Kila mmoja wetu anapenda kudhibiti vitu.
Kuwa na uhakika wa kile anachofanya au anachotarajia kufanya.
Kila mmoja angependa kujua na kuwa na uhakika kwamba kinachotokea ni kama alivyopanga au alivyotegemea.
Lakini pamoja na kutaka huku kudhibiti, ukweli ni kwamba hatuwezi kudhibiti chochote kilicho nje yetu.
Hatuna nguvu hiyo, licha ya kuwa na shauku kubwa lakini hatuwezi.
Tungependa kuona wengine wanafanya kile tunachotaka au tunachotegemea wafanye lakini hawafanyi.
Tungependa kuona dunia inakuwa sawa kwetu lakini mambo hayawi hivyo.
Tungependa kuona tunaowapenda na wao wanatupenda kwa kiasi kile kile lakini hatuwezi kudhibiti hilo.
Tungependa kuona tunaowaamini wanaendelea kuaminika lakini hatuwezi kudhibiti hilo.
SOMA; Kitu Kimoja Ambacho Wanafalsafa Wote Wanakubaliana Ndio Kimekufikisha Hapo Ulipo.
Kila kitu kinaweza kubadilika kwa wakati wowote.
Huwezi kuzuia dunia kubadilika.
Huwezi kuzuia watu kubadilika.
Huwezi kuzuia hali yoyote inayoendelea nje yako.
Na unapojaribu kufanya hivi ndipo unapopata msongo wa mawazo, unapoona maisha ni magumu, unapokata tamaa na kuona maisha hayafai na hayana maana. Lakini maisha ni yale yale, mabadiliko yamekuwa yanaendelea kutokea kwa zaidi ya miaka milioni 4 iliyopita.
Ufanye nini sasa?
Elewa huwezi kudhibiti chochote.
Jua kinachoendelea, kubaliana nacho na ona ni jinsi gani unaweza kukitumia vyema.
Yajue mawazo yako pale unapopata mawazo ya kutaka kudhibiti na jua huwezi kudhibiti ili uangalie njia nyingine ya kusonga mbele.
TAMKO LANGU;
Najua licha ya kutamani sana niweze kudhibiti kila kinachonizunguka, siwezi kufanya hivyo. Naweza kufanya kila ninachoweza, ila siwezi kuzuia mabadiliko. Ninaweza kuyatumia vyema na nikaweza kunufaika nayo, na sio kutaka kuyadhibiti na nikajikuta kwenye wakati mgumu.
NENO LA LEO.
The only thing you sometimes have control over is perspective. You don’t have control over your situation. But you have a choice about how you view it.
Chris Pine
Kitu pekee unachoweza kukidhibiti ni mtazamo wako. Huwezi kudhibiti hali yoyote uliyopo. Lakini unaweza kuchagua uichukulieje.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.
