Habari mwanafalsafa?

Naamini unaendelea kuweka misingi hii ya falsafa kwenye maisha yako ili yaendelee kuwa bora kadiri siku zinavyokwenda. Nikukumbushe tena ya kwamba maisha bila ya falsafa ni maisha ambayo hayana thamani ya kuishi.

Bila ya falsafa utajikuta unafanya mambo ambayo hayana tija kwako au hayawezi kukupeleka kule unakotaka kufika.

Leo katika falsafa yetu hii mpya ya maisha tutaongeza msingi muhimu sana. Msingi huu ni wa kutusaidia kupata chochote ambacho tunataka wengine watupatie. Leo utajifunza kitu ambacho kitakuwezesha kuwafanya wakupe kile ambacho unataka.

Na kabla hatujaenda mbali naomba nikupe tahadhari, hapa hutajifunza jinsi ya kuwalaghai watu. Hapa hujifunzi jinsi ya kuwadanganya watu wafanye kile ambacho ni muhimu kwako ila sio muhimu kwao. Kama unataka mbinu za aina hiyo hapa hutazipata. Utakachojifunza hapa ni njia ya uhakika ya kuwafanya watu waamue wenyewe kukupa kile ambacho wewe unataka. Bila ya kuwalazimisha na bila ya kuwaacha wakijuta kwa nini wamefanya.

Kila mmoja wetu anataka kitu kutoka kwa mwingine.

Hatuwezi kuishi hapa duniani kwa kila mmoja kuwa na maisha yake mwenyewe tu. Tunaishi maisha ya kutegemeana kwa kiasi kikubwa sana. Hivyo unavyoweza kwenda vizuri na watu wanaokuzunguka, ndivyo unavyoweza kuwa na maisha ambayo unayafurahia.

Kila mtu anataka kitu kutoka kwa mwingine, haijalishi una nafasi kubwa kiasi gani, haijalishi una fedha nyingi kiasi gani, bado una mahitaji yako mengi kutoka kwa wengine.

Unataka mwenza wako akupende na kukuheshimu.

Kama ni mwajiriwa unataka mwajiri wako akupe kipato bora kutokana na kazi unayotoa.

Kama ni mwajiri unataka wafanyakazi wako waweke juhudi kubwa kwenye kazi wanayofanya.

Kama ni mazazi unataka watoto wako wawe na juhudi kwenye masomo, wawe na nidhamu na tabia njema.

Kama ni mfanyabiashara unataka wateja wanunue kile unachouza ili maisha yako yaweze kwenda pia.

Kila mmoja wetu kuna kitu anataka kutoka kwa wengine.

Lakini jinsi ya kupata vitu hivi tumekuwa tunatumia njia ambazo sio sahihi.

Unasema mke/mume wangu akinipenda na kuniheshimu nitampa zawadi.

Mfanyakazi wangu akionesha juhudi kwenye kazi nitamwongeza mshahara.

Mwajiri wangu akiniongeza mshahara nitaongeza juhudi kwenye kazi yangu.

Watoto wangu wakiwa na nidhamu na tabia nzuri nitawapa zawadi.

Wateja wangu wakikubali kulipa bei ya juu nitawapa huduma au bidhaa bora zaidi.

Hivyo ndivyo tunavyofikiri mambo yanakwenda, kama wakifanya hivi na sisi tutafanya vile. Lakini kwa bahati mbaya sana mambo huwa hayaendi hiyo. Na hii kusababisha watu wengi kukosa kile ambacho wanakitaka, na maisha yao kuishia kuwa magumu.

Je ungepata njia bora ya kukuhakikishia kupata hayo isingekuwa vyema kwako? Kama itakuwa vyema basi karibu ujifunze njia hiyo hapa.

Njia bora kabisa ya kupata kile unachotaka kutoka kwa wengine.

Kuna njia bora sana unayoweza kutumia na ukapata chochote ambacho unataka kutoka kwa wengine.

Njia hiyo ni wewe kutoa kile ambacho unataka kupokea.

Wape kwanza watu kile ambacho wanataka, na wao watakuwa tayari kukupa kile ambacho wewe unataka.

Ni rahisi kama hivyo, wape watu wanachotaka na wao watakulipa kwa kukupa unachotaka.

Badala ya kusema mume/mke wako akikupenda na kukuheshimu utampa zawadi, hebu anza wewe kumpenda na kumheshimu kama na yeye hatakupenda na kukuheshimu.

Badala ya kusema mfanyakazi akiongeza juhudi nitamwongeza mshahara, hebu mpe motisha, hebu onesha kumuamini kwa kazi anayofanya, na uone kama hataongeza juhudi.

Badala ya kusema bosi akiniongeza mshahara nitaongeza juhudi kwenye kazi, hebu anza nakuongeza juhudi kwenye kazi, ifanye kuwa bora sana na uone kama hatakuongezea mshahara.

Badala ya kusema wateja wangu wakikubali kutoa bei kubwa nitawapa kilicho bora, hebu anza kuwapa kilicho bora kwanza na uone kama hawatakuwa tayari kulipa bei kubwa.

Chochote unachotaka kwenye maisha yako, watu wapo tayari kukupa, kama wewe utaanza kuwapa wao kwanza.

Kama ni rahisi hivi kwa nini wengi wanashindwa?

Kama ni rahisi hivi kupata chochote unachotaka, kwa nini bado watu wengi hawapati kile wanachotaka?

Kwa sababu binadamu tumetawaliwa na ubinafsi. Tunajiangalia sisi wenyewe kwanza, tunaangalia tunafaidika vipi kwanza, tunaangalia sisi ni nini tunapata kwanza, na hivyo kila mtu anavyoangalia hivi, hakuna ambaye anakuwa tayari kuwa wa kwanza kutoa.

Na hapa ndipo wanafalsafa kama sisi tunapopata faida kubwa, kwa sababu tunazijua tabia zetu wanadamu na hivyo tunakwenda kinyume nazo na tunanufaika sana. Kwa sababu tunajua watu ni wabinafsi, tunautumia ubinafsi wao kupata kile tunachotaka. Tunaanza kwa kuwapa kile ambacho wanakitaka, na hivyo wanafurahia na wanakuwa tayari kutupa sisi kile ambacho tunakitaka. Ni rahisi kama hivyo na kama ukianza kutumia njia hii leo, utaona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.

Lakini bado sio rahisi, kuna mambo mawili makubwa unayohitaji kuyafanyia kazi ili uweze kunufaika na hili;

Jambo la kwanza; Jua ni nini watu wanataka.

Unaweza kusema nitawapaje watu kitu wanachokitaka na wakati sijui hata wanataka nini? Sasa hili ndio jukumu lako la kwanza kabisa, kujua watu wanataka nini. Na wala sio jukumu gumu kama ambavyo unaweza kuwa unafikiria.

Binadamu wote tunafanana, kama tulivyoona hapo juu kila mmoja wetu ana ubinafsi, ni kiwango tu cha kuwa tayari kutoa ndipo tunatofautiana. Hivyo kile ambacho wewe unataka, ndio hiko hiko ambacho na wengine wanataka. Hivyo angalia ni kipi ambacho unataka halafu wape wengine.

Bado hujui ni nini wewe unataka? Basi acha nikuambie ni nini mimi ninataka, na wengi watakuwa wanataka hivyo hivyo;

Nataka kupendwa na kuthaminiwa.

Nataka kazi ninayofanya ithaminiwe.

Nataka kusikilizwa na kuonekana ni wa muhimu.

Nataka kulipwa sawa sawa na thamani ninayotoa.

Nataka kupata kilicho bora kwa gharama ninayotoa.

Nataka kuhudumiwa na mtu anayejua kweli kile ambacho anakifanya na ananisaidia kweli kuondokana na tatizo nililonalo.

Hivyo ni baadhi ya vitu ninavyotaka na ninajua kila mtu anataka vitu hivyo. Sasa angalia wale wanaokuzunguka ni jinsi gani unaweza kuwapatia hayo wanayotaka.

Jambo la pili; Kujua kile unachotaka na wanavyoweza kukupa.

Ni vigumu kupata kitu ambacho hukijui. Hivyo wakati unatoa kile unachotoa kwa wengine, jua ni nini unataka na unawezaje kupata kutoka kwao. Kumbuka watu hawatakupa tu kile ambacho wewe unataka, wanahitaji kujua pia ya kwamba unategemea kukipata kutoka kwao, na hii ni baada ya wewe kuwapatia kile wanachotaka.

Unahitaji uvumilivu.

Sio kwamba ukishawapa watu kile wanachotaka na wao hapo hapo watakupa unachotaka. Au watakimbia haraka na kuanza kukupa unachotaka. Ni rahisi kusema na kufikiri hivi. Lakini dunia haiendi hivyo. Unaweza kutoa kile ambacho watu wanataka, na wakakifurahia sana lakini bado wasikupe kile ambacho unataka wewe. Mara nyingi itachukua muda kwa watu kuelewa na kuanza kukupa kile ambacho wewe unataka.

Hivyo usikate tamaa pale unapoona unafanya lakini hakuna majibu, jua bado unapanda mbegu na ipo siku zitazaa matunda. Kuwa mvumilivu na endelea kufanya, baada ya muda utaona faida kubwa sana.

Jinsi unavyowapa wengine kile ambacho wanataka, jua ni mbegu unazipanda. Na hakuna mtu yeyote mwenye akili timamu anayepanda mbegu na kutegemea mavuno siku hiyo hiyo, mbegu zinahitaji muda kukua, kuzaa matunda na kukomaa ndio uanze kuvuna, kuwa mvumilivu kama mkulima mwenye busara.

Jambo muhimu sana la kuzingatia katika kutekeleza hili.

Kama nilivyokwambia mwanzo, hii sio mbinu ya kuwalaghai wengine wakupe kile ambacho unakitaka. Na hivyo usitoe kitu kwa sababu unategemea kupata kitu. Unapotoa, toa kwa moyo wako wote, usitoe kwa moyo mmoja ukijua umetoa kufanya maisha ya wengine kuwa bora. Iwe atakulipa au hatakulipa hiyo sio juu yako, wewe lengo lako kubwa ni kutoa.

Najua hapa inaweza kukuchanganya ukizingatia hapo juu nimekwambia unayempa ajue kuna kitu na wewe unataka. Lakini humlazimishi yeye kukupa, na wala asipokupa sio kwamba utamchukia. Wewe unafanya hivi kwa sababu ndio falsafa ya maisha yako, ndio kitu umeamua kufanya. Na ninakuhakikishia inalipa.

Binadamu ni viumbe wajanja sana, tunajua ni wakati gani watu wanafanya kitu kwa moyo mmoja na ni wakati gani watu wanafanya kitu ili kutuhadaa. Hivyo usipoteze muda wako kujaribu kuwahadaa wengine, watajua na hawatakupa chochote unachotaka. Na kibaya zaidi watakuwa wanakuhadaa wewe. Kwa mfano kama una utaratibu wa kumpa mtu zawadi ili afanye kitu fulani, basi atakuwa hafanyi mpaka umpe zawadi, wewe utafikiri unamhadaa kumbe anakuhadaa wewe.

Unapofanya hili fanya kwa moyo mmoja, fanya kwa sababu ndio umeamua kufanya na ni lazima utalipwa.

Kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako, jua ni kitu gani wengine wanataka, wapatie na wao watakuwa tayari kukupa kile unachotaka.

Ni rahisi kama hivyo na unakuwa na maisha bora sana.

Endelea kuboresha falsafa yako mpya ya maisha, ili uwe na maisha bora zaidi kila siku.

Kila la kheri.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

AMKA CONSULTANTS