Kitabu THE TIME WARRIOR ni kitabu ambacho kinatufundisha mbinu mbalimbali za kuweza kuwa na matumizi mazuri ya muda ili kuweza kukamilisha malengo na mipango yetu muhimu kwenye maisha.

Kitabu hiki kinatoa njia za kuondokana na hali ya kuahirisha mambo, kutaka kuwaridhisha watu, kujishuku wewe mwenyewe, kujiwekea majukumu mengi na pia kuvunja ahadi ambazo umeweka na wengine. Kwa kushindwa kuwa na matumizi mazuri ya muda unajikuta miaka inaenda lakini hujioni ukisonga mbele.

Kama lilivyo jina la kitabu TIME WARRIOR(SHUJAA WA MUDA) hapa unajifunza mbinu ambazo zitakufanya uwe shujaa kweli kweli. Na kama unavyowajua mashujaa hawana huruma, hivyo pia utakapokuwa shujaa wa muda hutakuwa na huruma na mambo ambayo sio muhimu kwako.

Yafuatayo ni mambo 20 muhimu kati ya mengi niliyojifunza kwenye kitabu hiki;

1. Watu wengi hutumia muda mwingi kufikiri na hii inawafanya washindwe kuchukua hatua. Wanapokuwa na jambo la kufanya hulifikiri sana na kulichambua hali inayowaacha wakiwa wamechoka na wasijue wanaanzia wapi. Unapoamua kwamba unataka kufanya kitu fulani, jua ni wapi pa kuanzia na anza mara moja. Kufikiri kwa muda mrefu hakutakusaidia kuanza.

2. Watu wanaofanya kazi zinazoonekana ni za chini na za kudharaulika, na wakazifanya kwa mapenzi na nguvu kubwa, huwa wakipata nafasi za kupandishwa vyeo na baadae kuwa kwenye kazi zenye hadhi kubwa. Hawa ni wale watu ambao wanajua ipo njia hata kama mambo ni magumu kiasi gani. Lakini wale wanaolalamika kwamba kazi ni ya chini na hivyo kutokujituma hujikuta wamenasa kwenye kazi hizo kwa maisha yao yote na hivyo kuwa na maisha magumu.

3. Ifanye leo kuwa siku muhimu na pekee kwako. Chochote kile unachotaka kufanya, sema unakifanya kwa leo tu. Jana isikukwamishe, maana imeshapita, chochote ulichofanya jana huwezi kubadili. Kesho isikutishe, bado haijafika. Hata ungeihofia vipi bado huwezi kuibadili, lakini leo, yaani sasa ndio muda mzuri wa wewe kufanya chochote unachotaka kufanya.

4. Kinachofanya tuone mambo fulani ni mabaya sio ubaya wa mambo hayo, bali mawazo yetu sisi binafsi juu ya mambo hayo. Hakuna jambo lolote lenye maana, bali sisi ndio tunaoyapa mambo maana na kuamua yatufurahishe au yatuumize. Kwa mfano mvua inaponyesha unaweza kuona ni baraka kwamba mazao yatapatikana au unaweza kuona ni mkosi kwamba kutakuwa na mafuriko au kutatokea magonjwa. Mvua ile ile inaweza kuleta mtazamo tofauti.

5. Wewe mwenyewe ndio unayeweza kujihamasisha sana na kufanya jambo lolote kwa ufanisi mkubwa. Jambo lolote lile unalofanya, kuna njia ambayo unaweza kujihamasisha ili kufanya zaidi. Na kama huoni furaha kwenye jambo unalofanya, basi huenda unalifanya kwa makosa.

6. Kinachofanya watu waahirishe mambo ni pale ambapo akili zetu zinafanya mambo yajayo kuonekana makubwa sana na yanayotisha. Kwa hali hii mtu anaogopa kuchukua hatua mara moja na kusogeza mbele, kuahirisha. Njia rahisi ya kuondokana na hali hii ni kutafuta hatua ndogo sana ya kuanzia, na jipe dakika tatu tu za kufanya jambo. Jiambie kwa dakika tatu tu unakwenda kufanya jambo hilo na kaa dakika hizo tatu, zikiisha ongeza nyingine tatu, baada ya muda utajikuta umeshafanya sehemu kubwa sana.

7. Kama utaweza kufanya kazi bora sana, ambayo haijawahi kufanywa na wengine, dunia nzima itakutafuta pale ulipo. Badala ya kupoteza muda kuangalia ni jinsi gani unaweza kuwashawishi watu wajue upo, hebu anza kwa kufanya kazi iliyo bora sana, na watu wataifuata popote ilipo.

8. Kabla hujaanza kuangalia njia za mbali za kuongeza kipato chako, hebu anza kuangalia pale ulipo sasa, hebu anza kumwangalia mwajiri wako wa sasa, ni mambo gani unaweza kumsaidia na akakuongeza kipato. Hebu angalia mteja uliye naye sasa, ni huduma gani bora zaidi unaweza kumpa na yeye akaongeza fedha anayokupa. Fikiri hapo kwa kina na utaona fursa nyingi zaidi.

9. Unahitaji kutenga muda wako wa pekee kila siku, muda huu unaepuka usumbufu wowote na unautumia kufanya mambo ambayo ni muhimu sana kwako au kwa kazi yako. katika muda huu kaa mbali kabisa na usumbufu, usiwe karibu hata na simu. Kupata saa moja ya utulivu kama hii ni bora kuliko masaa matano ambayo unafanya kitu huku unasumbuliwa na simu, watu, mtandao na kadhalika.

10. Hofu inafanya mwili unakuwa katika hali ya kushindwa kuchukua hatua, hali ya ubaridi. Matendo yanafanya mwili unakuwa kwenye hali ya kuchukua hatua, hali ya moto. Hivyo njia bora ya kuondokana na hofu ya kufanya jambo ni kuanza kulifanya jambo hilo.

11. Matumizi bora sana ya muda wako ni kufanya mambo ambayo yanawasaidia wengine. Unapowekeza kwenye kuwasaidia wengine unatengeneza njia kubwa sana ya wewe kufaidika. Matumizi mabaya kabisa ya muda wako ni kujaribu kuwaridhisha wengine, kukubali vitu sio kwa sababu unataka ila kwa sababu tu unataka mtu aridhike, hapa utapoteza muda wako mzuri sana.

12. Kutokuwa na hofu sio sawa na kuwa jasiri. Ukiwa jasiri maana yake hofu ipo ila unakazana kuishinda. Ila kutokuwa na hofu hushindani chochote, bali umeyaweka mawazo yako kwenye hali ya uwezekano na hali ya upendo na hivyo huwezi kuwa na hofu yoyote.

13. Hofu ni kama giza. Huwezi kupima giza, yaani hakuna kitu unachoweza kusema hiki ni giza, bali giza ni ukosefu wa mwanga. Palipo na giza, ukileta mwanga giza linapotea. Hivyo pia kwa hofu, ni ukosefu wa upendo, upendo unapokuja iwe ni kwa mtu, kwako binafsi au kwa kile unachofanya, hofu inapotea.

14. Usijaribu kumbadili mtu kwa kumkosoa, utapoteza muda wako bure. Unapomkosoa mtu anataka kukuonesha kwamba hakosei na hivyo kile ambacho unataka asifanye ndio atakifanya zaidi. Badala yake, kama unataka kumbadili mtu, mpe hamasa, mwoneshe jinsi wewe unavyofanya, na yeye atakuiga na kufanya hivyo pia.

15. Haiba uliyojijengea ni adui mkubwa sana wa mafanikio yako. ukishajijengea picha kwamba wewe ni mtu wa aina fulani, huwezi kufanya vitu fulani, utajinyima fursa nyingi sana. Ishi kutokana na hali iliyopo sasa, kutokana na kile unachoamini sasa kwamba ni sahihi na sio kusema ulichokuwa unaamini zamani hata kama kwa sasa mambo yamebadilika.

16. Ni muhimu sana uwe na kocha au mshauri wa pembeni kwenye jambo kubwa unalofanya kwenye maisha yako. hii ni muhimu kwa sababu unapojikuta kwenye changamoto, mtu wa pembeni anaweza kukupa ushauri mzuri kuliko ule unaoweza kuwa nao mwenyewe. Mtu wa pembeni hajashikamana kihisia na lile jambo unalofanya, ila wewe umeshikamana kihisia, na hisia zinazuia kufikiri sawasawa.

17. Maliza kile unachoanza. Usianze kitu na kuishia katikati, hii itakurudisha nyuma sana. Kadiri una mambo mengi ambayo hujayamaliza ndivyo unavyoshindwa kuanza mambo mengine mapya. Maliza yote ambayo bado hujamaliza na ukianza jambo jipya hakikisha unalimaliza.

18. Kama huwezi kufanya jambo ambalo unaona ni hatari huwezi kukua. Kukua hakuji kwa kufanya mambo yale yale ambayo umezoea kufanya, kukua kunakuja kwa kufanya mambo ambayo yanaonekana ni hatari na unaposhindwa unajifunza zaidi.

19. Ili kuweza kulinda muda wako vizuri, jua ni wakati gani wa kusema NDIO na wakati gani wa kusema HAPANA. Kwa mfano kama ungekuwa unawahi ndege kwa ajili ya safari, mtu yeyote atakayekufanya na kukuomba umsaidie kitu ni lazima utamwambia hapana, na wala haitakuumiza kwa sababu upo kwenye haraka ya kuwahi ndege, lakini katika hali ya kawaida hilo linakushinda. Pale ambapo una jambo mhimu la kufanya, chukulia kama unawahi ndege.

20. Kama unaomba kazi na unaitaka kazi hiyo kweli, basi fanya vitu vya kipekee na vya tofauti sana. Unajua ni vitu gani ambavyo waombaji wa kazi kwa kawaida huwa wanafanya, wewe fanya zaidi ya hapo. Hii itakuweka wewe mbele zaidi kwa sababu pale ambapo sifa za wengi zinafanana atakayesimama ni yule mwenye kitu cha tofauti, je wewe ni kipi cha tofauti unaweza kuonesha kwa wengine?