Ili biashara yako iweze kukua na kukuletea mafanikio makubwa, unahitaji watu makini sana wa kukusaidia kwenye biashara yako. na ili uweze kupata watu hawa makini ni lazima wewe mwenyewe uwe makini kwenye kuajiri. Wafanyabiashara wengi wamekuwa na malengo mazuri sana na biashara zao na wamekuwa wakijitoa sana ili biashara zao zikue. Lakini wafanyakazi ambao wamekuwa wanawaweka kwenye biashara hizo wamekuwa wakiwaangusha.

Leo kupitia kona hii ya mjasiriamali tutaziangalia mbinu bora za wewe kutumia wakati wa kuajiri ili kupata wafanyakazi bora wa biashara yako. baada ya mbinu hizi sasa utaacha kuajiri kwa sababu tu mtu yupo tayari kulipwa fedha kidogo au kwa sababu tu mtu hana kazi. Kama upo makini na biashara yako ni vyema ujifunze mbinu hizi na uzifanyie kazi.

Zifuatazo ni mbinu bora za kuhakikisha unapata mfanyakazi bora wa biashara yako;

1. Angalia uwezo binafsi wa mfanyakazi.

Pamoja na kwamba utahitaji sifa za ujuzi na uzoefu, kuna kitu muhimu sana unachotakiwa kukijua kutoka kwa mfanyakazi unayekwenda kumwajiri. Kitu hiko ni uwezo wake binafsi. ujuzi na uzoefu anaweza kujifunza lakini uwezo binafsi ni kitu kilichopo ndani yake.

Na kwa uwezo binafsi hapa unaangalia uwezo wake wa kufanya maamuzi katika hali za kawaida za kijamii. Japokuwa utampatia majukumu mfanyakazi wako, kuna wakati ambapo anahitaji kutumia busara zake mwenyewe kufanya maamuzi. Ni muhimu mfanyakazi unayemwajiri akawa na uwezo binafsi mzuri wa kufanya maamuzi ambayo yatanufaisha biashara yako.

Utaujua uwezo binafsi wa mfanyakazi unayemwajiri kwa jinsi anavyojieleza na vile anavyojibu maswali utakayomuuliza.

2. Uliza maswali sahihi.

Wakati unapata nafasi ya kumfanyia usahili mtu unayetaka kumwajiri, unahitaji kuuliza maswali sahihi ambayo yatakuwezesha wewe kumjua vizuri mfanyakazi kabla hujamwajiri. Ni katika maswali haya pia utaweza kuujua uwezo binafsi wa mfanyakazi unayetaka kumwajiri.

Uliza maswali ambayo yatakuwezesha kujua mfanyakazi wako ana malengo gani ya baadae. Pia jua kwamba anaichukuliaje kazi unayokwenda kumpatia, jua ni nini kinamfanya atake kazi hiyo. Jua ni mchango gani anaoleta kwenye kazi unayokwenda kumpa. Japo lengo la kufanya kazi ni fedha, lakini ukipata mfanyakazi ambaye anaipa kazi uzito wa ziada na sio tu fedha, utakuwa umepata mfanyakazi bora sana.

Kwa kuuliza maswali sahihi na yanayomfanya mtu kufikiri unakuwa umepata nafasi ya kumjua vizuri mfanyakazi kabla hujamwajiri.

3. Angalia kwenye mitandao yake ya kijamii.

Kwa sasa watu wengi utakaokwenda kuajiri ni vijana, na vijana karibu wote wapo kwenye mitandao ya kijamii. Ni vyema kama utajaribu kutafuta jina la mfanyakazi unayetaka kumwajiri kwenye mtandao na utaletewa taarifa zake anazoweka kwenye mitandao ya kijamii. Kwa kupitia yale mambo anayoandika kwenye mitandao hii ya kijamii unaweza kujua ni mtu wa aina gani unayekwenda kumwajiri.

Japokuwa unaweza kufikiri mitandao ya kijamii ni sehemu ambayo mtu ana uhuru wa kushirikisha chochote anachotaka, pia hapo ndipo pa kumjua mtu vizuri. Mtu kwenye wasifu wake anaweza kukuandikia ni mchapa kazi, anapenda kusoma na kujifunza na sifa nyingine nzuri. Kama haya ni ya kweli, ni rahisi kuyaona kwenye mitandao yake ya kijamii kwa sababu atakuwa anawashirikisha marafiki zake vitu vinavyohusiana na kile anachokipenda.

Hivyo katika mchakato wako w akupata mfanyakazi bora kwa biashara yako, mitandao ya kijamii inahusika sana. Ipitie na jua upande wa kijamii wa mtu upoje.

4. Angalia wafanyakazi ambao unao sasa.

Kama una ajiri mfanyakazi mpya na tayari una wafanyakazi wengine, basi kabla hujafikia hatua ya kumwajiri mtu angalia kwanza aina ya wafanyakazi ambao unao sasa, angalia utamaduni wa eneo lako la biashara kisha angalia je mfanyakazi huyu unayetaka kumwajiri ataendana na wafanyakazi wako wengine? Je ataendana na utamaduni wa eneo lako la biashara?

Lengo lako la kuajiri ni kuongeza nguvu na ufanisi kwenye biashara yako, sasa kama utaleta mtu ambaye haendani na wale ulionao tayari, utabomoa badala ya kujenga. Ielewe vizuri haiba ya mfanyakazi na kisha linganisha na wale ambao tayari unao.

5. Usihukumu kwa kuona.

Baadhi ya watu huhukumu wengine kwa mwonekano tu, kama na wewe utafanya hivi unaweza kukosa wafanyakazi wazuri sana au unaweza kuajiri wafanyakazi wabovu sana. Pamoja na kwamba mwonekano wa mtu utakupa picha fulani, jaribu kuiweka picha hiyo pembeni mpaka pale ambapo utakuwa umemsikiliza mtu, umemwuliza maswali na kujua hasa ni kitu gani anacho.

Jipe muda wa kumjua mtu vizuri kabla hujafanya maamuzi kwamba utamwajiri au utamwacha.

Kuajiri kwenye biashara sio zoezi rahisi, kama kweli unataka kupata wafanyakazi bora. Lakini pia sio zoezi ambalo linashindikana. Tumia mbinu hizi tano ulizojifunza hapa na utaweza kuajiri wafanyakazi bora na wanaoendana na biashara yako.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani.