Tunaendelea kuongeza misingi kwenye falsafa yetu hii mpya ya maisha.

Kumbuka kila mara kufuata misingi hii. Usiache hata siku moja kufuata misingi.

Misingi hii tunayoiweka kwenye falsafa yetu mpya ya maisha ni misingi ambayo imedhibitishwa kuleta matokeo mazuri kwenye maisha. Ni misingi ambayo imetumiwa enzi na enzi na imekuwa inaleta majibu mazuri sana kwa wale wanaoitumia.

Hatua ya kwanza ya kufikia mafanikio ni kuangalia waliofanikiwa wanafanya nini na wewe kufanya. Na kwenye falsafa yetu mpya ya maisha, tunaangalia waliokuwa na maisha bora wamekuwa wakifanya nini, wamekuwa wanafuata misingi gani na sisi kufanya kama wao.

Leo tutaongeza msingi muhimu sana kwenye falsafa yetu hii mpya ya maisha. Msingi huu pale utakapoutumia utakupa nafasi kubwa sana ya kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa. Msingi huu utakutenganisha na kundi kubwa la watu ambao wanaishi maisha ya kawaida, ambao wapo tu kusukuma siku.

Kabla hatujaangalia msingi huu muhimu, tuangalie kwanza msingi huu ulipojengwa.

Msingi tutakaojadili leo umejengwa kwenye tabia moja ambayo binadamu wote tunayo. Na tabia hii ni uvivu.

Kila mmoja wetu ni mvivu, hata wale ambao tunawaona wanachapa kazi sana, wana tabia ya uvivu ila wao wameweza kuidhibiti tabia hii na kuweza kufanya zaidi.

Hivyo watu wengi wanaokuzunguka ni wavivu. Hawapo tayari kuweka jitihada kubwa ili kupata kile wanachotaka kupata. Wanataka kuweka nguvu kidogo na kupata matokeo makubwa. Sio vibaya, ila pia dunia haiko hivyo.

Kama ni kwenye ajira basi watu hawa wanafanya kazi kwa kiwango kile ambacho hawatafukuzwa kazi. Wanafanya kidogo sana. Na wakati mwingine wanafanya vile ambavyo vitawafanya waonekane kama wanafanya kazi sana, kumbe ukweli ni kwamba hawafanyi kazi. Kwa muda wa kazi wanaokuwa nao, nusu wanautumia kufanya vitu ambavyo havihusiani na kazi kabisa. Wanasubiri sana muda wa kuondoka ufike na wanafurahi sana. Siku nyingine inapoanza wanajisikia vibaya sana kwenda tena kwenye kazi.

Kama ni kwenye biashara, watu hawa wanatoa huduma au bidhaa kwa kiwango cha chini sana kiasi kwamba mteja hatokimbia. Wanajitahidi sana kuhakikisha wanapata faida kubwa huku wakitoa thamani na mteja kuendelea kuwa nao. Hivyo wanaweza kudanganya, wanaweza kuficha baadhi ya taarifa ili tu mteja aendelee kufanya biashara na wao.

Hivyo tuna dunia ambayo imejaa watu wengi wanaotafuta njia ya mkato ya kupata kile wanachotaka. Hawapo tayari kuweka juhudi kubwa na wanataka kupata matokeo makubwa zaidi.

Lakini kama tulivyojifunza kwenye misingi mingine iliyopita, dunia haifanyi kazi hivyo. Dunia inajibu kama unavyouliza, inarudisha kwa kiasi kile kile ulichotoa. Kama unatoa kidogo unapokea kidogo. Kama unatoa kikubwa unapokea kikubwa. Ndivyo ilivyo kwenye maisha, kazi na hata biashara. Weka juhudi kidogo na unavuna kidogo, weka juhudi kubwa na unavuna kikubwa. Lima shamba heka moja na utapata mavuno yanayoendana na heka moja. Lima heka kumi na utapata mavuno yanayoendana na heka kumi. Ndivyo ilivyokuwa, ndivyo ilivyo na ndivyo itakavyoendelea kuwa kwa siku zijazo.

Tabia hii ya binadamu inakusaidiaje?

Sasa tabia hii ya watu kuwa wavivu, watu kutokuwa tayari kuweka juhudi kubwa, inakusaidiaje?

Inakusaidia kwa kiasi kikubwa sana.

Kwanza kabisa kwa watu wengi kutokuwa tayari kwenda hatua ya ziada, wanaacha pengo kubwa sana ambalo akipatikana wa kuliziba basi ataleta mabadiliko makubwa.

Hebu fikiria eneo la kazi ambapo wafanyakazi wote wanafanya kazi kwa mazoea, wanafanya kwa kiwango kidogo sana ili tu wasifukuzwe. Wanatumia muda wao wa kazi kufanya mambo ambayo hayana mchango wowote, na uzalishaji wao ni wa chini sana. Huoni ni jinsi gani kuna pengo kubwa la kuzibwa na mtu atakayekuwa tayari kufanya kazi zaidi ya hawa wengine?

Hebu fikiria kwenye biashara ambayo wafanyabiashara wanafanya kwa mazoea, wanakazana kutoa thamani kidogo na kupata faida kubwa. Wanawadanganya wateja au kuwanyima taarifa muhimu ili waendelee kunufaika. Huoni kwamba kuna nafasi kubwa sana kwa mtu atakayeamua kuingia kwenye biashara hii na kutoa thamani kubwa, kuwa mwaminifu na kutoa huduma bora kufanikiwa kupitia biashara hii? Je kama kuna huduma umekuwa unailalamikia sana, na akaja mtu anaitoa kwa ubora wa hali ya juu, je utaendelea na wale uliokuwa unawalalamikia au utaenda kwa huyu mpya?

Msingi muhimu sana.

Sasa msingi muhimu sana wa kujijengea kwenye falsafa yetu mpya ya maisha ni KWENDA HATUA YA ZIADA kwenye kila jambo unalofanya kwenye maisha yako.

Chochote ambacho unaamua kufanya, nenda hatua ya ziada. Kuwa tayari kuweka kazi kubwa na juhudi kwenye kile unachofanya zaidi ya wengine wanavyofanya. Kuwa tayari kuongeza thamani kubwa kwenye kile unachofanya. Kuwa tayari kuona maeneo ambayo hayajaguswa na wewe kuyagusa.

Msingi huu muhimu utakufungulia njia nyingi sana ambazo ulikuwa hujawahi kuziona au kuzifikiri zipo. Utaona ni jinsi gani ambavyo watu walikuwa wanasubiri mtu kama wewe utokee ili matatizo yao yaweze kutatuliwa. Utaona jinsi ambavyo watu wengi watakavyofurahia ile thamani kubwa unayotoa.

Kwenda hatua ya ziada sio tukio, bali ni mfumo wa maisha.

Utaniuliza sasa nikienda hatua ya ziada na nikapata mafanikio si wengine nao wataanza kwenda hatua ya ziada? Ndio kuna ambao watafanya hivyo na hilo halina shida yoyote kwako. Hii ni kwa sababu huendi hatua ya ziada mara moja na kupumzika. Hili ni tukio linaloendelea kila siku. Kila siku unaenda hatua ya ziada, hata kama hakuna ambaye anakuja. Wewe unaenda sio kwa sababu wengine wanaenda, ila kwa sababu unajua unakotaka kufika na unajua njia hii ndio itakayokufikisha. Kama wengine watafuata njia hii ni vizuri sana na sio tatizo kwako.

Ufanye nini?

Leo hii kaa chini na utathmini kazi au biashara unayofanya. Angalia kwa undani sana jinsi ambavyo wewe mwenyewe umekuwa unaifanya. Kisha angalia jinsi ambavyo wengine wamekuwa wanaifanya. Halafu angalia ni maeneo gani ambayo hayajaguswa kabisa. Ni sehemu gani ambazo bado kuna nafasi kubwa ya kwenda hatua ya ziada. Jua maeneo hayo na yafanyie kazi.

Pia angalia watu ambao wamefanikiwa sana kwenye lile eneo ambalo na wewe unataka kufanikiwa zaidi. Angalia ni hatua gani ya ziada ambayo walikwenda. Angalia ni kipi kikubwa walikuwa tayari kufanya wakati wengine walipokuwa wanaendelea kufanya kwa mazoea. Jua mambo haya na yafanyie kazi.

Angalizo kwenye kwenda hatua ya ziada.

Sio kwamba ukishaamua kwenda hatua ya ziada basi mambo yako yatanyooka, mambo yatakuwa mteremko na mafanikio utayaona haraka. Kabla hujaendelea kufikiri hivyo naomba uchukue maangalizi haya;

1. Kwenda hatua ya ziada ni kazi ngumu sana.

Ni rahisi kusema lakini ngumu kufanya. Utahitaji kufanya kazi kubwa na ngumu. Utahitaji kufanya kazi kwa muda mrefu kuliko wengine wanavyofanya. Utaona wenzako wakichelewa kufika na kuwahi kuondoka, wakati wewe utahitaji kuwahi sana kufika na kuchelewa sana kuondoka. Utaona wenzako wakienda kupumzika wakati wewe bado una mengi ya kufanya. Nakuambia sio rahisi.

2. Utakatishwa tamaa.

Ingekuwa ni kazi ngumu tu halafu watu wanakuacha mwenyewe uende na mambo yako, mbona kila mtu angeweza kwenda. Ugumu zaidi unakuja pale ambapo watu wanakukatisha tamaa. Watu watakuambia maneno mengi sana ambayo ukiyaangalia kwa uhalisia yanaleta maana. Watakuambia unajisumbua bure, hata ukifanya sana bado kipato chako hakitaongezeka, kwa nini usifanye tu kawaida. Na wewe ukiangalia inakuja kweli kwamba licha ya kueka jitihada kubwa bado unakuwa huoni mabadiliko makubwa kwenye kipato. Watakupa na mifano ya wengine waliojaribu kama wewe na wakashindwa. Unaweza kuwa tayari kuweka kazi, lakini maneno ya watu, ni sumu. Inaweza kukumaliza haraka sana.

3. Utakutana na changamoto.

Mpaka sasa hii inabidi iwe kawaida kwako, maana hata usipoenda hatua ya ziada basi utakutana na changamoto. Ila changamoto za hatua ya ziada ni kubwa zaidi. Jiandae kukabiliana nazo.

Habari njema.

Pamoja na ugumu wa msingi huu wa kwenda hatua ya ziada, habari njema ni kwamba kama ukienda njia hii, kama utang’ang’ana kwenye njia hii basi utafika mbali sana. Utawaacha wengine wakishindana kwenye vitu vidogo vidogo wakati wewe unakwenda na vitu vikubwa.

Je upo tayari kwenda hatua ya ziada kwenye jambo lolote unalofanya?

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

AMKA CONSULTANTS