Wote tunakubaliana kwamba hatuwezi kufanya kila kitu ambacho tunatamani kufanya.
Na pia hatuwezi kukubali kila kitu kinachokuja mbele yetu.
Hii ni kwa sababu tuna mambo mengi na muhimu ya kufanya na wakati huo huo muda sio rafiki kwetu.
Hivyo basi tunahitaji kuwa makini sana ni wakati gani wa kusema NDIYO na wakati gani wa kusema HAPANA.

Uhuru wako na mafanikio yako makubwa yapo kwenye kuweza kutumia neno HAPANA. Kadiri utakavyoweza kusema hapana mara nyingi, ndivyo utakavyopata muda wa kufanya yale ambayo ni muhimu kwako.
Lakini je, ni kigezo gani unachoweza kutumia kusema NDIO au HAPANA? Maana kuna wakati unajikuta umeshasema ndio ila baadae unajuta kwa nini ulisema ndiyo.
SOMA; Sema HAPANA, Hapa Ndio Uhuru Wako Ulipo.
Leo nakupa siri moja muhimu ya kujua kabla hujasema ndio, itakusaidia sana.
Kabla hujasema ndio hakikisha ni kitu ambacho kina thamani kweli kwenye maisha yako. Jiulize kama ungekuwa tayari kulipia tsh laki moja kwenye kusema ndio kwenye ombi hilo ulilopewa na mwingine. Yaani kukubali kwako ungetakiwa ulipe laki moja.
Au jiulize kama ungehitajika kulipa elfu 20 kwa saa unayotumia kusoma kitu ambacho umekubali kusoma. Kwa mfano ungekuwa tayari kulipa elfu 20 usome gazeti? Vipi kuhusu mitandao ya kijamii na habari za udaku?
Kama jibu ni hapana, yaani usingekuwa tayari kulipia fedha katika kukubali ombi au kusoma kitu basi kitu hiko sio muhimu na sema HAPANA haraka sana.
Hakikisha unaweka thamani kubwa kwenye jambo lolote unalokubali kufanya. Hii itakuweka kwenye njia ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
TAMKO LA LEO;
Kabla sijasema NDIYO nitahakikisha ni kitu ambacho kina thamani kubwa kwangu. Nitahakikisha ni kitu ambacho nipo tayari kutoa fedha zangu na kukilipia, kama ingebidi kufanya hivyo. Kama kitu kimekosa thamani hii basi sio muhimu kwangu na jibu la haraka sana ni HAPANA. Najua kufikia mafanikio kunahitaji matumizi mazuri sana ya muda maana ndio rasilimali yenye thamani kubwa sana kwangu.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.