Unapofanya jambo lolote la kukufikisha kwenye mafanikio makubwa, maana yake hili ni jambo kubwa na ambalo huenda hujawahi kufanya, mawazo yako yanaweza kuwa sehemu moja kati ya hizi mbili.
Sehemu ya kwanza ni kufikiria yale matokeo unayotaka kuyapata, kufikiria kile kitakachotokea baada ya wewe kukamilisha hilo. Hapa unaiona picha ya maisha yako yatakavyobadilika baada ya kukamilisha hilo.
Sehemu ya pili ni kufikiria usiyoyajua, hapa unafikiria mambo ambayo hujui kama yatatokea, na mambo yenyewe pia huyajui. Hapa unakuwa umejawa na woga kwa sababu jambo hili hujawahi kufanya basi pia huna hakika ni nini utapata. Kila ukiangalia mbele unaona giza.
Unafikiri ni sehemu ipi bora ambayo kwa kuweka mawazo yako utaweza kufikia unachotaka?
Hii iko wazi, weka mawazo yako kwenye matokeo unayotaka na hii itakupa ujasiri hata pale ambapo unakuwa huna uhakika. Lakini unapoweka mawazo yako kwenye yale usiyojua, unajipa hofu na kushindwa kufanya zaidi.
Fikiria zaidi yale matokeo unayotaka na utaona fursa nyingi za kuyafikia.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Njia Ya Uhakika Ya Kuwafanya Watu Wakupe Kile Unachotaka.
TAMKO LANGU;
Najua ya kwamba ninapofanya jambo la mafanikio, ambalo ni kubwa na sijawahi kufanya, ni rahisi kufikiri zaidi kwenye yale nisiyojua. Najua hofu inaweza kunizuia kabisa kufikiri kile ninachotaka. Lakini sasa nimejua ya kwamba ni muhimu kufikiri yale matokeo ninayotaka maana kwa kufanya hivi itanipa ujasiri wa kuendelea kusonga mbele. Mara zote nitafikiri yale matokeo mazuri ninayotaka kupata na najua nitaziona fursa nyingi zaidi.
NENO LA LEO.
Don’t dwell on what went wrong. Instead, focus on what to do next. Spend your energies on moving forward toward finding the answer.
Denis Waitley
Usizame kwenye yale ambayo yamekwenda vibaya. Badala yake fikiria kile unachokwenda kufanya. Tumia nguvu zako kusonga mbele katika kutafuta majibu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.