Kama unasoma hizi makala za kurasa kila siku, lengo lake kubwa ni moja, kukufanya wewe kuwa bora zaidi, kila siku. Ndio maana kila siku nakupatia mbinu hata kama ni ndogo sana, lakini iweze kukusaidia kufanya maisha yako, kazi yako au biashara yako kuwa bora zaidi. Kila siku bila ya kujali ni sikukuu au la nakuletea makala hizi fupi sana ili uwe na kitu cha kuanzia siku yako. Hivyo ni wewe tu kuchukua hatua na kuianza siku yako ukiwa chanya.

Sasa leo naomba nikuulize swali moja.

Ikiwa utaacha kufanya unachofanya, je watu watagundua haupo?

Kwa lugha iliyozoeleka naweza kukuuliza watu “watakumiss”?

KAMA KWA MBAAALI SANA WATU HAWAKUONI, BASI UMESHAPOTEA, HATA KAMA UPO.
KAMA KWA MBAAALI SANA WATU HAWAKUONI, BASI UMESHAPOTEA, HATA KAMA UPO.

Yaani kama leo umeamua kufunga biashara yako na ukaondoka kabisa, je kuna watu watakaoumia kwa wewe kutokuwepo? Au wataenda tu kwenye biashara nyingine zilizopo kama zako?

Kama leo hii ukaandika barua ya kujiuzulu kazi na kuondoka zako. Je watu wataona pengo lako kubwa? Na sio pengo lile la kuambiwa, tutaona pengo lako, ila lile pengo la watu kusema kabisa kama fulani angekuwa hapa tatizo hili lisingetokea au angeweza kulitatua.

SOMA; Tofauti Kati Ya WORLD CLASS na MIDDLE CLASS(Daraja la kimataifa na daraja la kati).

Kama pengo lako litakuwepo dhahiri na litawaumiza wengi unafanya vyema ila usibweteke na kuona umeshamaliza, endelea kufanya vyema zaidi na zaidi.

Kama ukiondoka watu watasema afadhali, basi kuna pahala umejisahau. Hebu anza kufanya kazi yako vyema. Anza kuweka ubora kwenye kazi yako na mambo yatabadilika.

Kumbuka hufanyi kwa ajili ya watu, ila kipimo kizuri kipo ndani ya wengine.

TAMKO LANGU;

Chochote ambacho nitaamua kufanya kwenye maisha yangu, nataka kiwe mchango mkubwa kwa wengine kiasi kwamba nisipokuwepo pengo langu linaonekana. Hii ni njia bora sana ya kutoa ubora ambao upo ndani yangu. Kila siku nitapigania hili ili niweze kuwa bora zaidi.

NENO LA LEO.

In order to be irreplaceable one must always be different.

Coco Chanel

Ili uwe wa kipekee na uweze kuacha pengo mara zote kuwatofauti.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.