Binadamu sisi ni viumbe wajanja sana.
Na wala sio binadamu tu, ni sheria ya asili.
Kwa mfano, maji yanatiririka kutoka sehemu ya juu kwenda ya chini. Na yakikutana na kizuizi, yanapita njia nyingine ambayo ni rahisi kupita.
Umeme vile vile, unapita kwenye njia ambayo ni rahisi(path of least resistance).
Na sisi binadamu ndivyo tulivyo, tunapokutana na hali ngumu tunaangalia ni kipi rahisi kufanya. Na tukishakipata basi tunaondokana na ule ugumu tuliokutana nao.

Yafuatayo ni baadhi ya mambo rahisi kufanya.
1. Kulalamika na Kulaumu.
2. Kukosoa.
3. Kusema hata mimi ningeweza.
4. Kusema muda haukutosha.
5. Kusema iko nje ya uwezo wangu.
6. Kusema nitafanya kesho.
7. Kukopa.
8. Kuchukia.
9. Kukasirika.
10. Kususa.
Hivi ni baadhi ya vitu rahisi sana kwa kila mtu kufanya pale anapokutana na mambo magumu.
Lakini mambo haya rahisi kufanya yana changamoto yake.
Kitu chochote rahisi kufanya, kwanza hakina thamani kubwa, kwa sababu kila mtu anaweza kufanya.
SOMA; SIKU YA 7; Tiba Rahisi Kwa Walioacha Shule, Walioacha Kazi na Walioacha Maisha.
Hivyo wakati wowote unapojikuta unachagua njia rahisi, jua kabisa ya kwamba unajiondoa kwenye njia yenye manufaa makubwa na kuingia kwenye njia ambayo haina manufaa.
Je hiko ndio unachotaka kwenye maisha yako?
Kama ndio endelea, kama sio usichukue njia ambao ni rahisi, inakupotezea muda wako.
TAMKO LANGU;
Najua ninapokutana na mambo magumu, kitu cha kwanza kufikiria ni njia rahisi ya kupitia. Naweza kuona njia yoyote ni rahisi ila baadae itakuwa na madhara makubwa kwangu kwa sababu inanizuia kupata kile ambacho ninataka. Kuanzia sasa nitaacha kutafuta njia rahisi ya kupita na kuendelea na njia ngumu mpaka pale nitakapopata ninachotaka.
NENO LA LEO.
The path of least resistance is the path of the loser.
H. G. Wells
Njia rahisi kupita(yenye upinzani mdogo) ni njia ya wanaoshindwa.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.