Mara nyingi adui yetu mkubwa sio macho yetu wenyewe, bali macho ya wengine.
Kuna watu wengi ambao wamejikuta wakifanya mambo ambayo sio muhimu kwao ila wanafanya tu ili waonekane nao wanafanya au wapo.
Sasa hebu jiulize, kama watu wote duniani wangekuwa vipofu, na wewe pekee ndiye unayeona, je ungekuwa na maisha uliyonayo sasa.
Kama hakuna mtu yeyote ambaye angekuwa anakuona kwa hiko unachofanya au unachomiliki, je ungefanya hivyo?

Kutaka kuonekana na wengine au kufanya kwa sababu kila mtu anafanya imekuwa shimo la wengi kuzika ndoto zao. Wengi wameshindwa kufanya kile ambacho ni muhimu kwao baada ya kujikuta wanafanya kila ambacho kitawapendeza wengine.
Wengi wamekuwa wakivaa mavazi kwa sababu ndio fasheni na waonekane. Wengi wamekuwa wakisukumwa kuwa na vitu vya kifahari sio kwa sababu vinawapa furaha, ila ni kwa sababu wanataka nao waonekane.
Haya ni maisha magumu sana kuishi, lakini cha kushangaza, asilimia 90 ya watu ndio wanaishi maisha haya.
SOMA; Tabia Tano Mbaya Ambazo Kila Mtu Anazo Na jinsi unavyoweza kuzitumia kufanikiwa.
Jifanyie tathmini leo, kama kila mtu angekuwa kipofu ungekuwa kama ulivyo sasa? Kama jibu ni hapana, basi acha mara moja kile unafanya na fanya ambacho ungekuwa tayari kufanya hata kama hakuna anayeona. Lengo hapa sio kukurudisha wewe nyuma, bali kukuwezesha kufanya kile ambacho ni muhimu zaidi kwako.
Na hiki kitakuletea amani, furaha na mafanikio makubwa.
TAMKO LANGU;
Najua kuna vitu nimekuwa nafanya ili nionekane au kukubalika. Nimekuwa nafikiri hii ndio njia ya maisha, lakini nimejua ukweli kwamba hapa ni kuchagua maisha magumu. Kuanzia sasa kama kitu chochote ninafanya au nataka kuwa nacho, na kama kitu hiki nisingekuwa tayari kuwa nacho au kufanya kama hakuna anayeona, basi nitaachana na kitu hiko. Kuanzia sasa nimechagua kuishi maisha yangu na sio ya kusukumwa na macho ya watu.
NENO LA LEO.
Before you try to keep up with the Joneses, be sure they’re not trying to keep up with you.
Erma Bombeck
Kabla hujakazana kufanya kile ambacho wengine wanafanya, hakikisha na wao hawakazani kufanya kile ambacho wewe unafanya.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.