Kila mmoja wetu ana nembo yake, na ni nembo ya ubora.

Na nembo hii tunaiweka kwenye kila kitu ambacho tunafanya, kila kitu ambacho tunagusa na kila kitu ambacho tunasema au kufikiri.

JE NI NEMBO GANI UNAWEKA KWENYE KILE UNACHOFANYA?
JE NI NEMBO GANI UNAWEKA KWENYE KILE UNACHOFANYA?

Umewahi kuwa mahali na kukawa kuna kitu kimefanyika na aliyefanya hajulikani lakini watu wakasema huyu atakuwa ni fulani?

Kwa mfano ni vitu vimepotea kwenye eneo fulani na aliyepoteza au kuchukua hajulikani, lakini kila mtu ana wasiwasi na mtu fulani?

Au ni kazi imefanyika hovyo sana, na aliyeifanya hajulikani lakini wote wanamwangalia mtu fulani?

Au kazi bora sana imefanyika na kila mtu anakuwa na uhakika ni fulani kaifanya?

Kila mmoja wetu anaacha nembo kwenye kile kitu anachofanya, kile anachogusa kwa mikono yake.

SOMA; UAMINIFU; Jinsi ya kujijengea tabia ya uaminifu.

Jiulize je wewe ni nembo gani umekuwa unaiacha kwenye kila kitu unachogusa. Ukiwa haupo watu wanachukuliaje kazi yako au biashara yako? usijiulize hivi ili kukazana watu wakupende, bali jiulize hivi ili kujua kama nembo unayoacha ni nzuri au la. Kama nembo unayoacha inajitangaza yenyewe na kuwavutia wengine wengi zaidi.

Boresha nembo yako leo, hakikisha yeyote anayeona kazi yako au anayeguswa na kile unachofanya anaona utofauti mkubwa. Hakikisha watu wanategemea makubwa kutoka kwako, na pitiliza mategemeo yale.

Hili ni jukumu ambalo lipo ndani yako, na halihitaji nguvu za ziada, bali linahitaji kujali kwa ziada. Jali sana kuhusu nembo unayoiacha kwenye kila unachofanya. Hii ndio njia rahisi kwako kujitangaza na kuwafikia wengi zaidi.

TAMKO LANGU;

Najua kila kitu ambacho ninakishika ninaacha nembo yangu. Kuanzia sasa nimeamua kwamba nitaacha nembo ambayo ni bora sana na watu watategemea makubwa kutoka kwangu. Na mimi nitawapa makubwa zaidi ili nembo yangu iendelee kusambaa na kuwafikia wengine wengi zaidi. Najua kuboresha nembo yangu hakuhitaji nguvu kubwa bali nahitaji kujali zaidi kile ninachofanya.

NENO LA LEO.

Whoever renders service to many puts himself in line for greatness – great wealth, great return, great satisfaction, great reputation, and great joy.

Jim Rohn

Yeyote anayetoa huduma bora kwa wengi, anajiweka kwenye nafasi ya kufikia ukuu – utajiri mkubwa, faida kubwa, kuridhika, sifa kubwa na furaha kubwa.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.