Habari mpenzi msomaji wa mtandao huu wa Amka Mtanzania? Natumaini unaendelea vema katika kufikia malengo ya safari yako ya mafanikio na karibu katika makala ya leo ambapo leo tutazungumzia kuhusu kuwa na fikra chanya/mtazamo chanya na kuwa na fikra hasi ina athari gani katika maisha yako ya kila siku.
Ufunguo wa kwanza katika maisha ya binadamu ili afikie mafanikio ni kuwa na mtazamo chanya kwanza na kuwa na mtazamo chanya katika maisha yako au kuwa na mtazamo hasi hilo ni chaguo lako hakuna mtu aliyekuchagulia. Kama unataka kubadilika, badili kwanza fikra yako kuwa na fikra chanya hapo utaona mabadiliko. Kama akili yako haina mtazamo chanya basi ni hatari sana.

UNAONAJE HIYO BILAURI, IMEJAA NUSU AU IPO TUPU NUSU?

 
Tunatakiwa kuishi maisha ya fikra chanya wakati wote, weka akili yako katika ushindi, mafanikio, weka matarajio ya kufanikiwa. Ukiwa na fikra chanya utachagua kuwa na furaha, utachagua kuwa na imani ya kuwa mshindi. Maisha ya kuishi mtazamo hasi ni maisha mabaya sana huwezi kufanikiwa unajiwekea vikwazo mwenyewe na wasiwasi wa maisha.
Kuishi maisha ya mtazamo chanya ni kuishi maisha ya kuamini katika uwezekano, mhubiri maarufu nchini marekani Joel Osteen anasema hivi wachukue watu 10 wenye mtazamo chanya na watu 10 mwenye mtazamo hasi wapatie maswali sawa halafu utaona majibu yao baadaye. Watu wenye mtazamo chanya lazima watatoa majibu yenye uwezekano wa kufanyika lakini watu wenye mtazamo hasi watatoa majibu ambayo yana mtazamo hasi majibu ambayo hayana uwezekano.
SOMA; Mambo Nane(8) Yatakayokufanya Uwe Na Fikra Chanya Kila Wakati Ili Uweze Kufikia Mafanikio.
Binadamu akikosa fikra chanya maisha yake yanakuwa ni ya wasiwasi tu huamini katika kushindwa wakati wote. Unapoamka asubuhi ni vema ukaanza siku yako na kuingiza habari chanya na siyo hasi, amka ukiwa na hamasa kubwa ya kwenda kufanya shughuli zako ukiwa na mtazamo chanya wa kushinda na siyo kushindwa.
Mwanafalsafa mkubwa aliyeiongoza Roma, Marcus Aurelius alisema hivi ‘’our life is what our thoughts make it’’ maisha yetu yanajengwa au kutengenezwa na mawazo yetu.
Kama mwanafalsafa huyu anavyosema maisha ya yetu yanajengwa na mawazo yetu, kwa hiyo kama unaishi maisha ya mtazamo hasi basi maisha yako yatakuwa hasi tu na kama unaishi maisha ya mtazamo chanya maisha yako yatakuwa mazuri yenye mtazamo chanya utakuwa unaamini katika uwezekano wa kushinda na kufanikiwa.
Kama utafikiria mawazo yenye furaha utakua na furaha, ukifikiria mawazo mabaya basi mabaya yatakupata, ukifikiria mawazo ya kua na woga basi woga utakupata, ukiwa na fikra za kuumwa na utakua mgonjwa, ukifikiria kushindwa utashindwa.
Hivyo basi, uchaguzi wa maisha yako uko mikononi mwako, kuchagua kuishi maisha ya fikra chanya au hasi. Ili tuweze kubadilika kwanza na tuweze kufikia mafanikio kwanza tubadilike kimtazamo/kifikra kwanza.
Ndugu mpenzi msomaji, sasa tuangalie dalili za mtu mwenye fikra hasi katika kufikia mafanikio.
1. Wanaamini katika Kushindwa
Kabla mtu hajafanya kitu chochote ameshatanguliza kushindwa kauli za kujinenea kushindwa nayo akili inapokea inajijengea picha ya kushindwa. Kufanya hivi ni kuathiri akili yako kabisa unadhoofika kimwili na kiakili pia. Kama wewe una dalili hii acha mara moja na ingia katika kundi la mawazo chanya lenye uwezekano.
SOMA; Mambo 4 Yanayosababisha Uwe Na Fikra Hasi.
2. Wanachukia Matajiri
Kuwachukia matajiri ni kuchukia mafanikio, watu hawa matajiri wanachochea mafanikio katika jamii sasa kama unawachukia utajifunza kwa nani? Ni muhimu kujifunza kutoka kwa matajiri au kwa watu waliofanikiwa katika mambo mbalimbali.
Fikra za watu wenye mtazamo hasi hawapendi kuona watu wakifanikiwa.
3. Hawapendi Kuona Mtu Akibadilika
Siku zote watu wenye mtazamo hasi wanapenda kukuona ukiwa kama wao walivyo hawapendi kuona mtu abadilike kabisa wanataka ufanane nao, ukibadilika tayari umejenga uadui. Adui yako hawezi kukusemea mema hata siku moja kwa sababu hamuendani kifikra na wala kiitikadi.
4. Hawapendi Kufanya Kazi
Chunguza katika jamii yako unayoishi utawaona watu wenye mtazamo hasi ambao hawapendi kufanya ila wanapenda kua na hela na mafanikio kazi yako ni kukaa na kupiga stori mtaani wakiamini maisha yao yatabadilishwa na wengine. Sasa bila kufanya kazi na kujishughulisha utapataje maendeleo? Kama unaamini mafanikio bila kufanya kazi katika dunia hii hujajua thamani yako ya wewe kuwa hapa duniani.
5. Hawapendi Kujifunza
Wanapenda kulalamika sana na kufikiria maisha yao yatabadilishwa na wengine. Maisha yako yatabadilika kutokana na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Pendelea kujifunza ingia katika mtandao wa google utajifunza mambo mengi, soma vitabu na mengine mengi yanayohusiana na kujifunza.
SOMA; Kama Wewe Ni Kijana Unayataka Mafanikio,..Huu Ndio Ukweli Unaotakiwa Kuujua Ili Kufanikiwa.
6. Wanaamini Mafanikio Yanakuja Ghafla
Mafanikio hayatokei kama ajali au kama radi mafanikio ni safari, ni hatua kama vile unavyopanda ngazi na huwezi kupanda ngazi ukiwa umeweka mikono mifukoni lazima upande ngazi na siyo kupanda lift katika safari ya mafanikio.
Kaa mbali na mtu mwenye mawazo au fikra hasi, ishi maisha yenye mtazamo chanya wakati wote.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com