MUHIMU;
Mafunzo ya semina MIMI NI MSHINDI yameshaanza kutumwa. Kama ulifanya malipo na hujapokea mafunzo haya piga simu 0717396253. Tafadhali iwe ulilipa tayari. Kwa sasa hakuna nafasi za kujiunga tena. Asante.

Karibu tena kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto ambazo zinatuzuia kufikia malengo tuliyojiwekea na hatimaye kufikia mafanikio makubwa.
Wiki hii tutaangalia kuhusu changamoto ya kuanzisha biashara ili iweze kukua na kukufikisha kwenye malengo yako.
Mwanzoni mwa biashara kuna changamoto nyingi sana. Na kama hujawahi kufanya biashara nyingine basi unaweza kujikuta unafanya mambo mengi lakini hayana umuhimu kwenye biashara yako.
Watu wengi wanaoingia kwenye biashara, bila ya kupata ushauri wa kina huwa wanajikuta wakifanya mambo ambayo hayana mchango wowote kwenye ukuaji wa biashara yao. Mambo haya huwapotezea muda na hata fedha. 

ANZA KWA KUFANYA YALIYO MUHIMU.

 
Leo tutaangalia moja ya kosa kubwa linalofanywa na watu wanaoingia kwenye biashara kwa mara ya kwanza. Kosa hili linawapotezea muda na fedha na kuwafanya washindwe kufikia malengo waliyokuwa wamepanga kufikia.
Kabla hatujaona hili kwa undani, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili;

Nimesajili jina la biashara/kampuni itakayo dili na kilimo lakini bado sijapata eneo na mtaji vile vile naomba ushauri namna ya kuanza. Kilimo cha Karoti au Vitunguu au Matikiti. Ahsante

Kama tulivyoona maoni ya msomaji mwenzetu hapo juu, tayari amesajili biashara ambayo huenda hata haijui. Mwenzetu amekwenda hatua ya mbali kabisa ya kusajili biashara wakati hajajua anaanzaje biashara, anapata wapi mtaji na mambo mengine muhimu.
Katika kuanza biashara unahitaji kuwa makini sana na kujua ni kitu gani cha kufanya na kwa wakati gani. Kusajili biashara ni jambo muhimu sana ila sio la kufanya mwanzoni mwa biashara, hasa pale unapoanza biashara mpya na mtaji huna au ni kidogo.
Kusajili biashara ni kitu ambacho unahitaji kukifanya pale unapokuwa umeshaona biashara unaweza kuifanya na umeshajifunza changamoto zake na unajua kuikuza unaifikisha wapi. Unaweza kuwa na mawazo mazuri sana ya biashara, lakini unapoanza kuyafanyia kazi ukagundua hukuwa na taarifa za kutosha wakati unaweka mipango yako hiyo, na hivyo kuhitaji kubadili kabisa kile ambacho ulikuwa umepanga kufanya.
SOMA; Umekuwa Kwenye Kazi Muda Mrefu Na Huoni Mafanikio? Zingatia Mambo Haya Muhimu Sana.
Hivyo muhimu sio kusajili bishara hasa mwanzoni, muhimu ni nini basi?
Kuna mambo muhimu sana ya kuanza nayo. Na hapa tutayajadili yale muhimu zaidi.
1. Pata mteja.
Kabla hata hujafikiria biashara itakuwa kubwa kiasi gani, pata kwanza mteja. Jua ni mtu gani ambaye atakuwa tayari kununua bidhaa au huduma unayotoa. Unapopata mteja unakuwa na uhakika kwamba kile unachotoa kuna watu wapo tayari kukinunua na kutumia. Unaweza kuwa na wazo zuri sana la biashara, lakini unapoanza kulifanyia kazi ukagundua hakuna wateja wa biashara hiyo. Au wateja wapo lakini hawatoshi kukupatia wewe soko la kutosha.
2. Ijue biashara nje ndani.
Usisajili biashara halafu ndio uje kuuliza ninafanyaje hii biashara, ni jambo la ajabu sana kufanya. Kabla hujakimbilia kufanya, jua biashara husika nje ndani. Ijue kwa kujifunza kupitia kujisomea mambo yanayohusiana na biashara hiyo. Ijue kwa kuzungumza na watu wanaofanya biashara hiyo. Ijue kwa kuzungumza na wateja wa biashara hiyo. Na ijue kwa kufanya kazi kwenye biashara hiyo. Kwa vyovyote vile jua kila kinachoendelea kwenye biashara husika. Unapoangalia biashara kwa nje ni tofauti sana na kile kinachoendelea ndani ya biashara hiyo husika.
3. Ifanye biashara hiyo kwa ngazi ya chini kabisa.
Watu wengi wanaotamani kuingia kwenye biashara, hasa vijana, na hawana mtaji, huwa wanafikiri kwamba akitokea mtu akawapa mtaji basi wataendesha biashara zao vizuri sana. Huu ni uongo au kujidanganya wenyewe. Biashara sio mtaji, biashara ni utayari wa wewe kupambana na changamoto, kwenda hatua ya ziada, kuvumilia nakuwa na ubunifu. Vitu hivi unaweza kuvijenga vizuri kama utakuwa tayari kuanza biashara yako kwa ngazi ndogo sana kwa kiasi chochote cha fedha ulichonacho au unachoweza kupata.
Una ndoto za kilimo kikubwa, vizuri sana, anza na kilimo kidogo ambacho kitakuhitaji gharama kidogo. Kupitia sehemu hii ndogo utajifunza mengi na pia utawaonesha wengi kwamba upo tayari na hivyo wanaweza kukuongezea mtaji. Lakini kama umekaa chini na unawapa watu hadithi kwamba ukipata mtaji utafanya kilimo, watapenda kusikiliza hadithi zako lakini hakuna atakayekupa mtaji huo. Kwa nini? Kwa sababu kuongea ni rahisi, na biashara ni ngumu.
Kama unapanga kuingia kwenye biashara, tafadhali sana anza na mambo haya muhimu. Anza kidogo, jifunze kila kitu kinachohusiana na biashara hiyo na kazana kupata mteja mmoja kisha mwingine na mwingine. Ndio una ndoto kubwa. Lakini hutaweza kuzifikia kama hutapita huku chini. Anza na haya madogo ya chini na ukishaweza kuyasimamia vizuri, hayo mengine yatafuata.
Kuhusu upate wapi mtaji wa kuanza biashara soma makala hii; USHAURI; Jinsi Ya Kupata Mtaji Wa Kuanzia Biashara.
Fanyia kazi mambo hayo na kama utataka ushauri wa kina zaidi ambapo tunajadili hali yako kwa kina na kuona ni hatua gani unaweza kuchukua bonyeza maandishi haya.
Nakutakia kila la kheri katika kuanza na kukuza biashara yako. kama umejitoa kweli nakuhakikishia hakuna kinachoweza kukushinda.
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
AMKA CONSULTANTS