Kitabu 52 Weeks Of Sales Success ni kitabu ambacho kinaeleza mbinu muhimu z akuweza kufanikiwa kwenye kazi ya kuuza. Kitabu hiki ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu kwa sababu wote tunauza. Kila mtu kuna kitu anauza. Kama umeajiriwa unauza muda na utaalamu wako kwa yule aliyekuajiri. Kama unafanya biashara basi unauza bidhaa na huduma kwa wateja wako.

Kwa kuzijua mbinu bora za uuzaji utaweza kuuza kwa ubora na kupata faida kubwa na hivyo maisha yako kuwa bora.

Karibu tushirikishane mambo 20 muhimu niliyojifunza kwenye kitabu hiki 52 weeks of sales success.

1. Ianze siku yako kwa usahihi kwa kufanya yale majukumu ambayo ni muhimu na magumu. Kwa kuianza siku yako kwa kufanya majukumu magumu na ukayakamilisha mapema unakuwa na muda mzuri w akufanya mambo mengine uliyopanga. Ila kama utaacha mambo magumu na kusema utayafanya tu, siku inaweza kuisha na kushangaa unashindwa kufanya.

2. Wakati wote kuwa chanya. Watu ambao wako chanya wanatengeneza nguvu chanya ambayo inawavutia watu wengi zaidi kushirikiana naye, watu hawa wanaweza kuwa wateja, washirika na hata fursa mbalimbali. Watu hasi wanatengeneza nguvu hasi ambayo inawafukuza watu wasije karibu naye.

3. Jiwekee ahadi wewe mwenyewe ya kufanikiwa kwenye kile ambacho unauza, iwe bidhaa au huduma au muda au utaalamu. Jiwekee ahadi ya kuweka juhudi na maarifa mpaka pale ambapo utafikia kile unachotaka.

4. Mgodi wa hela upo hapo ulipo sasa. Mara nyingi ni rahisi kufikiri kwamba ukienda sehemu nyingine ndio kuna fursa zaidi ya kupata fedha. Lakini ukweli ni kwamba hiko unachopuza sasa, ndio kina hela nyingi sana. Unahitaji kujua jinsi ya kuuza kwa ubora, kuuza kwingi ili uweze kupata kipato kikubwa.

5. Kabla wateja hawajanunua kile unachouza, wanakununua wewe kwanza. Kabla wateja hawajaridhika na kile ambacho unawauzia, wanataka kuridhika na wewe kwanza. Tabia zako na mtazamo wako zina mchango mkubwa sana kwa wateja wako kukuamini na kuwa tayari kufanya biashara na wewe.

6. Kazi zako zinapokuwa nyingi, unapoanza kukutana na wateja wengi na unapopanga kuongeza unachofanya ili kuongeza kipato, unahitaji kuajiri msaidizi. Kama huna msaidizi, basi wewe ndio msaidizi. Na hapa utafanya kazi nyingi ambazo ungeweza kumpa mwingine afanye na wewe ukatumia muda wako kufanya yale ya muhimu zaidi.

7. Kumbuka; watu walioshindwa wanapenda kuona na wengine nao wanashindwa. Watu wenye mtizamo hasi wanapenda kuona na wanaowazunguka nao wana mtizamo hasi. Kitu muhimu sana unachotakiwa kufanya ni kuepuka sana watu ambao wana mtizamo hasi. Maana watakurudisha nyuma na hutaweza kufanikiwa. Wakimbie haraka watu hawa.

8. Ni lazima uweke malengo ya kila siku, kila wiki, kila mwezi na kila mwaka. Na weka vipaumbele vyako ili kuweza kutimiza malengo hayo. Bila ya malengo ni vigumu sana kwako kufanya mambo makubwa na kufikia mafanikio makubwa. Na kama ikitokea hujafikia lengo, lifanyie tena kazi, usikate tamaa.

9. Jifunze na kuwa tayari kugatua/kutoa majukumu yako kwa wengine. Kama kuna kitu unafanya sasa na kuna mtu mwingine anaweza kukifanya kwa gharama ya chini, mpatie mtu huyo. Hii inakupatia wewe muda wa kutosha kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi. Kitu kinachowazuia wengi kushindwa kugatua majukumu ni kufikiri kwamba hakuna mtu anayeweza kufanya vizuri kama wao, hapo ni kujidanganya. Vitu vingi unavyofanya, kuna wengine wanaweza kufanya pia.

10. Hakikisha unajua vizuri kile ambacho unakiuza, kama hukijui unapoteza muda wako bure. Jua vizuri, yaani jua nje ndani, hakikisha unajua kila kitu kinachohusiana nacho. Jua changamoto ambazo mteja anaweza kukutana nazo kwa kutumia hiko unachouza. Kama kuna uwezekano, wewe inabidi uwe mtumiaji wa kwanza kabisa wa kile ambacho unauza. Unahitaji kuamini sana kile unachouza kama kweli unataka kufanikiwa.

11. Chagua kuuza kitu ambacho unakipenda na kukifurahia. Iwe ni kwenye kazi au biashara, ni muhimu sana upende kile ambacho unafanya. Inawezekana fedha ndio msukumo wa kwanza lakini kama kitu hukipendi, hata kama utapata fedha nyingi kiasi gani, bado utajisikia hujakamilika ndani yako.

12. Wajue vizuri wateja wako. Ili uweze kuuza vizuri ni lazima umjue yule ambaye unamuuzia. Jua anapendelea nini, jua tabia zake katika manunuzi, jua ni changamoto gani anazopitia na jua ni vitu gani anapendelea.

13. Watu ni muhimu kuliko faida. Wekeza kwa watu zaidi na kwa uwekezaji huu faida itakuja moja kwa moja. Ni lazima watu wako waweze kutoa huduma bora sana kwa wateja. Jenga biashara yako kwenye misingi ya watu na itakuwa bora sana.

14. Kama unaona tatizo kwenye kazi yako au biashara yako, jua kwamba wengine nao wana tatizo kama hilo. Hivyo badala ya kulalamikia tatizo hilo, litafutie suluhisho halafu wauzie wengine pia suluhisho hilo. Au unaweza kuwa mshauri kwenye eneo hilo.

15. Kujitangaza ni muhimu sana. Na kujitangaza sio mara moja, ni zoezi la kila siku na kila mara. Popote unapokuwa hakikisha watu wanajua kwamba wewe ni nani na unafanya nini. Kadiri watu wengi wanavyojua unachofanya, ndivyo wataweza kuwaambia wengine kuhusu wewe na unachofanya.

16. Sasa hivi kuna njia nyingi sana za kuweza kujitangaza na kwa bei nafuu. Kwa kazi au biashara yoyote ambayo unafanya, hakikisha unatumia njia hizi kujitangaza.

A) hakikisha unakuwa na business card ambazo zinaelezea wewe ni nani na unafanya nini na pia kuwe na mawasiliano yako.

B) hakikisha unakuwa na taarifa zako kwenye mtandao wa intaneti, kwa kuwa na tovuti au blog ambayo inaelezea kile unachofanya. Watu wanapokuwa na shida wanatafuta suluhisho kupitia mtandao, hivyo taarifa zako zikiwa kwenye mtandao ni rahisi kukutafuta.

C) Tumia nafasi za kijamii, vyombo vya habari na kila fursa kuhakikisha watu wengi zaidi wanajua kuhusu wewe.

17. Mafanikio ya mteja wako ndio mafanikio yako. huwezi kufanikiwa wewe kama mteja wako hajafanikiwa, hivyo chochote unachofanya, fikiria mteja wako anafanikiwaje. Na akishafanikiwa na wewe ni lazima utafanikiwa. Mfikirie zaidi mteja wako na matatizo yako yatatatulika bila ya shida.

18. Watumie wateja ulionao sasa kukuletea wateja wengi zaidi. Kama umewaridhisha wateja ulionao sasa, basi wanasubiri kwa hamu sana kujua wanawezaje kulipa fadhila. Watumie wateja hawa kuwaambia wengine kuhusu biashara yako ili nao waweze kuja kununua kwako pia. Mteja anapomwambia mtu wake wa karibu, anaamini zaidi kuliko kusikia kwenye matangazo.

19. Unahitaji kuwa na mtu wa kukusimamia ili uweze kufikia malengo na mipango unayojiwekea. Mtu huyu ana mentor, au kocha au mtu wa karibu ambaye mnafanya naye kitu pamoja. Kwa kuwa na mtu wa kukuliza pale ambapo unakosea au wa kukutia moyo pale ambapo unaelekea kukata tamaa inakuwa rahisi kwako kufikia malengo yako.

20. Unapotafuta mtu wa kushirikiana naye, kuwa makini sana, kuwa makini kuliko hata unavyokuwa makini kwenye kuchagua mke au mume. Mtu unayeshirikiana naye kwenye biashara ana mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yako. ukichukua mtu ni mtu tu atakuchelewesha sana wewe kuweza kufikia malengo yako. chukua mtu ambaye ana kiu kweli ya mafanikio na ana mtizamo chanya. Pia awe mtu wa kujituma na anayechukua hatua badala ya kulalamika.

Mafanikio yako kwenye jambo lolote yanategemea umahiri wako kwenye kuuza, kama unauza kitu ambacho unakiamini, unakipenda na unamjua unayemuuzia, basi juhudi zako zitakuwezesha kupata chochote ambacho unakitaka.