
Moja; watu hatupendi mabadiliko. Ndio hatupendi kabisa. Hatujui ni kitu gani kitakachotokea baada ya mabadiliko na hivyo hii inatuletea hofu zaidi. Tunapenda kufanya kile ambacho tuna uhakika nacho, “nikifanya kazi mwisho wa mwezi nitapewa mshahara. Nikiingia kwenye biashara sina uhakika kama nitapata wateja”. Hivyo hili linawazuia wengi kubadilika.
Mbili; kama mambo yataendelea kuwa kama mtu anavyopenda yawe, mabadiliko hayana nafasi. Kama kila kitu kinakwenda vizuri kwa kile unachofanya sasa, mabadiliko hayawezi kupata nafasi yoyote. Kawaida au mazoea ni adui mkubwa sana wa mabadiliko. Mtu atakuambia “nina kazi inayonipatia chochote ninachotaka, kwa nini nijisumbue na biashara”.
SOMA; Mabadiliko Yanaanzia Hapa…
Tatu; inapokuwa hakuna namna nyingine, mabadiliko hayaepukiki. Hali inapokuwa ngumu na mtu hawezi kuvumilia tena, hapo lazima mabadiliko yatatokea, tena kwa nguvu yoyote ile. Maisha yanapokuwa hatarini hapo mabadiliko yatatafutwa kwa nguvu na gharama yoyote ile. Huu ni wakati ile kazi iliyokuwa inakuridhisha inayeyuka ghafla, au inakuwa ngumu kiasi cha maisha kushindwa kwenda. Pale maumivu ya hali iliyopo sasa yanapozidi hofu ya kubadilika, hakuna kinachobaki ila kubadilika.
Kwa kuwa moja na mbili sio uhakika, basi tatu ndio uhakika, kila kitu lazima kibadilike. Hivyo ni vyema sana ukajiandaa kwa mabadiliko wakati wowote.
Kama mpaka sasa hujasoma kitabu JINSI YA KUNUFAIKA NA MABADILIKO YANAYOTOKEA, kisome sasa kwa kubonyeza hayo maandishi kukipata.
TAMKO LANGU;
Najua mabadiliko ni kitu ambacho hatukipendi ila hakiepukiki. Mabadiliko ndio njia pekee inayotuhakikishia kuwa na maisha bora. Mara zote nitakuwa tayari kwa ajili ya mabadiliko kwa sababu najua siwezi kushindana na mabadiliko.
NENO LA LEO.
The world hates change, yet it is the only thing that has brought progress.
Charles Kettering
Dunia inachukia mabadiliko, lakini mabadiliko ndio kitu pekee ambacho kimeleta maendeleo
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.