Habari mwanafalsafa?
Karibu tena kwenye mfululizo wa makala hizi za falsafa mpya ya maisha ambapo tunaendelea kuongeza misingi muhimu kwenye falsafa yetu hii mpya ya maisha. Kumbuka misingi hii tunayojijengea ni muhimu sana na inabidi tuiishi ili kweli tuweze kuona mabadiliko makubwa kwenye maisha yetu.
Katika moja ya misingi muhimu sana ambayo tulishajijengea kwenye falsafa yetu hii mpya ya maisha ni kitu kimoja ambacho wanafalsafa wote wanakubaliana. Na kitu hiko ni kwamba maisha yetu yanatokana na mawazo yetu. Yaani uko hapo ulipo na jinsi ulivyo kutokana na mawazo ambayo umekuwa unayaweka kwenye akili yako kwa muda mrefu. Na hivyo kama mtu anataka kubadilisha maisha yake, ni lazima aanze kubadili kwanza mawazo yake.
Leo tutajenga msingi mwingine muhimu ambao unaendana sana na msingi huo wa mawazo yako kujenga maisha yako. japo msingi huu unatofautiana kidogo na huo mwingine kwa sababu huu unakwenda moja kwa moja kwenye kile kitu ambacho unakitaka.
Dunia imejengwa katika hali ya upacha, ya vitu viwili vinavyotofautiana katika hali moja. Kuna usiku na kuna mchana. Kuna utajiri na kuna umasikini, urefu na ufupi, kupanda na kushuka, kupata na kukosa na mengine mengi. Kila hali na kila kitu kipo katika hali moja au nyingine inayopingana na hiyo. Na hakuna hali ya kati kati. Wakati mwingine tunaweza kufikiri kuna hali ya katikati lakini hakuna.
Kila mmoja wetu hapa duniani, anataka moja kati ya vitu hivyo viwili vilivyopo kwenye hali ya kutofautiana. Na kwa mtu yeyote ambaye ana akili timamu na anataka kuwa na maisha bora ni lazima atataka kile ambacho ni bora zaidi. Hivyo tunapenda utajiri, tunapenda kupanda, tunapenda kwenda mbele, tunapenda kufanikiwa, tunapenda kupendwa, tunapenda kukua na mengine mengi.
Pamoja na kupenda vitu hivi vizuri ambavyo vina upande wake mbaya, bado maisha yetu hayaanzii kwenye upande huo mzuri, maisha yetu mara nyingi yanaanzia upande wa pili wa hali hizi mbili. Yanaanzia kwenye umasikini, chini, nyuma, kushindwa, kuwa na hofu na hali nyingine kama hizo.
Katika hali hii, jukumu letu kubwa kwenye maisha linakuwa kupambana na kutoka kwenye hali hizi za chini na kwenda kwenye hali zile za juu ambazo tunazitaka. Na hapa ndipo matatizo yote yanapoanzia kwa sababu mara nyingi tunakuwa tunakwenda kinyume kabisa na msingi wa maisha ulivyo.
FIKIRIA KILE UNACHOTAKA.
Kulingana na msingi muhimu wa kwamba chochote ulichonacho kwenye maisha yako, kinatokana na fikra zako. Hivyo ni dhahiri kwamba kama kuna kitu chochote ambacho unataka, inabidi uweke kitu hiko kwenye fikra zako. Kifikirie kwa kina kitu hiko na akili yako itaanza kukuwezesha wewe kuona fursa nyingi za kuweza kupata unachotaka.
Ni muhimu uwe na picha kubwa ya kile unachotaka na kuishi picha hii kila wakati. Ni lazima uweze kutafakari vyema juu ya kile unachotaka. Ni lazima ukijue kwa undani sana, na uweze kueleza kwa ufasaha ni nini hasa unachotaka, na akili yako ikishirikiana na dunia hii ambayo imejitosheleza, itakuonesha fursa nyingi sana za kuweza kupata kile unachotaka.
Hivi ndivyo akili yako inafanya kazi, hivi ndivyo dunia inavyofanya kazi.
Lakini wengi hawafanyi hivi, ni kwa nini?
USIPAMBANE NA USICHOKITAKA.
Kitu kikubwa kinachowafanya watu wengi kushindwa kupata kile wanachotaka ni kwa sababu wanatumia muda wao kupambana na kile ambacho hawakitaki. Wanaweza kuona wamefanya kazi kubwa sana ya mapambano, ila kazi hii ni sawa na sifuri, maana haiwasaidii kwa vyovyote vile kupata kile wanachotaka.
Unapopambana na usichokitaka ni mawazo gani unayojaza kwenye akili yako? mawazo ua kile ambacho wewe hukitaki. Na akili yako inafanyaje kazi? Kwa kuchukua yale mawazo unayoweka kwenye akili yako bila ya kujali ni mazuri au mabaya na kuyafanyia kazi. Hivyo wewe unapojaza akili yako mawazo ya kupambana na kile ambacho hutaki, ile akili yako ya ndani ambayo huwa inapokea kila kitu(subconscious mind) inachukua mawazo hayo na inafikiri ndio kitu unachotaka na hivyo inakuletea fursa za kupata kitu hiko.
Kwa mfano, kama unataka kuwa tajiri, basi kosa kubwa sana unaloweza kufanya kwenye maisha yako ni kupambana na umasikini. Kufikiria kuhusu umasikini, kuuchukia na kulaani umasikini kila mara. Kutumia muda wako mwingi kuzungumza jinsi umasikini ulivyokutesa, kuusema umasikini katika mifumo mbalimbali. Kwa njia hii akili yako inachukua kwamba wewe unachotaka ni umasikini na hivyo inaendelea kukuletea mazingira yatakayoendelea kukuacha kwenye umasikini. Kama unataka utajiri hili liwe neno lako la mwisho kufikiri na kuzungumza kuhusu umasikini.
Hivyo kama unataka utajiri unafanya nini? Unafikiri kuhusu utajiri, unajifunza matajiri wamefikaje pale walipo, unajifunza na kutumia mbinu za kufikia utajiri, unawashukuru matajiri kwa mchango mkubwa walioleta kwenye maisha yako. kwa kuwa na mawazo haya kwa muda mrefu akili yako inachukulia kwamba hiki ndio unachokitaka na inakutengenezea mazingira ya kupata utajiri.
UKICHANGANYA UNAJIPOTEZA.
Watu wengi hufikiri juu ya kile ambacho wanakitaka na kweli kuanza kuvutia kile ambacho wanakitaka. Lakini wakati akili inaendelea kuwaletea fursa za kile wanachokitaka, wanachanganya tena na mawazo ya kile ambacho hawakitaki. Kwa hali kama hii akili nayo inachanganyikiwa, inashindwa kuelewa ni nini hasa unachotaka na hivyo kuacha kukuletea zile fursa ulizokuwa unataka mwanzo na kuanza kukuletea zile hali unazotaka kuona.
Chochote unachofanya kwenye maisha yako, usichanganye hali hizi mbili, chagua moja na ifikirie hiyo, usijihusishe na kile ambacho hutaki, hapa ni kuvuruga mipangilio yako ya fursa ambazo akili yako imeshakusogezea.
Amua ni nini unataka, fikiria kwa kina kile unachotaka, ipe akili yako nafasi ya kuzitambua fursa zilizopo na zifanyie kazi. Upande wa pili wa hali unayotaka, usijihusishe nao kabisa, utakuwa unajipotezea muda wako bure.
HII IPO PIA KWA WATU.
Hata kwa watu wanaotuzunguka, dhana hii inahusika sana. Kama kuna kitu ambacho hukipendi kwa mtu, kama kuna tabia ambayo huipendi kwa mtu, hutaweza kamwe kuibadili kwa kupambana nayo.
Kama mtu anakuchukia, hutaweza kuondoa chuki yake kwa wewe kumchukia pia, sana sana utaongeza chuki hiyo mara dufu.
Kama mtu ni mzembe, hutaweza kuondoa uzembe wake kwa kumkosoa kila mara ambapo anafanya uzembe, hii itamfanya awe mzembe zaidi.
Badala ya kupambana na kile ambacho hukipendi kwa mtu, hebu tumia muda huo kufanya kile ambacho ungependa kukiona kwa mtu huyo.
Kama mtu anakuchukia, hebu wewe mpende, onesha kumjali, na baada ya muda utaona na yeye akifanya hivyo.
Kama mtu ni mzembe hebu acha kumkosoa kila anapofanya uzembe, na badala yake tafuta wakati ambapo anafanya vizuri na msifie kwa hilo zuri alilofanya. Angalia jambo zuri ambalo unajua kalifanya na mpe sifa, sifa hizo ziwe za kweli na usiongeze chumvi. Kwa hali kama hii atapenda kusifiwa zaidi na hivyo atafanya yaliyo bora zaidi na kuwa makini zaidi.
Ukipambana na ambacho hukitaki hata kwa watu, utaendelea kukipata, ukitengeneza kile ambacho unakitaka, ni lazima utakitaka, ndivyo ilivyo, ni sheria ya asili.
JINSI YA KUPATA KILE AMBACHO UNAKITAKA KWELI.
Kuna vitu vingi sana ambavyo huvitaki kwenye maisha yako, kuanza kufikiria vyote hivyo kwanza inakuchosha na kukupotezea muda. Kuliko kupoteza muda wako huo mzuri kwenye kufikiria kitu ambacho hutaki, ni vyema kupeleka mawazo yako yote kwenye kile ambacho unakitaka.
Ili kupata kile ambacho unakitaka kweli, tengeneza picha kubwa ya kitu hiko, ona maisha yako jinsi yanavyokuwa baada ya kupata kile unachotaka kupata. Jione kama wewe tayari unaishi yale maisha unayotaka ukiwa na kila kitu ambacho unataka. Baada ya hapo ifikirie picha hii kila mara, mawazo yako yote peleka kwenye picha hii. Akili yako itafanya kazi ya ajabu na utashangaa kuanza kuona fursa nzuri za kukufikisha kwenye picha ile.
Utapata mawazo yanayokinzana na picha hiyo. Lakini usibembeleze mawazo ya aina hii, yakatae haraka sana, achana nayo haraka sana na rudisha mawazo yako kwenye kile ambacho unakitaka.
Na pale unapoziona fursa zinazoendana na kile unachotaka, CHUKUA HATUA. Kufikiri ni sehemu moja muhimu ya wewe kupata kile unachotaka, ila kuchukua hatua, kufanyia kazi fursa zinazojitokeza ni hatua nyingine muhimu zaidi.
MSINGI WA FALSAFA.
Tuhitimishe kwa kukubaliana kwamba kuanzia sasa, utaacha kufikiri na kupambana na vile ambavyo hutaki na mawazo yako yote utapeleka kwenye kile unachotaka. Usiyagawe mawazo yako, usiyachanganye mawazo yako. jua kile unachokitaka na kifikiri kwa kina. Akili yako, ikishirikiana na dunia iliyojaa kila kitu, itakuonesha fursa nyingi sana ambazo kwa sasa huzioni. Tegemea kilicho chema wakati wote, ondokana kabisa na hofu za kile ambacho hukitaki na utapata uhuru wa kufanyia kazi kile ambacho unakitaka.
Nakutakia kila la kheri katika utekelezaji wa msingi huu muhimu sana wa FALSAFA yetu mpya ya maisha. Usifikiri kwamba haiwezekani, badala yake tumia muda huo kufikiri ni jinsi gani unaweza kufanya.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.