Kwa nini unanijua mimi? Kwa sababu ninaandika, ninaandika kitu unachoweza kusoma, ukaelewa, ukafanyia kazi na ukaona mabadiliko kwenye maisha yako. Sio kwamba ninakaa mahali na kuanza kuwaambia watu, naweza kweli kuandika, ninaweza kuandika vitu vizuri. Badala yake nakaa chini na kuandika, na wewe umenijua mimi kupitia hilo.
Kwa nini unamjua Nyerere? Kwa sababu alikuwa mkombozi wa Tanzania. Alipigania Tanzania kuwa taifa huru na linalojitegemea. Alikazana kujenga umeja wa kitaifa. Na ndio hivyo unamjua. Hakukaa na kuanza kusema ujue mimi naweza kukomboa hii nchi, ujue naweza kujenga mshikamano, alifanya na majibu yakaonekana na tukamjua wote.
Kwa nini unamjua mwanamuziki Diamond? Kwa sababu anaimba, kwa sababu anakazana kutoa nyimbo ambazo zinawaburudisha watu wengi. Na wanazifurahia na tunamjua. Hakukaa chini na kuanza kuwaambia watu kwamba ujue mimi ninajua sana kuimba, naweza kuimba nyimbo nzuri. Badala yake aliimba na anaendelea kuimba na tunaendelea kumjua.
Katika mifano hiyo mitatu niliyotoa hapo juu, nafikiri umeona picha moja nzuri sana, kilichokufanya ukawajua hao watu sio kwa sababu walikuambia wanaweza au uliambiwa tu kuhusu wao. Ila ni kwa sababu walikuonesha wanaweza, kwa kufanya kile ambacho wameamua kufanya, na sio kusema.
SOMA; Kama Unataka Mafanikio, Fanya Kazi Yako Kwa Mbinu Hii…..
Na hata wewe pia, tunaweza kukujua kama ukifanya kazi yako. fanya kazi yako vyema, weka moyo wako pale, hakikisha unatoa thamani kubwa, na hakika tutakujua, tutataka kupata huduma zako zaidi.
Fanya kazi yako na tutakujua. Huna haja ya kutafuta wapi pa kujipendekeza ili uonekane, huna haja ya kuangalia ni jinsi gani unaweza kuwaambia watu na wakakuelewa. Wewe fanya, na fanya kwa ubora, na wale unaotaka wakujue, watakujua tu.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba njia bora ya watu kunijua mimi ni kufanya kile ninachofanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Sina haja ya kuwashawishi watu kwa maneno kwamba ninaweza. Ninahitaji kuwashawishi kwa vitendo, kwa kufanya kile nilichoamua kufanya na wao wenyewe wataona ubora ninaotoa. Nitafanya kile nilichoamua kufanya kwa ubora wa hali ya juu.
NENO LA LEO.
Do your work with your whole heart, and you will succeed – there’s so little competition.
Elbert Hubbard
Fanya kazi yako kwa moyo wako wote, na lazima utafanikiwa. Kuna ushindani mdogo sana kwako kama utafanya hivyo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.
