Wafanyabiashara wengi huwa hawaandai michanganuo ya biashara yao kwa matumizi yao wenyewe. Wengi hulazimika kuandaa michanganuo pale ambapo wanahitajika kufanya hivyo na taasisi mbalimbali. Labda mfanyabiashara anataka kuchukua mkopo na moja ya vigezo na masharti ya mkopo ni kuwasilisha mchanganuo wa biashara na jinsi mkopo huo utakavyotumika. Wafanyabiashara wengi huandaa michanganuo kwa njia hii lakini hata wanapopata mikopo hawatumii tena hii michanganuo.
Leo kupitia kona hii ya mjasiriamali nataka nikuambie kwa nini ni muhimu sana wewe kama mjasiriamali au mfanyabiashara uandae mchanganuo wa biashara yako kwa matumizi yako binafsi. Yaani unaandaa mchanganuo wa biashara hata kama huendi kuomba mkopo au kuomba wawekezaji wawekeze kwenye biashara yako.
Tunaishi kwenye kipindi ambacho ufanyaji wa biashara umekuwa na changamoto kubwa. Biashara unayofanya kila mtu anaweza kuifanya na ushindani unaweza kuwa mkali sana. Kama utaingia tu kwenye biashara kwa sababu umeona wengine wanafanya, utajikuta unaendeshwa sana na ushindani unaokuwa kwenye biashara unayofanya. Kuepuka ushindani huu kukusumbua na hata kufikia kukuondoa kwenye biashara , unahitaji kujua umetoka wapi, upo wapi na unaelekea wapi.
Mchanganuo wako wa biashara utakusaidia kwa mambo yafuatayo kwenye biashara yako.
Utakuwezesha kujua utofauti wako na wengine wanaofanya biashara kama yako.
Hata kama biashara unayofanywa inafanywa na watu wengi, bado unalazimika kuwa na kitu cha tofauti ambacho wateja wako hawawezi kukipata kokote. Kitu hiki cha tofauti ndio kinakufanya wewe uendelee kuwepo kwenye soko ambalo linaweza kuwa na ushindani mkali sana. Kwa kuwa na mchanganuo mzuri wa biashara yako, utaainisha wazi ni kitu gani utakachokuwa unafanya tofauti na wafanyabiashara wengine. Na hata pale unapoingia kwenye ushindani na kujisahau, ni rahisi kurudi kwenye misingi ambayo ulikaa na kuiweka kabla hata biashara haijafika hapo ilipo sasa.
Utawajua vizuri wateja wako.
Siri muhimu sana ya wewe kufanikiwa kwenye biashara ni kuwajua wateja wako vizuri. Huwezi kufungua biashara ambayo mteja ni kila mtu. Unahitaji kujua unawalenga watu wa aina gani ili pia iwe rahisi kwako kujua utawafikiaje. Unapokuwa na mchanganuo wa biashara unaeleza wazi wateja wa biashara yako ni watu gani na kuweka sifa zao zote. Hii inakuwa njia rahisi kwako wakati unaweka mikakati ya kuwafikia wateja wengi zaidi au kuongeza wateja wapya kwenye biashara yako.
Unawajua washindani wa biashara yako kwa undani.
Bila hata ya kuwa na mchanganuo wa biashara, bado utawajua washindani wako kwenye biashara. Ila kwa kuwa na mchanganuo utawajua washindani wako vizuri zaidi. Kwa kuandaa mchanganuo utajifunza zaidi kuhusu washindani wako, kujua uimara wao, kujua mapungufu yao, kujua wateja wao na kinachowafanya waendelee kuwepo kwenye biashara. Hii inakusaidia kujua ni maeneo gani kwenye biashara unayofanya sasa bado hayajafikiwa vizuri na washindani wako na hivyo kuweza kuyatumia vyema maeneo hayo.
Utafanya mabadiliko yanayoendana na mpango wa biashara yako.
Biashara za sasa zinabadilika sana, kwa sababu karibu kila kitu kinabadilika. Kama huna mchanganuo wa biashara ambao unaonesha unataka biashara yako iwe wapi miaka mingi ijayo, unaweza kujikuta unayakimbilia mabadiliko ambayo yatakupoteza kabisa kwenye biashara. Ni rahisi kila mtu kukuambia fanya hiki biashara yako itakuwa nzuri. Au fanya kile biashara yako itakua zaidi. Ukiangalia wote ambao wanakupa ushauri huo wala hawafanyi biashara hiyo. Sawa, ushauri ni mzuri lakini sio kila ushauri unaendana na biashara yako. hivyo unapokuwa na mchanganuo wa biashara yako unajua ni ushauri upi unaendana na biashara yako na upi hauendani. Na hata unapoamua kufanya mabadiliko unajua uyafanye kwa njia gani ili uweze kufikia malengo yako makubwa ya kibiashara.
Utajenga utamaduni mzuri kwenye biashara yako.
Unajua kila mahali kuna utamaduni wake, kila eneo la biashara, kila eneo la kazi kunakuwa na utamaduni fulani. Watu wote wanaofanya kazi eneo fulani kuna vitu wanafanya na kuna vitu hawafanyi. Hivyo pia kwenye biashara yako unahitaji kuwa na utamaduni ambao utawaongoza wafanyakazi na wasaidizi wako kuweza kutekeleza majukumu yao vyema.
Mchanganuo wa biashara yako ni muhimu sana kwa matumizi yako binafsi. kama mpaka sasa bado hujawa na mchanganuo wa biashara yako, basi andaa mchanganuo huo. Unaweza kuandaa mwenyewe kama unauelewa kidogo au unaweza kutafuta mtaalamu na mkasaidiana kuandaa mchanganuo wa biashara yako. ukishakuwa na mchanganuo huu maamuzi yako yote muhimu ya biashara unayafanya kulingana na mipango mikubwa uliyoweka.
Nakutakia utekelezaji mwemawa haya uliyojifunza.