Pamoja na ugumu wa maisha ambao wengi wanakuwa wanausema, lakini sehemu kubwa ya ugumu huu inasababishwa na mtu mwenyewe.
Kuna mizigo mingi ambayo umejibebesha na hii inafanya maisha yawe magumu zaidi na zaidi.
Leo kwa ufupi sana hapa tutaangalia mizigo uliyojibebesha ili uweze kuitua mara moja;
1. Kinyongo kwa watu waliokutendea ubaya. Huu ni mzigo mzito sana unaong’ang’ania kuubeba lakini hauna msaada wowote kwako. Haijalishi mtu alikutendea ubaya kiasi gani, hata kama alikuwa na njama za kukuua, achana naye, usiwe na kinyongo naye, msamehe na songa mbele. Kuwa na kinyongo kunakurudisha kwenye hali hiyo kila mara, na hutaweza kusonga mbele.
2. Kutaka kuwafurahisha watu, au kutawa kila mtu akukubali. Huu ni mzigo mzito sana kwa sababu hata ufanye nini, sio wote watafurahia na sio wote watakubali na kukusifia. Sasa kama wewe ndio unachotaka hiko, umejibebesha mzigo mzito.
3. Kufanya kazi kwa viwango vya kawaida. Chochote unachofanya, kama unafanya kwa viwango vya kawaida, unapoteza muda wako bure. Usijibebeshe mzigo huu mzito wa kufanya kawaida, hutaweza kwenda mbali. Kuwa tofauti na fanya kwa ubora, utaweza kufika mbali zaidi.
Usikubali kuendelea kubeba mizigo ambayo inakurudisha nyuma kwenye safari yako ya mafanikio. Hakikisha akili yako na njia yako ni safi ili kazi kubwa kwako iwe kufanyia kazi kile unachotaka na sio kufikiria waliokutendea ubaya au kufikiria ufanye nini ili watu wakukubali.
SOMA; Dakika 20 Kwa Siku Zinakutosha Kuwa Bora Duniani(WORLD CLASS)
TAMKO LANGU;
Japo nimechagua safari ya mafanikio, najua kuna mizigo ambayo nimejibebesha na hii imekuwa inanirudisha nyuma kwenye safari hii. Kuanzia leo naitua mizigo hii ili iwe rahisi kwangu kufanya kile ambacho ni muhimu zaidi kwangu.
NENO LA LEO.
When you are content to be simply yourself and don’t compare or compete, everybody will respect you.
Lao Tzu
Unapokuwa umeridhika na kuwa kama ulivyo wewe na ukaacha kujilinganisha au kushindana, kila mtu atakuheshimu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.