Karibu tena kwenye makala ya wiki hii ya FALSAFA MPYA YA MAISHA. Naamini umekuwa unajifunza na kujijengea maisha mapya kupitia falsafa hii ambayo tunaitengeneza.

Kama ambavyo tumeshajifunza, iwe unajua au hujui, unaishi falsafa fulani. Sasa kama unaishi falsafa ambayo huijui ni vigumu sana kuwa na maisha ya furaha na mafanikio. Ndio maana ni muhimu sasa kujitengenezea falsafa mpya ya maisha ambapo tunafanya vitu kwa sababu tumechagua kufanya na sio kwa sababu tunalazimika kufanya.

Leo katika falsafa mpya ya maisha, tunakwenda kuongeza kitu kingine muhimu sana. Kitu hiki ni nguvu kubwa sana ambayo kila mmoja wetu anaimiliki. Hii ni nguvu ambayo kila mtu anayo lakini kuitumia tunatofautiana. Kuna ambao wanaweza kuitumia, wengine hawawezi kuitumia.

Nguvu hii ni kubwa sana kwa kiasi kwamba unaweza kuitumia kuyabadili kabisa maisha yako na hata kuibadili dunia. Ndio nguvu hii unayo hapo ulipo, na unaweza kuanza kuitumia wakati wowote unapoamua.

Nguvu hii kubwa inaweza kukutoa kwenye maisha magumu na kukufikisha kwenye maisha ya furaha na mafanikio makubwa.

Nguvu hii kubwa unayoimiliki inaweza kukupatia chochote unachotaka kutoka kwa mtu yeyote anayekimiliki.

Nguvu hii kubwa unayoimiliki inaweza kufanya maisha yako kukumbukwa hapa duniani hata baada ya kuwa umeondoka kwa muda mrefu.

Hii ni nguvu kubwa sana ambayo unaimiliki, lakini huenda hujaanza kuitumia au umekuwa huitumii kwa kiasi cha kutosha.

Nguvu hii haijalishi jinsia yako, kabila lako au umri wako, unayo na unaweza kuitumia kwa hali yoyote ile.

Nguvu hii haijalishi umezaliwa kwenye familia ya kitajiri au ya kimasikini, haijalishi kama ulipata elimu au hukupata, haijalishi kama darasani ulikuwa unafaulu au unafeli. Hii ni nguvu ambayo unayo na haiingiliwi na hali nyingine yeyote.

Na nguvu hii hakuna anayeweza kukuzuia wewe kuitumia, hakuna wa kukupa au kukunyima, ni nguvu ambayo ipo ndani yako na matumizi yake ni juu yako.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Kitu Kimoja Ambacho Kila Mmoja Wetu Anapigania Kukipata Na Jinsi Ya Kukipata Kwa Uhakika.

Je nguvu hii ni ipi?

Nafikiri kama umekuwa unajiuliza kwa makini kutokana na maelezo yote hapo juu nguvu hii itakuwa nini utakuwa umeshaanza kupata majibu. Lakini kama hujapata dalili zozote za majibu basi utaijua nguvu hiyo hapa na jinsi ya kuweza kuitumia kwa ubora zaidi.

Nguvu ambayo inaweza kufanya makubwa na ambayo kila mmoja wetu anaimiliki ni UPENDO.

UPENDO ni nini?

Kuna maelezo mengi sana kuhusu upendo, kuna falsafa nyingi sana kuhusu upendo. Kuna aina nyingi sana za upendo ambazo zimechambuliwa na kuelezwa vizuri. Kwa lengo letu la kutengeneza falsafa mpya ya maisha yetu tutumie njia rahisi ya kueleza upendo.

Upendo ni hisia za kujijali wewe mwenyewe na kuwajali wengine pia kwa njia ya wema. Upendo sio kitu ambacho tunaweza kukiona au kukishika, ni nguvu ya hisia ambayo ipo ndani ya kila mmoja wetu.

Kwa nini kujijali wewe mwenyewe kwa wema?

Unapojijali wewe mwenyewe kwa wema, unahakikisha kwamba maamuzi yoyote unayofanya, maisha unayochagua kuishi yanahakikisha kwamba unaendelea kuwa vizuri na kuyafurahia pia. Hii ina maana kwamba utaepuka kufanya yale mambo ambayo yanapelekea maisha yako kuwa hovyo au kuharibika.

Kwa nini kuwajali wengine kwa wema?

Sio kila maamuzi mazuri kwako yatakuwa mazuri kwa kila mtu. Ndio maana kwa upendo utaangalia je hili linawanufaisha wengine au la. Kwa kuwajali wengine kwa wema, utahakikisha kwamba jambo lolote unalofanya lina mchango mzuri kwa wale wanaokuzunguka pia. Hii itakuondolea ubinafsi na kuweza kuwasaidia wengine nao kuwa na maisha bora.

Kwa nini upendo ni nguvu kubwa?

Upendo unapotumika kwa usahihi, unapofanya kitu ambacho ni muhimu kwako na kwa wengine pia, unatengeneza dunia nzuri sana itakayokusaidia kuwa na maisha bora.

Kumbuka ya kwamba hatuishi ndani ya chungu, au ombwe. Tumezungukwa na watu wengi. Na watu hawa wana tabia tofauti na tabia zetu, wana mipango tofauti na mipango yetu. Lakini inapokuja kwenye upendo, hii ni nguvu ambayo inaweza kuwaweka watu wote pamoja bila ya kujali tofauti zetu.

Ndio maana upendo ni nguvu kubwa sana, kwa sababu inaweza kutuunganisha, hata kama hatuwezi kuelewana kwa lugha, lakini kwa upendo wote tunaelewana.

UPENDO sio falsafa mpya.

Kama ambavyo tumekuwa tunajifunza kwenye falsafa hii mpya, sio kwamba tunajifunza mambo mapya kabisa, ila tunajifunza mambo ambayo tunayajua ila hatuyatumii. Au tunayatumia ila hatujui ni kwa nini hasa tunayatumia, kwa sababu waliotuuzia falsafa hii mwanzo hawakupata muda wa kutuambia kwa kina ni kwa nini ni muhimu kuishi na falsafa fulani.

Dini zote duniani, zimejengwa kwenye msingi wa falsafa hii, UPENDO. Kwa wakristo, katika AMRI KUMI ZA MUNGU, wanasema amri iliyo kuu ni upendo. Mpende Mungu wako, wapende wazazi wako, wapende majirani zako, usizini, usiibe…. zote hizi zinaingia moja kwa moja kwenye upendo.

Kwa dini zote na hata jamii zote ambazo zimeweza kuishi vizuri, upendo ni kiungo muhimu sana.

Ndio maana kama utaweza kuishi vizuri kwa falsafa hii ya UPENDO pekee, unaweza kupata chochote ambacho unakitaka kwenye maisha yako.

Kinyume cha UPENDO.

Kinyume cha upendo ni nini?

Utasema CHUKI, na umekosea, kinyume cha upendo sio CHUKI bali ni HOFU.

Hofu inaondoa upendo na hofu ndio imekuwa chanzo kikubwa cha watu kufanya mambo ambayo sio mema kwao au kwa watu wanaowazunguka.

Kwa nini wengi hatuwezi kuishi falsafa hii ya upendo?

Kwa sababu wengi tumetawaliwa na hofu, wengi tunaongozwa na hofu.

Unahofu kwamba kesho hutapata fedha, hivyo unapopata nafasi ya kushika fedha za wengine unaziiba. Una hofu kwamba kila unayekutana naye anataka kukudhuru na hivyo kuanza kumdhuru kila unayekutana naye.

Hofu ni nguvu kubwa sana ambayo imetutenganisha na upendo, imetufanya tuishi maisha yasiyo ya maana kwetu na kushindwa kufikia mafanikio makubwa.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Hakuna Kisichokuwa Na Changamoto.

Tunawezaje kuutumia upendo na kuwa na maisha bora?

Kuna njia nyingi sana ambazo tumekuwa tunatumia upendo kujaribu kuwa na maisha bora, lakini njia hizi mara nyingi zimekuwa zinaleta maisha ambayo sio tuliyotegemea.

Baadhi ya njia hizo ni kufikiri upendo unatokana na vitu vinavyoonekana, kwa mfano kufikiri ukiwapa watu fedha ndio watakupenda. Hii sio kweli na imekuwa inaharibu mahusiano mazuri baina ya watu.

Zifuatazo ni njia nzuri za kuweza kutumia upendo katika kuboresha maisha yetu.

1. Upendo unaanza na wewe mwenyewe.

Watu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba hakuna anayewapenda. Wakati hilo linaweza kuwa kweli, swali muhimu wanalotakiwa kujibu ni je wao wanawapenda watu gani?

Ukweli ni kwamba upendo unaanza na wewe mwenyewe, upendo unaanza na wewe kuonesha kuwajali wengine. Kama hakuna anayekupenda maana yake hata wewe hakuna unayempenda. Upendo una nguvu kubwa sana kiasi kwamba ukianza kutoa tu, unapokea mwingi sana.

2. Msingi wa mafanikio ni upendo.

Biashara yako inakupa shida? Weka upendo. Kazi yako imekuwa mzigo kwako? Weka upendo. Maisha ya familia yako yamekuwa kama ya vita? Weka upendo.

Unaweka upendo kwenye biashara pale unapojali sana kuhusu mteja wa biashara yako. Mpende na kuona ni mtu anayekutegemea wewe ili maisha yake yawe bora. Usifanye kitu chochote ambacho kitakunufaisha wewe na kumuumiza yeye. Kitu hiki kitaharibu mahusiano yenu na kama utaweza kufanya kwa mteja mmoja, unaweza kufanya kwa kila mteja na muda sio mrefu biashara yako inakuwa kwenye matatizo makubwa. Anza na upendo kwa wateja wako.

Kama kazi unaona imekuwa mzigo kwako, kabla hujaanza kusema hupendwi au watu wanakufanyia mabaya, hebu anza kuweka upendo zaidi. Anza kwa kupenda ile kazi ambayo unaifanya. Iangalie kwa jicho la tofauti, usiiangalie kama sehemu ya wewe kulipwa, bali angalia kama sehemu ya wewe kuwasaidia wengine. Kama ni mwalimu hebu ona kama unawasaidia watu kujifunza na kuwa na maisha bora, kama ni daktari hebu ona unawasaidia watu kuwa na afya bora na hivyo kuendelea na maisha yako. Kama ni mfanya usafi hebu ona kwamba unawasaidia watu kukaa sehemu safi na hivyo kuweza kufanya yale ambayo ni muhimu. Chochote unachofanya, weka fedha au chochote unachopata pembeni kwa muda na fikiria ni mchango gani unaoutoa kwa binadamu wenzako wanaofaidika na kile unachofanya. Pia wapende wale unaofanya nao kazi, kuna mtu anagombana na wewe kila siku, mpende, akikusema vibaya mseme vizuri, akifanya chochote kibaya usilipe.

Kwenye familia pia weka upendo. Upendo ni zaidi ya kila kitu ambacho unafikiri watu wanataka. Watu hawataki tu kutimiziwa mahitaji yao ya chakula, malazi na mavazi. Watu wanataka kuona wanajaliwa na upo kwa ajili yako. Anza kuweka upendo zaidi na utabadili sana familia yako.

3. Hakuna anayekuchukia, ila wana hofu zao.

Kitu kikubwa sana ambacho kitakupa uhuru kwenye maisha ni pale utakapojua kwamba hakuna mtu anayekuchukia wewe. Watu wana hofu zao binafsi na njia ya kuonesha hofu hizo ni kuonesha kwamba wana chuki na wewe, kumbe ukweli ni kwamba wana chuki na wao binafsi, yaani wanajichukia wao wenyewe.

Kwamba wafanyabiashara wenzako wanakuchukia kwa sababu biashara zako zinakwenda vizuri kuliko za kwao? Hapana, wana hofu kwamba biashara yako inavyokwenda vizuri na kukua basi za kwao zitakufa. Na hivyo wanajichukia kwa sababu hawajaweza kufanya biashara vizuri kama wewe(au wewe ndio unajichukia kwa sababu hujaweza kufanya biashara vizuri kama wengine). Na hivyo badala ya wewe kuwalipa hili kwa chuki au hofu, wapende, waoneshe kwamba inawezekana na kwao pia.

Kwamba wafanyakazi wenzako wanakuchukia kwa sababu wewe upo makini zaidi na kazi, hupotezi muda na unakamilisha majukumu yako na kuomba mengine. Ukweli ni kwamba wana hofu kwamba kwa ufanyaji kazi wako wewe, wao wataonekana ni wazembe na hivyo wananichukia kwa kushindwa kuwa kama wewe. Ila wanaonesha chuki ile kwako wewe. Sasa kama na wewe utawachukia hautasaidia hali hiyo. Wapende na waoneshe kwamba hata wao wanaweza kufanya kazi zao kwa umakini mkubwa kama wewe.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Huwezi Kuidanganya Dunia, Acha Kujidanganya.

4. Jisahau kwenye kitu unachochagua kufanya, na toa huduma iliyo bora.

Njia nyingine nzuri ya kutumia nguvu ya upendo ni kujisahau wewe mwenyewe kwenye kile kitu ambacho unakifanya. Sahau wewe unanufaika nini, sahau nani anakuambia nini, wewe kazana kuweka kila uwezo uliopo ndani yako kuhakikisha unatoa kilicho bora sana. Penda kile unachofanya na wapende wale wanaokipokea. Kwa njia hii utafanya mambo makubwa sana kwenye maisha yako.

Upendo ni nguvu kubwa sana ambayo ipo ndani ya kila mmoja wetu. Kama utaweza kutumia nguvu hii utaweza kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa. Kama utashindwa kutumia nguvu hii utakuwa na maisha ya hofu na yasiyo ya uhakika.

Ifanye kuwa falsafa yako kwamba jambo lolote unalofanya unalifanya kwa upendo. Jisahau wewe mwenyewe na fanya kitu ambacho kitawanufaisha wengine, jijali sana na jali wengine kwa wema. Kwa njia hii kila utakachosema au utakachofanya, kitaongeza thamani kwa wengine na kitakupa wewe fursa ya kuwa zaidi na zaidi.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz