Habari za Jumapili mpenzi msomaji wa Amka Mtanzania. Ni siku nyingine tunakutana tena kuendelea na mfululizo wa makala zetu ambapo tumekuwa tukikumbushana na kujulishana mambo mbalimbali ili kuzidi kufanya duniani kuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi. Natumaini kuwa wewe ambaye umekuwa ukinisoma kila Jumapili mahali hapa kipo kitu ambacho unakipata kila unaposoma makala hizi.
Watu wengi wamekuwa ni watu wa kuhitaji majibu na mafanikio ya haraka , mtu anataka anapofanya kitu leo basi kesho akiamka au baada ya siku chache tu kimlipe vizuri, kwa mfano mtu anaweza kuanzisha biashara au shughuli fulani leo na kutegemea ndani ya siku chache tu awe ameanza kupata faida kubwa sana. Si vibaya kutamani kupata faida kubwa kutokana na kile unafanya lakini ni vyema pia kama hautakuwa na haraka sana na ukapata muda na nafasi ya kuandaa msingi mzuri na kuimarisha msingi wa biashara au shughuli yako ili ikianza kukulipa iwe ni kitu endelevu ambacho kimepangiliwa vyema.

 
Wanafunzi wakiwa vyuoni wengi wanafikiri kuwa akisoma na kuhitimu masomo yake basi akitoka tu kule atapata kazi nzuri na pengine kupata cheo na nafasi za juu na kuweza kutengeneza pesa nyingi na pengine kuweza kuishi maisha ya ndoto zake, na wengi kwa kuondoka na fikra hizo hata wanapokuja kwenye uhalisia na kukuta mambo yapo kinyume, mfano mtu anapoomba kazi na kupata anajikuta analipwa mshahara mdogo sana tofauti na alivyokuwa akitegemea iwe, wengi huwaumiza sana na wengine hujikuta wanagoma hata kufanya kazi hizo wakisubiri kupata zile nafasi kubwa zenye mishahara ya juu, wanatamani jambo jema hilo lakini ni vyema wakielewa kuwa ili uweze kufika kule juu ni lazima uanzie mahali fulani , hauwezi kujikuta upo juu tu, hata ndege kabla haijapaa angani inakuwa chini kwanza, inaanzia safari yake chini ndipo inafika kule juu angani.
SOMA; Sababu 7 Zinazokufanya Upoteze Hamasa Kwa Kile Unachokifanya.
Hivyo ni vyema kama wengi wetu katika maisha haya iwe ni kwenye kazi au biashara ni vizuri kama tutatambua kuwa katika maisha haya inawezekana kufanikiwa na kufikia pale tunatamani kufika lakini ni lazima tuwe tayari kuanza chini, ni lazima uwe tayari kujenga msingi na si msingi bora msingi, unatakiwa uwe msingi imara, Mfano ikiwa nataka kuwa meneja wa fedha mzuri , ni vyema kama utakaa chini na kutafuta wale watu unaona wanafanya vizuri kwenye maeneo hayo na ukiweza kupata nafasi ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwao ni vyema, uwaulize maswali, wahoji uweze kujua walianzaje, wamekutana na changamoto gani njiani, walizikabili vipi na uwaombe hata ushauri kama wakiwa tayari ili uweze kukufaa wewe unapoanza safari hiyo , uweze kujua uanzie wapi, uanzeje na katika kipindi hicho ni vyema kama utakwepa njia za mkato, maana njia za mkato zinaweza kuwa zinapendeza machoni kwa kuleta matokeo ya haraka lakini haziwezi kufaa wakati wote, zinaweza kukufanya ukaishia pabaya wakati mwingine.
Usiogope kuanza chini kabisa, usiogope kuanza na sifuri, hata unaowatamani walianza mahali fulani ndio maana unaona leo wapo walipo, huenda walianguka lakini kuanguka kwao hakukuwafanya wakate tama ya kusonga mbele. Hivyo jitie moyo, pengine umekata tama kuendelea kufanya hicho unafanya kwa kuwa hauoni matunda uliyoyategemea, ndugu usikate tamaa, kaa chini angalia ulianzaje, chunguza angalia wapi unaanguka na kwa nini unaanguka, jifunze sana, jifunze kwa waliofanikiwa katika hilo , usiogope kuuliza na hata kutafuta maarifa sehemu yoyote unayoona inafaa. Usiogope kushindwa , maana unapojaribu na kushindwa lipo unalokuwa umejifunza, hata katika kaunguka kuna darasa, yapo mengi unajifunza na unapoinuka tena unaikuna na nguvu mpya na kuweza kufika kule unaenda.
SOMA; WAHITIMU; Vumilia Mateso Ya Muda Mfupi Ili Uweze Kupata Furaha Idumuyo.(Mambo Manne Yatakayokusaidia Kufikia Mafanikio Makubwa)
Pengine hauoni mwanga leo, pengine hauoni faida ya hicho unafanya leo lakini nikuambie hata mkulima akilima havuni siku hiyo hiyo kuna hatua lazima zipitiwe ili mtu aweze kuvuna, usitake njia za mkato , usitake mavuno ya haraka haraka, fuata hatua zote na uwe na uhakika kuwa ili mradi unafanya kila kitu kwa usahihi basi ipo siku na wakati utayaona majibu chanya yenye faida.
Nashukuru sana kwa kutoa muda wako kusoma makala hii. Tukutane tena wiki ijayo mahali hapa tukijaaliwa uzima na Muumba wetu.
Makala imeandikwa na Beatrice Mwaijengo
+255 755 350 772