Zaidi ya nusu ya vitu utakavyopanga kufanya leo kuna uwezekano mkubwa hutaweza kuvifanya, hutapata nafasi ya kuvifanya.
Zaidi ya nusu ya vitu utakavyotaka kusoma leo, hutaweza kuvisoma.
Zaidi ya nusu ya vitu utakavyosema NDIO leo hutaweza kuvitimiza.
Vipindi vya tv utakavyopanga kuangalia leo hutapata muda huo.

Kwa kifupi ni kwamba tuna muda ule ule kwa siku, lakini vitu vya kufanya vinaongezeka mara dufu.
Kuna simu na jumbe za kujibu, kuna kutembelea mitandao ya kijamii, kuna email za kujibu, kuna umbea wa kusikiliza na mengine mengi ndani ya masaa hayo hayo uliyonayo.
SOMA; Usikubali jua lizame leo kabla hujafanya kitu hiki muhimu.
Huwezi kufanya vitu vyote hivi, lakini lazima siku yako hii iishe. Je unaimalizaje?
Ili kuwa na maisha yenye mafanikio, hakikisha kila siku inayopita inahesabika.
Siku iwe inahesabika kwa maana kwamba baada ya muda kupita ukumbuke kwamba siku hii ya leo ilikuwa muhimu sana kwako kwani ulifanya jambo ambalo ni muhimu sana.
Hivyo kwa siku ya leo na kila siku, katika mambo mengi unayopanga kufanya, chagua yale ambayo ni muhimu zaidi. Chagua yale ambayo ukiyakamilisha siku yako itakuwa bora sana. Na fanya mambo hayo tu.
Ila kama utaendelea kuichukulia siku kama ulivyozoea, na kuamua kufanya kila kinachojitokeza mbele yako, utashangaa miaka inakatika huku ukiwa huna kitu kikubwa unachoweza kuonesha kwa miaka hiyo.
Ihesabu leo kuwa siku kwa kufanya kitu ambacho kina manufaa makubwa kwako kwa siku za mbeleni. Hii inahitaji ujasiri na nidhamu ya hali ya juu kwa sababu kuna vingi vya kuvutia vinavyotaka kuiba muda wetu.
TAMKO LA LEO;
Najua ya kwamba vitu ninavyopanga na kutamani kufanya ni vingi kuliko muda nilio nao wa kutekeleza. Na pia najua kama nitaamua kufanya chochote kinachojitokeza nitapoteza siku za maisha yangu. Naamua leo kwamba nitatumia leo na siku zangu zijazo kufanya yale ambayo ni ya muhimu sana kwangu, ili hata nitakapokuja kuangalia nyuma nione kwamba siku ya leo ilikuwa muhimu kwa mafanikio yangu. Nitahesabu leo kuwa siku kwangu kwa sababu nitafanya yale ambayo ni muhimu.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.