Usiogope Kuanza Na Marekebisho Madogo Madogo Pale Unapogundua Makosa.

Habari za leo mfuatiliaji na msomaji wa makala za Amka Mtanzania, furaha yangu na matumaini yangu wewe ni mzima ndio maana umepata fursa ya kufungua hapa, naamini unaendelea kupambana na una hamasa kubwa ndani yako ya kuendelea kutimiza malengo yako. Hata kama umefika wakati umejisikia kuchoka kwa kutoona matokeo mazuri kwa kile ulichokianzisha isikufanye ukaanza kufanya kwa kawaida, endelea kuweka juhudi zako kubwa zaidi ya uliyoanza nayo, kuonyesha kwamba una nia na malengo ya kukipata hicho unachokihitaji. 

MABADILIKO MADOGO MADOGO YANALETA MATOKEO MAKUBWA.

 
Amini kwamba mafanikio yangekuwa ni rahisi leo hii isingekuwa na maana ya watu kuhangaika kuwa vizuri zaidi kwenye maeneo wanayohitaji, mfano hapa ninapokuandikia ujumbe huu nilianza kuandika saa kumi na moja alfajiri ilipofika na arobaini nikataka kubadili ukurasa niliokuwa natumia kuandikia baada ya kuona unaniletea shida badala ya kukopi mimi nikafuta, hapo nimetumia muda mwingi na nimefika mbali mno kwa kile nilichopanga ujifunze, ki binadamu imeniumiza na wazo la kuacha kabisa kuandika likanivamia lakini nikashindana nalo hatimaye nikaanza tena kuandika. Nilitaka nikuweke sawa kukuonyesha kwamba ili ufanikiwe huhitaji kuzira na kuacha kile ulichokuwa unafanya bali unatakiwa ubadili mtazamo kwa kuendelea mbele na sio kukaa na kuanza kulalamikia kile kilichosababisha ukwame, kukwama kwako kuwe funzo la kufanikiwa zaidi.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.
Mara nyingi tunajikuta tunapitia changamoto ngumu kwa huduma tunazotoa kwa watu, ulijitoa kutatua changamoto waliyokuwa wanaipata wana jamii kwa kuwaletea huduma husika, ili waipate inabidi watoe kiasi fulani cha pesa ili waipate hiyo huduma badala kuonyesha shukrani wanaanza kukulalamikia tena, wamesahau kuwa ili uendelee kuwahudumia zaidi utahitaji wakulipe kwa kile unachowapa, ili kesho uwape tena maana na wewe hupati bure kuna gharama unaitumia kupata hayo.
Una biashara yako ilikuwa inakua vizuri na ilikuwa na wateja wengi sana mwanzoni ila siku zilivyozidi kwenda mbele ukajikuta unabaki na wateja robo ya wale waliokuwa wanakuja kwako, tatizo nini? Kumbe kuna makosa madogo madogo ulikuwa unafanya hukujua walijaribu kukuambia kama vile kukushauri hukuwasikiliza na hukurekebisha kile ulichoambiwa. Marafiki na watu wako wa karibu walikuambia na kukushauri sana usioe/usiolewe na huyo mwanaume/mwanamke kwa sababu za msingi walizokupa na wewe ukaziona kabisa kwa mwenzako kama hatabadilika atakupa shida, ila kwa sababu ya upofu wa upendo ulisema atabadilika tu nikiingia naye kwenye ndoa umesahau kazi ya kumbadilisha mtu si ya kwako ni Mungu na mtu mwenyewe anapoamua sasa mimi kuanzia leo nabadili hii tabia mbaya niliyokuwa nayo na sasa naishi haya maisha yenye kuuletea moyo wangu furaha pasipo kujifariji kwa baya lolote kuwa ni zuri.
Unapojikuta kwenye vipindi kama hivi unafanyaje sasa? Usiogope rafiki yako nipo hapa kukupa maelekezo ya kufuata ili usiendelee kujuta kwa maamuzi uliyochukua hapo awali, cha kufanya ni kuanza kurekebisha yale makosa madogo madogo kama ni kwenye biashara yako, anza kurekebisha zile kasoro zinazomkera mteja, hapa usiangalie ukubwa wa tatizo maana kufanya hivyo utaendelea kupaniki na utaona kuna gharama kubwa sana kufanya marekebisho, kwanza kubali kweli kuna gharama kubwa kuondoa hilo tatizo, pili jua huna hicho kiasi cha pesa kuondoa hayo mapungufu kwa pamoja, ufanyeje sasa, anza na vitu mhimu tu hata kiwe kimoja, anza nacho hatua kwa hatua ukimaliza wape taarifa wateja wako kuwa hilo eneo hakuna tena tatizo, ondoka hapo bila kupumzika nenda hatua nyingine ya marekebisho, usiwe na haraka sana hakikisha na hapa unaondoa kabisa hilo tatizo, vivyo hivyo endelea na kutatua changamoto zingine zilizobakia hakikisha kila hatua ukiimaliza toa taarifa tena hata kwa hao wateja uliobakia nao, kufanya hivyo wataambiana wenyewe kwa wenyewe baada ya muda utajikuta umewarudisha baadhi ya wale waliokuwa wanakupenda kwa huduma zako ila uliwakwaza kwa utoaji wako mbovu wa huduma, na makosa mengine utaendelea kuyaondoa taratibu kadiri wanavyozidi kuleta faida kwenye bidhaa unazowapa maana huwezi kuimaliza changamoto ya leo ukaridhika wakati kila siku kunatokea mabadiliko mapya.

SOMA; Mambo Nane(8) Yatakayokufanya Uwe Na Fikra Chanya Kila Wakati Ili Uweze Kufikia Mafanikio.
Umejikuta umeingia kwenye maisha ya ndoa na mwanaume/mwanamke ambaye hapo awali hukujua kabisa yale matatizo yake uliyokuwa unaambiwa na marafiki zako kutokana na giza la upendo ulilokuwa nalo ndani sasa ameibua makucha yake nje ndio umemfahamu vizuri, umeanza kujuta na kufikiri bora umwache uishi maisha ya peke yako!! Kabla hujafanya hilo ya kutengana naye hebu angalia mtoto/watoto wenu wataishi maisha gani, pili kubali kwamba ulikosea, tatu jisamehe, nne badili fikra zile ulizojua anazo mwenzako kumbe hana na wewe ulipenda awe nazo, sasa hana ,unafanya nini? Badilika kabisa ndani mwako, hii itakufanya uishi maisha mapya ya furaha, na mtaendana tu na mwenzako, hayo ndio maboresho mapya ya kujenga ndoa yako, naona hujanielewa, iko hivi sio kila kufuli/kitasa unaweza kuking’oa na kukitupa pale unapopoteza funguo zake, kumbuka kuna mafundi wa kuchonga funguo ukaendelea kutumia kitasa chako, ya nini uingie gharama kubwa ya kununua kitasa kingine wakati kuna gharama ndogo tu ya kubeba kitasa chako kumpelekea fundi akakuchongea funguo nyingine, ndivyo ilivyo kwenye ndoa yako, kubadili fikra zako ulizokuwa unaishi nazo ni gharama kubwa mno na kuna maumivu makali sana kujifananisha na tabia mpya usiyotarajia, huna namna, maji ulishayavulia nguo hebu oga ukiona yanaharibu ngozi yako ndio uchukue hatua za msingi kumaliza tatizo hilo na si kukimbia maana huyo ni mke/mume wako na si mchumba wako ambaye unaweza kubadilisha pale unapoona tabia mbaya usizozipenda na msizoendana.
Naamini umejifunza vitu vya kufanya pale unapojikuta umeingia kwenye matatizo makubwa na ulikuwa hujui uanze na nini, tumekubaliana tuanze na hatua ndogondogo kwa kuwekeza nguvu ya kutosha ili tuweze kutatua vitu kwa wakati na si kulalamika tukisubiri tutatue changamoto zote kwa pamoja ambapo ni ngumu.
Nikushukuru sana kwa kuwa pamoja nami katika kujifunza haya, usiache kutembelea mtandao huu wa Amka Mtanzania, naamini hutobaki kama ulivyokuwa jana.
Makala hii imeandikwa na rafiki yako Samson Ernest, waweza kujifunza zaidi kwa kutembelea
www.mtazamowamaisha.blogspot.com, kwa mawasiliano zaidi piga/wasap no 0759808081, email; samsonaron0@gmail.com
Ahadi yangu kwako, Tutashirikiana mimi na wewe kujengana.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: