Kwanza, sikufundishi woga, hakuna kitu kibaya kama woga.

Pili, kuna mtu huyu mmoja unahitaji kumuogopa, japo kwa muda mchache tu.

Kwa kumwogopa mtu huyu japo kwa muda mchache tu, hakuna utakachopoteza na utafaidika kwa mengi.

Au kama kumwogopa bado ni vigumu kwako basi mwepuke.

epuka

Maana huyu ni mtu hatari kwa kipindi kifupi sana.

Mtu ninayekwambia hapa ni yeyote ambaye amejipanga kukushambulia kwa njia yoyote ile.

Yaani anakuja mtu amejipanga kabisa kugombana na wewe. Tayari amejipanga kukutukana, au kukuambia maneno mabaya au hata kukudhuru kwa vitendo.

Hata kama wewe ni shujaa kiasi gani, hata kama unaweza kumwambia maneno makali kiasi gani, mwogope kwa kipindi hiko kifupi.

Kwa sababu mwenzako alishajiandaa vya kutosha ila wewe hukuwa na maandalizi yoyote. Hivyo kama utaingia kwenye mtego wake atakukomesha. Ni vyema ukatumia busara kuondoka kwenye hali hiyo.

Wanasema ukipambana na mjinga, anachokifanya ni kukuteremsha mpaka ufikie ngazi yake ya ujinga halafu anakushinda kwa uzoefu. Yeye si amezoea ujinga?

Pia wanasema nguruwe akikupiga na wewe ukarudisha, wote mtaishia kuchafuka matope, nguruwe atakuwa nafurahia wakati kwako itakuwa aibu.

SOMA; Hii Ndio Sababu Kwa Nini Watu Wanafurahia Pale Unapoanguka…

Nakuandikia hili leo kwa sababu watu wengi wamekuwa wakishindwa kufanya mambo yao kwa kujikuta wanaingia kwenye mitego ya wajinga na wanagaragazwa kweli. Hii inawazuia wengi kufikia mafanikio makubwa.

Kubali kuonekana mjinga kwa muda mchache, lakini ubaki na ushindi mkubwa ndani yako. Kuliko kufikiri utamkomesha mtu halafu akakufanya uonekane mjinga daima.

TAMKO LANGU;

Najua kuna watu wengi wamejiandaa kunishambulia kwa njia mbalimbali. Njia nzuri ya kuwashinda watu hawa sio kujibu mashambulizi wanaponishambulia, bali kuwaepuka kwa njia yoyote ile. Ni bora nionekane mjinga mbele ya mjinga, kuliko kutaka kumuonesha mjinga halafu akanifanya mimi kuwa mjinga mwenzake. Nitaepuka mtu yeyote aliyejiandaa kunishambulia kwa ujinga.

NENO LA LEO.

“Never argue with an idiot. They will only bring you down to their level and beat you with experience.”

― George Carlin

Kamwe usishindane na mpumbavu. Atakushusha kwenye ngazi yake ya upumbavu halafu atakushinda kwa uzoefu.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.