kubwa zaidi. Wanajikuta wakipiga tena kelele kwamba huku pia hakufai.

Huenda umeshakutana na hali kama hizi tunazojadili hapa leo, ulitoka eneo moja kwa sababu ya matatizo au changamoto na ukiamini unakokwenda hakutakuwa na changamoto, lakini umekutana nazo nyingi zaidi.

Leo hii tunaongeza kitu hiki muhimu sana kwenye falsafa yetu mpya ya maisha. Na hatuongezi kitu hiki ili tuache kupambana na changamoto zetu, au tukubali kuendelea kuumia, bali tujue mapema ya kwamba hata kule tunakokwenda mambo sio mteremko kama yanavyoonekana.

Kuna usemi unaosema kwamba nyasi za shamba jingine huwa zinaonekana ni za kijani kuliko zile zilizopo kwenye shamba ulipo. Lakini unapokwenda kwenye shamba lile, ukiangalia ulipotoka utaona nyasi ni za kijani zaidi. Hivyo kwenye maisha, ukiangalia kitu kwa nje unaweza kujipa matumaini makubwa sana. Unaweza kuona wanaofanya kazi fulani wako bora kuliko wewe, au wanaofanya biashara fulani au waliopo kwenye mahusiano fulani. Lakini unapoingia kwenye hali hizo unaanza kuona ni tofauti na ulivyokuwa unaona.

Hakuna kitu ambacho hakina changamoto. Ni jambo la kusikitisha, na zuri pia ya kwamba vitu vyote vizuri kwenye maisha tunavipata kwa ugumu. Kuna gharama fulani ambayo ni lazima uilipe ili uweze kupata kile unachotaka. Na kama tulivyoona kwenye makala iliyopita, dunia ina akili kuliko wewe, huwezi kuidhulumu na ukafanikiwa bila ya kulipa gharama.

Ni katika kulipa gharama hii ndio changamoto mbalimbali zinaibuka katika jambo lolote unalofanya.

Unaweza kupata kazi ambayo ina malipo mazuri kuliko uliyonayo sasa, lakini pia kazi hiyo ikawa inahitaji muda mwingi kuliko unaotumia sasa kwenye kazi. Na hivyo ukakusa muda wa kuweza kufanya mambo yako ya pembeni. Hivyo unakimbia kazi moja ambayo haikuwa na malipo mazuri, lakini ilikuwa inakupa muda wa kusimamia biashara zako, ukaenda kwenye kazi nyingine ambayo ina malipo mazuri lakini inakubana sana kiasi kwamba huna muda wa kusimamia biashara zako. Na hivyo inakubidi uache kuendesha biashara na kuweka nguvu zako kwenye kazi. Sasa hii ni changamoto kubwa kuliko ile ambayo umeikimbia.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Huwezi Kuidanganya Dunia, Acha Kujidanganya.

Kwa kujua kila kitu kina changamoto kunakusaidia nini?

Kwa kuongeza kiungo hiki muhimu kwenye falsafa yako ya maisha kunakusaidia nini kwenye maisha yako?

1. Utaacha kupelekwa kama upepo.

Tumeona watu wengi wakiacha biashara zao nzuri na kwenda kujiingiza kwenye biashara zinazowapoteza kwa sababu tu wameambiwa hii inalipa kuliko unayofanya. Tumeona watu wengi wakivunja mahusiano kwa sababu wameahidiwa ukija huku utapata kile unachokosa huko. Kama mtu hawezi kufikiri na kujiuliza ni changamoto gani nakwenda kukutana nayo upande wa pili, ni rahisi sana kuingia kwenye matatizo makubwa. Unapojua ya kwamba hata kule unapokwenda kuna changamoto zake na kuanza kuzifuatilia kwa makini, utaacha kufanya mambo kwa kufuata tu mkumbo.

2. Itakuandaa kwa ajili ya changamoto.

Watu wengi wanaotoka eneo moja kwenda jingine, huwa wanatoka wakifikiria mabaya ya kule wanakotoka na kutamani mazuri ya kule wanakokwenda. Hisia hizi huwafanya wasahau, au wasifikirie kwa kina changamoto za kule wanakokwenda. Na hivyo wanapokutana na changamoto inakuwa kitu cha kushangaza kwao na kuona mbona huku nako sio bora kama walivyofikiri. Wewe unapojua ya kwamba hata huku ninakokwenda kutakuwa na changamoto zake, utaanza kuzijua kwa undani changamoto hizo na utakuwa tayari kuzikabili. Pia kabla hujaingia utakuwa tayari umekubaliana na zile changamoto utakazokwenda kukutana nazo.

3. Itakujengea heshima kwa wengine.

Kuna watu wengi wamepoteza heshima zao kwa kushindwa kujua vitu vidogo sana kuhusiana na jambo hili. Mtu anayeachana na mke au mume wake na kuanza kumsema vibaya anakuwa anajivunjia heshima sana, kwa sababu kila mtu anajua hakuna mtu aliyekamilika. Mtu anayeondoka kwenye kazi moja huku akitoa maneno mabaya, anavunja heshima na hata mahusiano mazuri na watu alioachana nao kwenye kazi yake ya zamani. Wewe kwa kujua kwamba kila kitu kina changamoto, huondoki ukijidanganya kwamba huku ninakokwenda ndio bora kuliko ninakotoka. Na kwa kuwa unajua utakwenda kukutana na changamoto pia, utaona ni ujinga kuanza kusema vibaya kule unakotoka. Kwa sababu hakuna ambapo ni bora zaidi ya pengine, bali kuna changamoto zinazotofautiana.

4. Utajua ni nini hasa unachotaka.

Ni rahisi sana kuvutiwa na vitu kama fedha, lakini tunachotaka kwenye maisha sio fedha pekee, fedha ni eneo muhimu sana, ila ni eneo dogo kati ya yale ambayo tunataka kwenye maisha. Mtu anaweza kuvunja mahusiano ya uchumba au ndoa kwa sababu ya aliyenaye kukosa fedha na akawa amepata mwenye fedha. Lakini anapofika kwa huyu mwenye fedha anakuta kuna changamoto kubwa zaidi, labda mtu huyu hapati muda wa kumjali na kuwa naye karibu kama kule alikotoka mwanzo. Kwa hiyo mtu alifikiri anachohitaji ni fedha, ila anapofika kwenye fedha anakuta kumbe sio kitu hasa alichokuwa anataka. Mtu anaweza kutoka kwenye kazi moja kwenda kazi nyingine kwa sababu kazi hiyo nyingine ina malipo makubwa. Lakini anajikuta anafanya kazi ambayo haipendi, kazi ambayo inamnyima uhuru, inamnyima muda wa kutosha wa kukaa na familia yake na mengine mengi. Hapa mtu atagundua ya kwamba kumbe kitu muhimu zaidi kwake hakikuwa fedha, bali kuishi maisha ya kazi ambayo anaifurahia na inampa muda wa kufanya mambo mengine muhimu kwake.

Kwa kujua kwamba hata kule unakokwenda kutakuwa na changamoto zake, kunakufanya ukae chini na kutafakari, hiki ninachokwenda kufuata kule ni kizuri. Lakini je niko tayari kuishi na changamoto hizo nitakazokwenda kukutana nazo? Swali hili litakufunulia ni kipi hasa unachotaka kwenye maisha yako.

5. Utadumu pale ulipo au kule unakokwenda.

Kwa kujua changamoto kabla hujaingia au kutoka mahali, kutakufanya uwe na maamuzi ambayo yatakuwezesha kudumu pale ulipo au kule ulikoamua kwenda. Kufikiri kwa kina kutakuwezesha wewe kuchukua maamuzi ya kina na utakayokuwa tayari kuyasimamia hata kama wengine hawawezi kufanya hivyo.

Leo umeongeza kiungo hiki muhimu sana kwenye falsafa yako mpya ya maisha, huenda ulikuwa unakijua lakini hukutilia maanani. Basi leo weka hii kuwa sehemu yako ya maamuzi. Usikubali mabadiliko yoyote kabla hujachunguza kwa makini ni changamoto gani unakwenda kukutana nazo na hivyo kujiandaa kwa changamoto hizi. Maisha bora ni haki yako ya msingi kabisa, na hayaanzii mbali bali ndani yako mwenyewe.

Nitoe angalizo kwamba usitumie dhana hii kuendelea kuwa na maisha magumu, kwa kuona uendelee kubali kwenye kazi/biashara ambayo haikupeleki popote kwa sababu tu ukienda kwenye kazi/biashara nyingine itakubana zaidi. Tumia dhana hii ya falsafa kuboresha zaidi kama utabaki, au kwenda ukiwa umejiandaa kama utaamua kuingia kwenye kazi/biashara nyingine.

Kila la kheri,

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz