Habari rafiki msomaji wa makala za uchambuzi wa vitabu. Karibu sana katika uchambuzi wa kitabu kinachoitwa Law of Attraction kilichoandikwa na mwandishi David Hooper. Kitabu hiki kinaelezea sheria ya mvuto (law of attraction) katika maeneo mbalimbali kama vile fedha, kazi, mahusiano, afya n.k. Mwandishi anafundisha kwamba sisi ni kama sumaku na tunavutia vile tunavyoviwaza kwa muda mrefu. Kila mtu ni matokeo ya mawazo yake. Hapa nimekuwekea baadhi ya mambo 20 niliyojifunza kwenye kitabu hicho
Karibu tujifunze
1. Kuna kanuni ya mvuto (law of attraction) ambayo ipo ulimwenguni ambayo inaongoza maisha ya watu na ndiyo nguvu kubwa iliyo nyuma ya vitu vyote. Napoleon Hill ni Mwandishi nguli wa maswala ya mafanikio aliwahi kusema kwamba, tupo jinsi tulivyo kutokana na vile tunavyofikiri. Akimaanisha vile tunavyofikiri kunavutia vitu vingi vinavyotupata katika maisha. Our life is what our thoughts make it.

 
2. Watu wenye mtazamo hasi katika maisha hua wanaonekana ni watu wavivu wasiopenda kuwajibika. Hakuna mtu makini anayependa kufanya kazi na mtu mwenye mawazo hasi kwenye kampuni yake ama hata kua rafiki yake.
3. Watu wengi wenye mtazamo hasi hua wanapoteza kazi zao maana ni wagumu wa kufuata maelekezo, pia si watu wenye kujituma. Wanapenda kutoa visingizio kila wakati, wakati wenzao wenye mtazamo chanya wakibuni njia mpya za kuboresha utendaji wa majukumu yao, wao wenye mawazo hasi wanaishia kulalama, hivyo kukosa ubunifu. Hii hupelekea waajiri wao kuona ni afadhali waondoke, maana kubaki kwao kunaweza kulisha wengine sumu ili wafanane na wao.
4. Watu wenye mawazo hasi hua hawatosheki. Ni ngumu sana kumridhisha mtu mwenye mtazamo hasi, hata utende mema kiasi gani hata kosa la kusema, na ataona bado ulipaswa umtendee vizuri zaidi. People who see a negative future become discontented.
5. Kama tukiamua ku focus kwenye hofu na matatizo ni uhakika kwamba tutavutia vitu vya mtindo huo kuendelea kutokea kwenye maisha yetu. Watu wengi wana hofu ya maisha ya kesho, hawajui kesho itakuaje. Hofu hizo zinatokana na mtazamo wa kuona vitu vinazidi kua vichache (scarcity). Suluhisho sio kua na hofu. Amini kwamba kesho ni nzuri kuliko jana, tambua vitu viko katika utoshelevu (abundance) unahitaji akili ya kuzalisha thamani kwa watu wengine, ili na wewe ufaidi malipo ya thamani unayozalisha.
SOMA; Kama Una Tabia Hii Moja Una Uhakika wa Zaidi ya 90% Wa Kufanikiwa Kwenye Chochote Unachofanya.
6. Mtu mmoja mgonjwa akiambatana na mtu ambaye ni mzima, ni rahisi zaidi wote kuishia kuumwa, kuliko wote wawili kua wazima. Hivyohivyo ukiambatana na mtu mwenye mawazo hasi, ni rahisi wote kuishia kwenye mawazo hasi kuliko kuishia kwenye mawazo chanya. Kaa mbali na wenye negative ideas.
7. Hisia hasi zinatokana na kuona kila kitu hakifai au hakina maana. Wenye mawazo hasi vitu vingi wanavyofanya wanakosa maana (meaning) ya vitu hivyo. Pia huishia kukosoa kila kitu, lakini wakishindwa kutoa suluhu yake. Hali hii hufanya kuvutia zaidi mambo ambayo wanayaona hayana maana. Mtu anaweza kuhama kazi moja kwenda nyingine, kwa kisingizio kwamba kazi ya kwanza sio nzuri ina changamoto kibao, lakini akiishaingia kwenye kazi ya pili baada ya muda utashangaa yale malalamiko yake yamerudi. Ukiona hivyo ujue shida iko kwa huyo mtu na si kwenye kazi anazofanya.
8. Sisi ndio waumbaji wa uhakika au uhalisia wa maisha yetu, na kufahamu ukweli huu ndiyo kitu cha kwanza tunachohitaji kufanya kabla ya furaha kua kipaumbele chetu. Unahitaji kujua kwamba wewe ndiye muumbaji wa furaha yako, wewe ndiye unayeumba huzuni zako pia. Uumbaji huo unaanzia kwenye akili kupitia mawazo yako kisha uumbaji huo unathibitika kupitia matendo na maneno yako. Unahitaji kuwaza mawazo mazuri ya furaha, na kufikiri kwamba furaha ni haki yako na mwenye kukupatia haki hiyo ni wewe mwenyewe.
9. Upendo unalenga zaidi katika kutoa kwa watu wengine na kuwabadilisha watu badala ya kuwadhibiti. Upendo una nguvu sana ya kuweza kuwabadilisha watu kuliko kutumia vitisho. Ukitaka kumbadilisha mtu kirahisi tumia nguvu ya upendo maana itakua rahisi kuvunja nguvu ya ukinzani uliyo ndani ya muhusika, ila ukitumia vitisho utafanya nguvu ya ukinzani iliyo ndani ya huyo mtu kuzidi kuimarika, na kuzidi kua ngumu kwake kubadilika.
10. Watu wengi waliofanikiwa katika shughuli zao (kazi au biashara) asilimia kubwa yao pia ndio waliofanikiwa vizuri kiroho. Hii ina maana waliofanikiwa ni waaminifu kwa Mungu wanaomuabudu. Kumbuka hakuna mafanikio pasipokua na imani ya kufanikiwa.
11. Hatuamini kile tunachokiona bali tunaona kile tunachokiamini. Imani ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Hivyo basi yale yanayokutokea au unayoyapata ni matokeo ya imani yako. Ukiona unakumbana na mabaya tu, ujue mzizi wa tatizo upo kwenye vitu unavyoviamini. Anza kwa kutambua imani hizo ambazo sio sahihi. Kisha epukana nazo.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Pesa Zako Na Kuwa Tajiri.
12. Kitu muhimu katika mafanikio ya muda mrefu hakipo kwenye hiyo kazi unayofanya au kwenye hicho unachokifanya. Kitu hicho muhimu ni kujifanyia kazi wewe mwenyewe wakati unaendelea kufanya hicho unachofanya. Hakuna biashara inayokua kubwa kumzidi mmiliki wake. Ili biashara yako au kazi yako ikue lazima ukue wewe kwanza kwa kujiboresha, kujifunza vitu vizuri kuhusiana na hiyo biashara, kazi au mambo yatakayofanya akili yako ikue. Ukuaji wa kile unachofanya utategemea na ukuaji wa akili yako.
13. Usihofu kufanya vizuri vile vitu vinavyoonekana ni vidogovidogo. Kila mara unapofanikisha jambo vizuri hata kama ni dogo litakufanya ujihisi mwenye nguvu na kua imara zaidi. Ukifanya vizuri mambo madogo basi mambo makubwa yatajishughulikia yenyewe. If you do the little jobs well, the big ones tend to take care of themselves.
14. Uwekaji wa malengo. Kitu muhimu sana katika kuyafikia mafanikio ni kufikiri kwa ukubwa (think big) hasa wakati unapoweka malengo. Jinsi unavyoweza kuweka vitu vizuri katika akili yako, ndivyo unavyoweza kuvifanikisha. Tatizo linalowakumbuka watu wengi si kwamba hawawezi kufikia malengo yao, bali ni kule kushindwa kuweka malengo sahihi ambayo wanayahitaji ili kufanikiwa. Kuweka malengo sahihi ni sehemu muhimu ya mafanikio yenyewe. Kwa maneno mengine unaweza kusema kwamba, ukiweza kuweka malengo sahihi basi umeshapata sehemu ya mafanikio.
15. Malengo yanapaswa kuwa na muda (deadline). Malengo yasiyokua na ukomo wa muda ni ngumu sana kutekelezwa kwa ufanisi, maana kwanza ni rahisi tu kuahirisha, au kuzembea maana utaona bado hujachelewa. Mfano kama una malengo ya kumiliki nyumba yako, unaweka na tarehe na mwaka unaotaka uwe unamiliki nyumba yako. Mfano: Ninamiliki nyumba yangu ifikapo 30.10. 2018. Lakini pia lengo linapokua na maelezo zaidi ndio zuri zaidi maana linatoa picha inayoeleweka zaidi. A goal needs to explain the useful aspects that are going to assist you in your achievement
16. Tumia muda mwingi kufikiria kuhusu malengo yako zaidi kuliko kulalamika. Kulalamika ni kufukuza fursa, yaani utaona vikwazo vingi kuliko kuona fursa mwishowe unakataa tamaa nakuona hakuna kinachowezekana katika vile ulivyojiwekea kama malengo. Njia nzuri ya kuanzia ili kuhakikisha kwamba unayafikiria malengo yako kwa muda mwingi ni kuyaandika malengo yako kwenye karatasi kisha kuyaweka mahali ambapo utakua unayaona kila siku. Unashauriwa kila siku uyasome malengo yako asubuhi kabla ya kuanza shughuli za siku na usiku kabla ya kwenda kulala. Kufanya hivyo kutaifanya akili yako iweze ku focus kwenye vile vitu vyenye uhusiano na malengo yako ambavyo vitakusaidia kuyafikia. Utavutia mazingira, watu na vitu vyenye mchango kwenye malengo yako. Anza leo kwa kuandika malengo yako na kuanza kuyasoma kila siku mara 2.
SOMA; Mambo Nane(8) Yatakayokufanya Uwe Na Fikra Chanya Kila Wakati Ili Uweze Kufikia Mafanikio.
17. Sheria ya mvuto (Law of attraction) inafanya kazi pia katika mahusiano. Mahusiano yenye afya yanahitaji wahusika kuwa na mawazo chanya, waweze ku focus zaidi kwenye vile vitu vinavyowaweka pamoja kuliko vile vinavyowatenganisha. Ukiwa na mawazo kwamba mwenzako sio mwaminifu ni kwamba utavutia kila hali itakayodhibitisha kile unachokiamini. Hata jambo dogo tu utaliona ni kubwa na wakati mwingine linaweza hata kupelekea kutengana
18. Jinenee maneno mazuri hata pale mahusiano yanapokua hayajaenda sawa kama ulivyokua ukitarajia. Wapo watu wengi wakitendwa au wakiachwa na wapenzi wao hujinenea maneno mabaya ambayo ni hasi. Mfano kuna wengine husema “yaani sitapenda tena” kwanza wanaume wote ni sawa au wanawake wote ni wasaliti. Kuna wengine huenda mbali na kusema “ ninahisi nina mkosi sina bahati bora niwe Malaya tu”. Kauli kama hizo hupelekea kuangukia kwenye mahusiano mabaya tena, maana mawazo yao yanawavutia mahusiano ambayo yako kwenye mawazo yao. Yaani umekua na mahusiano na watu kama 5 tofauti tofauti na umeachana nao wote na kisha unaona wote hao ndio tatizo. La hasha tatizo litakua ni WEWE, hebu jichunguze kwanza hua unawaza nini juu ya mahusiano? Unadhani wenye mahusiano mazuri wametoa hongo? au wamepata upendeleo maalumu, Jibu ni hapana, ni kwamba wamelipa gharama. Mahusiano yeyote mazuri unayoyaona yametengenezwa
19. Jikite katika kua bora wewe kwanza kabla ya kukazana kumfanya mwenzako kua bora au kutafuta aliye bora. Hata kwenye Biblia Mungu anasema atakupa wa kufanana na wewe. Hivyo mtu wa kua naye makini ni WEWE. Maana wewe ndiye unavutia mtu anayefanana na wewe. Kwa maneno mengine ni kwamba kama unataka mke au mume bora anza kua bora wewe kwanza. Andika zile sifa za mtu unayemtaka, kisha ukimaliza andika sifa za mtu ambaye atamfaa huyo unayemhitaji kasha anza kuzifanyia kazi kwa kuhakikisha unakua na hizo sifa. Mfano kama wewe ni Kijana wa kiume na unataka mke mwenye sifa Fulani, ziandike hizo sifa za mke unayemtaka, kisha andika sifa za mume ambaye anastahili kuishi na huyo mke mwenye sifa ulizotaja. Kuwa muwazi tu, hata kama hizo sifa huna, wewe ziandike halafu anza kujifanyia kazi WEWE mpaka umepata sifa hizo.
20. Unahitaji kufanya mazoezi mengi sana ili kuweza kushinda mawazo hasi, huzuni na hofu katika maisha. Hebu fikiri kama umekua kwenye dimbwi hilo la mawazo hasi toka unakua mpaka umefikia umri huo ulionao, una uzoefu wa muda gani kwenye upande huo? Jamii na mifumo mbalimbali ya maisha na elimu ndiyo iliyotujengea uzoefu tulionao. Hivyo ili kuondokana na uzoefu huo wa muda mrefu unahitaji kufanya mazoezi mengi sana. Utahitaji kufanya mazoezi ya kuwa na mawazo chanya mara kwa mara mpaka tabia hiyo itakapojijenga na kua tabia ya kudumu. Hiyo ndio gharama ya kulipa. Anza leo ili umalize deni mapema.
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com