Binadamu sisi ni wajanja sana.
Tunaweza kufanya kila kitu ili kutoroka tatizo na sio kulitatua.

Kwa nini tunafanya hivi?
Kwa sababu kutatua tatizo kunatutaka tufanye vitu ambavyo hatujisikii vizuri kufanya, au kunatuhitaji tubadilike.
Lakini sisi hatupendi kubadilika, hatupendi kufanya vitu ambavyo hatujisikii vizuri kufanya, hivyo hatua rahisi ya kuchukua ni kutoroka.
Ni njia zipi tunazotumia kutoroka matatizo?
Njia ya kwanza ni kulalamika na kulaumu. Hii tumeshaijadili sana, na tulishakubaliana ufanye zoezi moja muhimu sana ili kuondokana na njia hii ya kutoroka. Kama hukufanya zoezi lile tafadhali lifanye hapa; Naomba Ufanye Changamoto Hii Ya Siku Kumi, Utabadili Sana Maisha Yako.
Njia ya pili ya kutoroka ambayo wengi tunaitumia bila hata ya kujua ni kuzungumzia tatizo kwa mtu ambaye hawezi kusaidia chochote.
Kwa mfano una matatizo kazini, badala ya kuzungumza na wale ambao una matatizo nao, hufanyi hivyo, ila ukifika nyumbani ndio unazungumza matatizo ya kazini.
Au una matatizo nyumbani, badala ya kukaa chini na yule ambaye una matatizo naye, hufanyi hivyo badala yake unakwenda kusema kwingine.
Ni rahisi kumwambia mke/mume wako kwamba bosi wako au mfanyakazi wako anakupa changamoto, lakini sio rahisi kukaa uso kwa uso na mtu huyo na kumwambia wewe unanipa changamoto na mkakaa chini kutatua.
Ni rahisi kumwambia rafiki yako kwamba mke/mume wako anafanya mambo ambayo wewe hupendi, lakini ni vigumu kukaa naye uso kwa uso na kumwambia kitu fulani na fulani unachofanya sikipendi.
Tumekuwa tunakimbia matatizo kwa kuyasema kwa watu ambao hawahusiki na hata kama wangehusika hawawezi kutatua.
SOMA; Mambo Muhimu Ya Kuzingati Ili Kuwa Na Matumizi Mazuri Ya Muda Wako.
Njia ya tatu ya kutoroka tatizo ni kujisahaulisha kama tatizo lipo. Kutumia vilevi na kwa muda mfupi kuona maisha yako hayana shida yoyote. Lakini hii inadumu kwa muda mfupi tu, mambo yanarudi pale pale.
Njia ya nne ya kutoroka tatizo ni kuumwa. Kuna baadhi ya tafiti zinaonesha kwamba wengi wanatumia ugonjwa kama sehemu ya kukimbia matatizo wanayokutana nayo kwenye maisha. Sio kwamba wanajifanya wanaumwa, hapana, ila miili yao inatengeneza ugonjwa ili wajipe sababu ya kutoroka matatizo yao. Magonjwa mengi ya kisaikolojia na magonjwa mengi ya akili yanasababishwa na watu kukwepa majukumu yao au kutoroka matatizo yao.
Ni njia ipi umekuwa unatumia sana kutoroka matatizo yako?
Kama una tatizo lolote kwenye maisha yako, hata liwe kubwa kiasi gani, lipatie ufumbuzi. Kuzidi kuliacha hakulifanyi liondoke ila linazidi kukua na kushika mizizi. Chukua hatua leo kwa tatizo lolote ambalo linakusumbua.
TAMKO LANGU;
Najua nimekuwa natoroka matatizo yangu mwenyewe kwa kukimbilia kufanya vitu ambavyo ni rahisi lakini havisaidii tatizo. Najua kinachonifanya nitoroke matatizo yangu ni kwa sababu kuyatatua kunanihitaji nifanye vitu ambavyo sipo tayari kuvifanya na pia kunanihitaji nibadilike. Nimekuwa napoteza muda wangu kusema matatizo kwa watu ambao hawawezi kusaidia chochote. Kuanzia sasa nitatatua tatizo lolote linalotokea kwenye maisha yangu, sitatoroka tena.
NENO LA LEO.
You will find peace not by trying to escape your problems, but by confronting them courageously. You will find peace not in denial, but in victory. – Donald Walters
Utapata amani sio kwa kujaribu kuyakimbia matatizo, bali kuyakabili kwa ujasiri. Utapata amani sio kwa kukataa matatizo hayapo, bali kwa kuyashinda.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.