Fedha ni somo gumu sana ambalo linawashinda watu wengi. Na ugumu wa somo hili unaanzia na kukosa elimu ya msingi katika makuzi yetu. Fedha ni kitu ambacho kimekuwa kinaonekana kama vibaya kuzungumza na watoto, au kuzungumza kwenye mazungumzo ya kawaida.
Elimu ya fedha, hasa fedha binafsi pia imekuwa haitolewi mashuleni. Hivyo tunakua hatufundishwi kuhusu fedha nyumbani na wala hatufundishwi shuleni. Tunajikuta elimu ya fedha tuliyonayo tumeitoa kwa wengine ambao nao pia wameiga kwa wengine.
Kwa hali kama hii huwezi kushangaa kwa nini matatizo mengi duniani yanaanzia kwenye fedha.
Leo kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio makubwa, tunajadili kuhusu kujijengea nidhamu ya fedha na kuweza kuitumia fedha uliyonayo kukuzalishia zaidi.
Katika makala hii ya leo nitajibu swali la msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kuhusiana na hili la fedha.

KITABU HIKI KINAELEZA SABABU 25 ZA UMASIKINI NA JINSI YA KUONDOKANA NAZO. BONYEZA HAPA KUPATA MAELEZO ZAIDI.

 
Karibu sana tujifunze kupitia changamoto ya mwenzetu aliyotuandikia, huenda na wewe ukawa unapitia changamoto kama hii.

Nimekua nikipata hela lakini nashindwa kuitunza. Nikipata inaishia kwenye pombe. Naomba ushauri wako. J. I

Habari ndugu, kwanza pole kwa changamoto hii unayopitia. Lakini pia hongera kwa kuwa wazi na kujua kwamba hili ni tatizo, maana wenzako wanaona ni sehemu ya maisha. Kwa kuwa tayari kuandika hapa kuhusiana na changamoto hii kunaonesha upo tayari kubadilika kama utapata elimu sahihi.
Ili kuweza kuondokana na tatizo hili la kupata fedha na kuitumia yote mpaka iishe, ni lazima ujue kwanza kwa nini unafanya hivi.
Unaweza kuwa una matumizi mabaya ya fedha kutokana na makuzi ambayo uliyapata. Tangu ukiwa mtoto wewe ulikuwa ukipewa fedha unatumia mpaka inaisha. Huenda hata wazazi wako walikuwa wakiishi maisha kama hayo. Wakiwa na fedha wanatumia mpaka zinaisha. Hivyo na wewe ukachukua huo kama ndio utaratibu wa maisha. Ukweli ni kwamba siyo.
Sasa unahitaji kubadili tabia hii, na napenda nikuambie tabia hii umeifanya kwa muda mrefu hivyo unahitaji muda kuweza kuondokana nayo na pia unahitaji kuweka juhudi kubwa kufanya hivyo. Hapa nitakushirikisha njia ambazo unaweza kuzifanyia kazi sasa na ukaondokana na tatizo lako hilo la matumizi mabaya ya fedha;
1. Weka malengo makubwa na yanayokusukuma.
Moja ya vitu vinavyokufanya uendelee na tabia hiyo ni kukosa malengo makubwa ambayo yanakusukuma sana. Huenda hapo ulipo huna malengo makubwa ya fedha zaidi ya kuzipata na kuzitumia. Kwa mwenendo kama huu utazunguka sana mbuyu, utakimbia sana mbio za panya na umri utakapokuwa umekwenda ndio utakuja kustuka kwamba ulikuwa unafanya nini.
Leo kaa chini na weka malengo yako ya kifedha. Weka malengo ni kiasi gani unahitaji kuwa nacho kwenye akiba kila mwezi, mwaka na hata miaka mitano ijayo. Anza kutekeleza malengo haya.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Pesa Zako Na Kuwa Tajiri.
2. Kuna na bajeti ya matumizi yako ya fedha.
Kitu kingine ambacho kinachochea tabia hii ni wewe kukosa bajeti ya matumizi yako ya fedha. Na hivi unakunywa pombe, huenda ukifika baa unaagiza na kuwaagizia wengine. Na huenda wanakupenda sana kwa hilo.
Sasa leo kaa chini na uweke bajeti ya matumizi yako ya fedha ya mwezi mzima. Jua nyumbani unatumia kiasi gani, jua wewe binafsi unatumia kiasi gani. Jitahidi sana kupunguza matumizi yale ambayo sio ya msingi, ili uweze kubaki na kiasi cha fedha ambacho utaweka akiba. Matumizi yako yote hakikisha yanakuwa madogo kuliko kipato chako, hata kama maisha yatakuwa magumu kiasi gani, ni lazima uanzie hapa.
Kama umezoea kwenda baa na kutoa ofa kuanzia leo acha kabisa huo utaratibu. Kwanza jiwekee utaratibu hakuna kutoa ofa kwa watu wengi, labda mtu mmoja na iwe chupa moja tu. Pili weka utaratibu kwamba hata iweje, hutakuja kukopa pombe. Tatu nenda baa ukijua ni kiasi gani unakwenda kunywa, labda bia mbili, halafu beba fedha ya kutosha kiasi hiko tu. Ukimaliza uliyobeba ondoka na rudi nyumbani. Kumbuka hakuna kukopa, na ofa za wengine usizikimbilie, ni madeni hayo, hakuna cha bure.
Najua hili linaweza kuwa gumu, hasa kwa kuanzia, lakini fanya hivi, kuna watu watakuchukia mwanzoni lakini usijali. Jitahidi sana upunguze kunywa pombe, kwanza ondoka utaratibu wa kwamba kila siku lazima unywe, halafu endelea kupunguza. Usikubali pombe iwe sehemu ya maisha yako, ichukulie kama kitu unachoweza kuamua kunywa au kutokunywa.
3. Wekeza sehemu ambayo huwezi kutoa fedha yako kwa haraka.
Najua nimekwambia hapo juu kwamba uweke akiba, ila najua kama utaweka fedha benki, na ukawa huna fedha ni rahisi kwenda kuzitoa, tena na hizi ATM zilizopo kila kona, ni rahisi kushawishika kutoa fedha.
Kuondokana na hili, wekeza fedha zako sehemu ambayo sio rahisi kuzitoa kama benki. Unaweza kuwekeza kwenye kununua vitu vinavyoongezeka thamani kama ardhi. Lakini ardhi pia itahitaji uwe na kiasi kikubwa cha fedha ambazo utahitaji kuweka akiba miezi kadhaa ndio uweze kununua. Sasa wakati unaendelea kuweka akiba unaweza kujikuta unaitumia tena.
Hapa kuna uwekezaji mmoja naweza kukushauri uufanye, unahitaji fedha kidogo na sio rahisi kutoa fedha zako kama benki. Uwekezaji huu ni kununua vipande vya mfuko wa dhamana ya uwekezaji(UTT). Kwa kununua vipande unakuwa umewekeza fedha zako kwenye masoko ya mitaji na hivyo fedha uliyowekeza kuongezeka thamani. Uzuri wa uwekezaji huu ni kwamba unaweza kuweka kiasi kidogo sana, kuanzia tsh elfu kumi na pia unaweza kuwa unatuma fedha zako kwa kutumia M PESA. Hivyo unaweza kuwa unajiwekea utaratibu kwamba ukipata fedha tu, kitu cha kwanza unatuma sehemu ya fedha hiyo kwenye mfuko huo wa UTT. Njia hii itakusaidia sana.
Kuelewa zaidi kuhusu uwekezaji wa UTT soma makala hii; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja. pia kama utahitaji ushauri zaidi kuhusu uwekezaji tuwasiliane kwa simu 0717396253/0755053887
Kuna mambo mengi sana ambayo unaweza kuyafanya, anza na hayo matatu haraka iwezekanavyo, na kadiri utakavyokuwa unaona matokeo mazuri tuwasiliane. Hii sio kwa aliyeomba ushauri hapa tu, hata kama hujaomba ushauri huu ila ulikuwa na tatizo kama hili fanyia kazi mambo hayo halafu tuendelee kuwasiliana.
Kama ukiwa na dhamira ya dhati ya kuondokana na hilo, ni lazima utaitimiza. Nakutakia kila la kheri kwenye utekelezaji wa haya uliyojifunza. Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nami kwa namba hizo hapo juu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
AMKA CONSULTANTS 
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.