Sababu Tano Kwa Nini Biashara Nyingi Zinazoendeshwa Na Waajiriwa Huwa Zinakufa.

Kama unaendesha biashara na huku umeajiriwa ni muhimu sana usome hapa kwa sababu leo utakwenda kupata kitu muhimu sana kwenye mafanikio ya biashara yako. acha chochote unachofanya na soma hapa neno kwa neno na ujue ni hatua gani utachukua kama kweli upo makini na biashara yako.
Ninayoandika hapa ni kutokana na uzoefu ya yale niliyojifunza kutoka kwa watu wengi ambao nawashauri kwenye biashara zao. Hawa ni watu ambao wamekutana na changamoto kwenye biashara na kila tunapochimba sababu hizi tano zimekuwa zinapatikana kwenye biashara nyingi za aina hii.
Kwanza kabisa ni lazima ujue na kukubali kwamba kuendesha biashara sio kazi ndogo, sio lele mama. Biashara zina changamoto nyingi na biashara zinahitaji umakini mkubwa. Na kuendesha biashara huku bado umeajiriwa ni kazi kubwa zaidi kwa sababu unahitaji kuweza kujigawa kwenye kazi yako na kwenye biashara yako pia. Kwa hili tu biashara zinazoendeshwa na waajiriwa ni ngumu kuliko zile zinazoendeshwa na watu ambao wanafanya biashara tu.

UNAPOFANYA BIASHARA UKIWA BADO UMEAJIRIWA JUA WEWE NI WA TOFAUTI SANA.

 
Katika kushauriana na wafanyabiashara, hasa ambao wameajiriwa, nimegundua mambo haya matano yanasababisha biashara nyingi kupata changamoto na hata kuelekea kufa kabisa. Yajue na anza kuyafanyia kazi.
1. Kukosa muda wa kusimamia biashara.
Kutokana na kubanwa na kazi, waajiriwa wengi huwa wanakosa muda wa kusimamia biashara zao. Huwaachia watu wengine wasimamie biashara hizo na hapa ndipo matatizo mengi yanapoanzia.
Ukweli ni kwamba hakuna mtu anaweza kuwa na uchungu na biashara yako zaidi yako wewe mwenyewe. Hata kama ni ndugu yako wa karibu, hata kama ni mtoto wako, bado umakini unaokuwa nao wewe uliyeweka fedha yako kwenye biashara ni tofauti na wa mtu mwingine yeyote.
Kama unaanzisha biashara huku bado umeajiriwa, hakikisha unapata muda hata kama ni kidogo sana wa kuifuatilia biashara yako. hata kama watu ulioweka wasimamie unawaamini, bado unahitaji kuwa karibu sana na biashara hiyo ili uweze kujua ni nini kinaendelea na pale mambo yanapoanza kwenda vibaya unagundua mapema.
Pangilia muda wako vizuri ili uweze kupata muda wa kuwa kwenye eneo lako la biashara hata kama ni kwa muda mfupi. Kadiri wewe mwenyewe unapokuwa makini na biashara yako, hata wale uliowaweka wasimamie nao wanakuwa makini. Ila wakiona hujali, hata wao hawatojali na haiwaumizi sana pale hasara inapotokea.
Kwa dhana hii hii sikushauri kabisa ufungue biashara mbali na eneo ambalo upo. Wengi waliofanya hivyo wameishia kupata hasara. Mwanzoni mwa biashara unahitaji kuwa karibu sana na kuifuatilia kwa umakini. Ikiwa mbali utashindwa kuifuatilia kwa karibu na itakufa.
SOMA; Maswali Manne (4) Yakujiuliza Ili Uweze Kuongeza Ustawi Wa Biashara Yako.
2. Kuinyima biashara uhuru wa kujiendesha yenyewe, hasa kifedha.
Tabia moja ambayo nimekuwa naona kwa wafanyabiashara wengi ambao pia wameajiriwa na kuinyima biashara uhuru wa kifedha. Watu hawa wanashindwa kutenganisha matumizi ya fedha za biashara na fedha binafsi. wanapokuwa hawana fedha za matumizi, huchukua fedha za biashara na kutumia kwa kujiahidi kwamba watarudisha wakipata mshahara. Wakati mwingine wanarudisha, wakati mwingine hawarudishi.
Sasa iwe unachukua fedha na kurudisha au kutorudisha bado unaiathiri biashara yako kwa kiasi kikubwa sana kwa tabia hii ya kutoa fedha kwenye biashara. Unapotoa fedha biashara inashindwa kusimama yenyewe imara na hivyo inakuwa kama unapiga hatua mbele, halafu unapiga tena nyuma. Utashangaa miaka inakwenda lakini biashara haikui. Hii ni kwa sababu biashara inakosa mtaji wa kujiendesha yenyewe na mara zote inategemea mfuko wako.
Watu wa aina hii hupata shida kubwa sana pale wanapostaafu kwani ndio biashara zao hufa kabisa.
Kuepukana na hili tofautisha kabisa matumizi yako ya fedha binafsi na fedha za biashara. Iache biashara ijiendeshe yenyewe, usitoe fedha kwenye biashara kwa sababu ndogo ndogo. Hata pale unapokuwa na matatizo ya kifedha, usikimbilie kufikiri utapata kwenye biashara, fikiria kama biashara isingekuwepo ungechukua hatua gani? Hii itakusaidia kufikiri zaidi.
SOMA; Wazo Zuri La Biashara Linachangia Asilimia 1 Tu Ya Mafanikio, Asilimia 99 Inatoka Hapa…
3. Fikra ya kwamba hutegemei biashara hiyo kuishi.
Nimewahi kuongea na mfanyabiashara mmoja ambaye pia ni mwajiriwa na yeye wafanyakazi walikuwa wanamsumbua sana. Sasa siku moja akawa anaachana na mfanyakazi na akawa anamwambia kwanza unafikiri mimi nategemea biashara hii?
Fikra za aina hii zimekuwa zinawazuia wafanyabiashara wengi kukua. Wanashindwa kuiendesha biashara vizuri, wanashindwa kujitofautisha na washindani wengine kwa dhana kwamba wao hawategemei biashara hiyo kuishi.
Ni lazima uendeshe biashara yako kama ndio kitu pekee unachotegemea kwenye maisha yako. ni lazima uweke malengo ya kipato unachotaka kutoka kwenye biashara hiyo kila mwezi na lazima ukazane kufikia malengo hayo.
Kama unapata fikra kwamba hutegemei biashara hiyo kwa maisha na hivyo ipo tu, ni afadhali ukaachana nayo kwa sababu itakutesa sana.
4. Kutaka kuishi kama waajiriwa wengine.
Unapofanya biashara huku pia umeajiriwa ni lazima ujue kwamba hapa umeamua kuwa mtu wa tofauti, umeamua kuachana na waajiriwa wengine na hivyo kuchukua njia nyingine ya tofauti. Hii pia ina maana kwamba huwezi kuendelea kuishi kama waajiriwa wengine wanavyoishi.
Kumbuka wale wenzako wana muda mwingi sana wa kufanya mambo yao, wewe huna muda wa kutosha kwa sababu una kazi na una biashara. Hivyo kuna vitu vingi wanavyofanya wewe huwezi kufanya. Labda wakitoka kazini wanakutana eneo fulani kupumzika huku wakiburudika, hilo wewe huliwezi. Labda wafanyakazi wote wanamiliki kitu fulani cha ufahari, jua wewe huwezi hivyo kwa sababu unawekeza kwenye biashara yako.
Kubali kwamba hutaweza kuwa kama waajiriwa wengine na endesha maisha yako kwa utofauti. Utakapotaka kufanya kama wenzako wanavyofanya, biashara yako itapata shida.
SOMA; USHAURI; Ni Biashara Gani Unaweza Kufanya Kwa Mtaji Mdogo Ulionao?
5. Kupeleka tabia za kwenye ajira kwenye biashara.
Waajiriwa wengi sana wanafanya kazi zao kwa mazoea, wanasubiri kusukumwa na wanafanya kidogo sana ili kujihakikishia kwamba hawafukuzwi kazi. Na kama hii ndio tabia yako kwenye kazi, basi utaipeleka tabia hii kwenye kila eneo lako la maisha.
Sehemu kubwa itakayoathirika sana na hili ni biashara yako. kama utafanya biashara yako kwa mazoea kama ulivyozoea kufanya kazi, kama huwezi kuweka ubunifu kwenye biashara yako, utaishia kuua biashara.
Tofauti na ajira ambapo mshahara ni sawa hata kama hufanyi kwa viwango vya juu, faida yako kwenye biashara inategemea juhudi na ubunifu unaoweka. Ukiweka juhudi kubwa na ubunifu mkubwa utaona faida kubwa. Ukiweka juhudi kidogo utapata faida kidogo.
Kama unafanya biashara ukiwa bado umeajiriwa una changamoto ambazo wafanyabiashara wengine hawana. Na hivyo unahitaji kujiweka tofauti na wafanyabiashara wengine na hata waajiriwa wengine. Jipange vizuri ili uweze kukuza biashara itakayokufikisha kwenye malengo yako.
Kama unapata changamoto nyingi kwenye biashara yako na unaelekea kukata tamaa tuwasiliane na ninaweza kuwa kocha wako na tukafanya kazi pamoja kwenye kuiboresha biashara yako na kuikuza. Nipigie simu kwa namba 0717396253.
Nikutakie kila la kheri kwenye ukuaji wa biashara yako.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

2 thoughts on “Sababu Tano Kwa Nini Biashara Nyingi Zinazoendeshwa Na Waajiriwa Huwa Zinakufa.

Add yours

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: