Kama sio ngumu ni laini…

Kama sio moto ni baridi…

Kama sio haraka ni polepole…

Kama sio nyeupe ni nyeusi….

JITOE KWELI ILI UWEZE KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA.
JITOE KWELI ILI UWEZE KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA.

Hivi ndivyo mafanikio yanavyokwenda, ni unafanya kinachokupeleka kwenye mafanikio au hufanyi na hakuna hali ya kati kati, kwamba najiandaa kwamba nitaanza.

Chochote unachofanya, kipe kila kitu ulicho nacho au achana nacho na ukafanye mambo mengine ambayo ni muhimu zaidi.

SOMA; Sababu 15 Zinazokuzuia Kujiajiri Na Jinsi Ya Kuzishinda.

Kwa njia yoyote ambayo umechagua ikufikishe kwenye mafanikio, hakikisha unakuwa mgumu, hakikisha unakuwa moto, hakikisha unakuwa haraka na hakikisha unakuwa mweupe.

Unakuwa mgumu kwa kuhakikisha kwamba unachokifanya unakipa kila kitu kilichopo ndani yako, na kwenda hatua ya ziada, bila ya kuchoka au kukata tamaa.

Unakuwa moto kwa kuhakikisha hakuna kinachokuzuia kufika pale unapotaka kufika. Chochote kitakachojitokeza na kuwa kikwazo kwenye njia yako unakichoma.

Unakuwa haraka kwa kuhakikisha unazitumia vizuri fursa zinazojitokeza kwenye kile ulichochagua kufanya. Kwa sababu fursa hazikusubiri, ukichelewa umekosa.

Na unakuwa mweupe kwa kuhakikisha unakuwa mwaminifu na mwadilifu. Kwa kutekeleza kile unachoahidi na kufanya ambayo ni mema kwako na kwa wanaokuzunguka.

Kuwa mgumu, moto, haraka na mweupe kwenye chochote unachofanya na uone kama maisha yako yatabaki yalivyo. Na kumbuka chochote kati kati ya hapo ni hovyo, kwamba ni mgumu na mlaini, au vuguvugu, au haraka kiasi, au nyeupe iliyochanganyika na nyeusi kidogo? Unapoteza muda wako.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba maisha yanahitaji kuchagua kuwa upande mmoja na sio kuwa kati kati. Na upande mmoja unaleta mafanikio makubwa wakati upande mwingine unaleta kushindwa. Katikati ni kupoteza tu muda. Kuanzia leo nimechagua kuwa kwenye upande ambao ni wa mafanikio. Nitafanya mambo yale ya mafanikio bila ya kulegeza uzi. Nitakuwa mgumu kwa kuhakikisha naweka ubora wangu wote, nitakuwa moto kwa kuhakikisha hakuna cha kunizuia, nitakuwa haraka kwa kuzitumia fursa zinapojitokeza na nitakuwa mweupe kwa kuwa mwaminifu na mwadilifu kwa kila jambo ninalofanya.

NENO LA LEO.

Let others lead small lives, but not you. Let others argue over small things, but not you. Let others cry over small hurts, but not you. Let others leave their future in someone else’s hands, but not you. Jim Rohn

Acha wengine waishi maisha madogo, lakini sio wewe. Acha wengine wabishane kuhusu mambo madogo, lakini sio wewe. Acha wengine walie pale wanapoumizwa kidogo, lakini sio wewe. Acha wengine waache kesho yao kwenye mikono ya mtu mwingine, lakini sio wewe.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.