MUHIMU;
Tarehe 05/10/2015 itaanza semina muhimu na ya mwisho kwa mwaka huu kwa njia ya mtandao. Semina hii inakwenda kwa jina MIMI NI MSHINDI, na utajifunza mambo yote muhimu unayotakiwa kujua na kufanyia kazi ili uwe mshindi wa kweli kwenye maisha yako. Semina hii itaendeshwa kwa njia ya email, kundi la wasap na kutumiwa ujumbe wa simu. Usipange kabisa kukosa semina hii. Pia jiunge mapema kabla nafasi hazijajaa. Fungua hapa kupata taarifa na kujiunga;
SEMINA; MIMI NI MSHINDI (Ahadi Yangu Na Nafsi Yangu)

Tunafundishwa mambo mengi sana shuleni na hata kwenye maisha yetu ya kijamii. Lakini kuna mambo mengine muhimu sana ambayo huwa hatupati nafasi ya kufundishwa, iwe ni shuleni au kwenye jamii.
Moja ya mambo hayo ni kuhusu FEDHA. Katika mfumo wote wa elimu na hata kwenye maisha ya kwenye jamii hakuna sehemu ambapo tunapata nafasi ya kufundishwa kwa umakini kuhusu fedha.
Na hivyo elimu ya fedha tuliyonayo wengi tunaipata kwa kuona wengine wanafanya nini na sisi wenyewe tunaendeshwaje na tamaa zetu au maamuzi yetu.

PATA KITABU HIKI AMBACHO KITAKUTOA KWENYE CHANGAMOTO ZA KIFEDHA UNAZOPITIA. BONYEZA HAYA MAANDISHI KUKIPATA.

 
Kwa kuendesha maisha ya kifedha kwa njia hii ya kuangalia wengine au kukubali kuendeshwa na hisia zetu, kumesababisha watu wengi kujikuta katika wakati mgumu sana kifedha. Hali hii imezalisha masikini wengi sana.
Jambo lolote kwenye maisha, ili uweze kulifanya vizuri ni lazima ujifunze, upate maarifa sahihi ambayo yatakuwezesha kuchukua maamuzi sahihi yatakayokuletea matokeo bora.
Leo nitakushirikisha sheria tatu kuhusu fedha ambazo hujawahi kufundishwa popote. Kuna baadhi umekuwa unazitumia kutokana na mazoea lakini hujawahi kupata maarifa ya kutosha kuhusiana na sheria hizi za fedha.
Kwa kujifunza sheria hizi hapa na kuzifanyia kazi, maisha yako ya kifedha yataanza kubadilika na utaanza kuona mambo mazuri yakitokea kwenye maisha yako.
Zifuatazo ni sheria tatu muhimu kuhusu fedha, jifunze na zifanyie kazi;
1. Sheria ya kwanza; TENGENEZA FEDHA.
Sheria ya kwanza kabisa ya fedha ni kwamba lazima utengeneze fedha. Nakuhakikishia ulikuwa hujui sheria hii, japo utagoma kwamba ulikuwa unaijua. Unajua kwa nini nakwambia ulikuwa huijui? Kwa sababu ungekuwa unaijua usingeshiriki michezo ya bahati nasibu, au kucheza kamari(beting), au kuomba rushwa au kuibia wengine, au kufikiri utakutana na zali la mentali na mengine mengi kama hayo.
Sheria ya kutengeneza fedha inasema kwamba UTALIPWA KULINGANA NA THAMANI UNAYOZALISHA. Umeona ilivyo rahisi?
Hii ina maana kwamba ili ulipwe fedha ni lazima utoe thamani, ni lazima ufanye kitu ambacho kinawafaidisha wengine na wao wawe tayari kulipia kile ulichofanya. Iwe ni kazi au biashara, ni lazima ufanye kitu ambacho kinawasaidia wengine.
Sheria hii ni rahisi sana kwa sababu kama unataka kupata fedha, angalia wengine wanataka nini wapatie na kama unataka kupata fedha zaidi ya unavyopata sasa, ongeza thamani ya kile unachofanya sasa. Kama unahudumia watu watano, hudumia watu kumi, tayari utakuwa umeongeza wigo wako wa kupata fedha zaidi.
Kama umeelewa sheria hii ya kwanza inabidi usahau bahati nasibu, sahau kamari(beting), sahau njia nyingine zote ambazo zinakuahidi utapata fedha bila ya kutoa thamani, maana ni za uongo na utaishia kupoteza fedha au kutapeliwa.
SOMA; Sababu Tatu(3) Zinazokuzui Kufanikiwa Kwenye Kazi Unayofanya.
2. Sheria ya pili; HIFADHI/TUNZA FEDHA.
Hii ndio ulikuwa huijui kabisa, ila usiwe na shaka, utaielewa vizuri sana hapa.
Ukishapata fedha huwa unafanya nini? Umefanya biashara na ukapata faida, huwa unafanya nini? Au mwisho wa mwezi umepokea mshahara, huwa unafanya nini? Au wewe ni dalali na umekamilisha dili, na kupewa sehemu yako ya fedha huwa unafanya nini?
Watu wote huwa wanakimbilia kutumia fedha ile waliyopata. Unapata fedha na kukimbilia kuitumia, kununua vitu ambavyo unafikiri ni muhimu wakati sio muhimu. Unajikuta unaona sehemu nyingi sana za kutumia fedha. Na kadiri unavyokuwa na fedha ndivyo matumizi nayo yanaonekana.
Kama kuna sehemu inayozalisha masikini wengi, ni kushindwa kutumia sheria hii ya pili ya fedha.
Kila unapopata fedha unasukumwa kuitumia, unaona vitu vizuri, matatizo ndio yanajitokeza na vitu vingine vingi.
Katika sheria ya pili ya fedha, unahitaji kuweza kuitunza fedha, kuihifadhi kwa muda kabla hujafanya maamuzi yoyote. Hii ni hatua muhimu sana kama unataka kuweza kufikia uhuru wa kifedha.
Hivyo unapopata kipato chako, kabla hujakimbilia kufanya matumizi au hata uwekezaji, itunze kwanza, kaa nayo kwanza, iweke kama akiba benki, japo kwa kipindi fulani. Halafu katika kipindi hiki ambacho unaitunza, endelea na maisha yako kama vile huna fedha ile. Yaani endelea na maisha yako bila ya kufikiria kwamba una fedha benki ambazo unaweza kutumia kwenye kitu chochote unachotaka. Kwa mfano kuna kitu unatamani sana kununua, na ungeweza kununua kwa fedha uliyonayo, ila hufanyi hivyo kwa sababu fedha hiyo ipo kwenye hatua ya kutunzwa. Hata kama inakubidi kushinda njaa, fanya hivyo, lakini fedha ile uwe umeitunza.
Unaweza usielewe vyema hapa, lakini kwa kifupi ninachotaka ujenge hapa ni ile nidhamu ya wewe kuweza kuiendesha fedha na sio kuacha fedha ikuendeshe wewe. Kwa sababu watu wengi wanapokuwa na fedha ni kama akili zao zinaacha kufanya kazi mpaka fedha ile iishe.
Nafikiri umewahi kukutana na kauli hizi, mimi nikipata fedha siwezi kutulia mkapa fedha hiyo iishe, au ukiwa huna fedha unakuwa na mawazo mazuri sana, lakini ukishazipata mawazo yote yanapotea.
Yote haya yanatokana na kushindwa kuitunza fedha, kushindwa kuiendesha fedha na kukubali fedha ikuendeshe wewe.
Kuanzia sasa, tumia sheria hii ya fedha, unapopokea kipato chako, ukishatoa yale matumizi ya msingi, nyingine itunze, na sahau kama una fedha umetunza. Hutunzi kwa muda mrefu kwa sababu tunakwenda kwenye sheria ya tatu muhimu.
SOMA; Ushauri; Jinsi Ya Kutunza Fedha Ya Akiba Kama Una Matumizi Mabaya ya Fedha.
3. Sheria ya tatu; IFANYE FEDHA IKUZALISHIE.
Sheria hii nayo huwa tunafikiri tunaielewa na kuitumia lakini siyo kweli. Baada ya kupata fedha, kuweza kuitunza sasa unahitaji kuweza kuifanya fedha yako kukuzalishia. Hapa unaiweka fedha yako sehemu ambapo inazalisha faida zaidi ya kipato unachopata sasa.
Kuna sehemu nyingi sana ambazo unaweza kuifanya fedha yako ikuzalishie zaidi. Baadhi ya sehemu hizo ni;
Kuanzisha au kuendeleza biashara, hii ni njia nzuri kama una muda wa kutosha wa kusimamia fedha.
Kuwekeza kwenye mali, vitu kama ardhi na nyumba ambazo utazitumia kuingiza kipato.
Kuwekeza kwenye masoko ya fedha kama kununua hisa, vipande na kadhalika.
Sehemu yoyote unayoweka fedha yako, hakikisha kuna faida zaidi unapata.
Kuna sehemu ambazo watu huwa wanafikiri wamewekeza, lakini ukweli ni wanapoteza fedha. Baadhi ya sehemu hizo ni;
Kuweka fedha benki kwa kuamini unapata riba, hapo unapoteza fedha.
Kununua vitu vya matumizi, kama magari ya kutembelea, kuamini ukiwa na magari mengi ya kutembelea ni mali zinazokuzalishia, lakini ukweli ni hakuna kinachozalishwa kwenye magari mengi ya kutembelea, hasa kama hutumii yote kwenye kazi zako.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.
Hizo ndio sheria tatu muhimu za fedha unazotakiwa kuzijua na kuishi nazo kila siku. Huenda ulikuwa unazitumia lakini ulikuwa hujazijua vizuri, sasa umeshazijua. Ishi nazo na usijaribu kuvunja hata moja hapo, utajiingiza kwenye matatizo makubwa. Na maisha yako kuwa magumu.
Kama utahitaji ushauri zaidi katika maeneo hayo matatu muhimu, jinsi ya kuongeza kipato chako, au jinsi ya kujijengea nidhamu ya fedha au jinsi ya kuwekeza fedha zako tuwasiliane kwa kuniandikia email kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Nakutakia kila la kheri katika kujijengea uhuru wa kifedha.
TUPO PAMOJA,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz