Kama Utafanya Uamuzi Huu Leo, Utabadilisha Hali Yako Ya Kipato Kabisa.

Maisha ya mwanadamu siku zote yanaongozwa na maamuzi anayoyafanya kila siku. Yapo maamuzi ambayo ukiyafanya yanakupelekea moja kwa moja kwenye kufanikiwa na yapo maamuzi ukiyafanya yanakupelekea moja kwa moja kwenye kushindwa. Kwa hiyo hali yako ya kiuchumi uliyonayo sasa inategemea na maamuzi uliyoyafanya wewe siku za nyuma.
Kama ulikuwa ni mtu wa kufanya maamuzi mabovu basi maisha yako nina uhakika sio mazuri kwa sasa. Kwa lugha nyingine na nyepesi ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na maamuzi sahihi yatakayokuwezesha kubadilisha hali yako ya kipato leo na kesho. Je, unajua ni maamuzi gani unayotakiwa kuyafanya ili kubadili hali yako ya kipato cha sasa na kuwa na mafanikio makubwa?
1. Amua kuwa makini na kile unachokizingatia.
Mara nyingi kile unachokizingatia kila wakati, kila mara na kila siku ndicho kinachoamua maisha yako ya leo na baadae yaweje. Kama wewe mawazo yako kila wakati yamejikita katika tabia mbovu ambazo sio za kimafanikio zitakusababishia itakuwa siyo kitu rahisi sana kuweza kufanikiwa na kubadili hali yako ya kipato ulicho nacho kwa sasa.
Wengi wanaoshindwa kubadilisha hali zao za vipato walivyonavyo sasa utakuta ni watu ambao kiuhalisia wanazingatia sana mambo yanayowatoa nje ya mstari wa mafanikio. Mambo hayo yanaweza yakawa kupoteza, muda, kutokijisomea, kutokujiwekea malengo na mengineyo. Hivyo, ili uweze kufanikiwa ni lazima kufanya uamuzi wa kuwa makini na kile unachokizingatia kila wakati.
AMUA KUWEKEZA PESA ZAKO, HATA KAMA NI KIDOGO.
2. Amua kuwekeza.
Haijalishi unapata pesa nyingi kiasi gani kwenye kile unachokifanya ila kama bado hujaamua kuwekeza zaidi na zaidi, basi hali yako yakipato itabaki vilevile siku zote. Amua kuwekeza katika mambo mbalimbali ambayo yatakufanya uendelee na kuwa mshindi katika maisha yako. Acha kukaa na kubweteka na kuridhika na hali uliyonayo.
Hebu jaribu kuangalia, akina nani ambao ni watu wenye mfanikio makubwa? Utagundua ni wale tu ambao maisha yao wameamua kuwekeza kwa hali na mali. Uamuzi wa wewe kuwekeza ni wa msingi sana katika maisha yako ili uweze kubadili hali ya kipato chako. Weka vitega uchumi vingi kwa kadi unavyoweza, baada ya muda utakuwa mbali sana kimafanikio.
3. Amua kubadili mfumo wa matumizi yako.
Unaweza ukawa unapata kweli pesa ya kutosha inayoweza kukusaidia, lakini kama bado mfumo wako wa matumizi ni mbovu basi sahau kuweza kufanikiwa. Wengi mara nyingi wanaangushwa na matumizi yao mabovu ya pesa.  Wanakuwa ni watu wa kutumia wakati mwingine hata nje ya kipato chao wanachokipata.
Sasa ili uweze kufanikiwa na kuboresha hali yako ya kipato kwa namna yoyote ile ni lazima kuwa makini sana na kile unachokitumia. Umakini huu utakupelekea wewe kutunza pesa nyingi ambaza zingeweza kutumika hovyo bila sababu ya msingi. Ili uweze kufanikiwa na kubadili mfumo wa matumizi yako, Kikubwa cha kufanya jiwekee bajeti ya kukuongoza katika hilo.
4. Amua kuchukua hatua.
Unaweza ukawa umefanya maamuzi mazuri sana hapo juu ya kuwa makini na kile unachokizingatia , kubadilisha mfumo wa matumizi na hata kuamua kuwekeza. Lakini kama utakuwa mtu mzito wa vitendo basi sahau kabisa kuweza kubadili hali yako ya kipato na hadi kufanikiwa. Sana sana utaendelea kubaki kama ulivyokuwa mwanzoni.
Ukifatilia kidogo tu, utagundua kwamba watu wenye mafanikio makubwa mara nyingi ni watu wa kuchukua hatua za kubadili masiha yao kila siku. Hawa sio watu wa kukaa na kusubiri hali fulani ziwatokee, ni watu wa vitendo. Kwa vitendo hivyo hivyo huweza kuwafanikisha. Huu ni uamuzi wa lazima kuuchukua ili kuboresha hali yako ya kipato.
Hayo  ndiyo maamuzi ya msingi  unayoweza kuyafanya leo na kubadili hali yako ya kipato na kuwa mtu wa mafanikio. Kila kitu kinawezekana kwako ukiamua kuchukua hatua.
Kwa makala nyingine nzuri karibu pia kwenye DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Imani ngwangwalu,
Simu; 0713 048 035,

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: