Simba na yanga wakiwa na mchezo wa mpira, kuna majibu ya ya aina tatu yanaweza kutokea kwa timu yoyote kati ya hizo. Kushinda, kushindwa au kutoka suluhu.
Ikatokea simba wameshinda, watu wanakuwa na sababu z akutosha ni kwa nini wameshinda, na zitakuwa sababu nzuri sana. Na hata ikatokea simba wameshindwa, watu watakuwa na sababu kwa nini wameshindwa, na zitakuwa sababu za ukweli sana. Timu ile ile kwenye mchezo ule ule lakini kushinda au kushindwa kote watu wanakuwa na sababu.
Hivyo ndivyo ilivyo kwenye maisha yako pia.
Unapochagua kufanya jambo kubwa, jambo ambalo wengine hawajawahi kufanya, utakaposhinda kuna wengi watakuwa na sababu nzuri kwa nini umeshindwa. Tulijua, hiki kilimsaidia na mengine mengi. Lakini pia kwenye jambo hilo hilo ikatokea umeshindwa, watu watakuwa na sababu kwa nini umeshindwa. Tulimwambia, asingeweza hili na mengine mengi.
Aa ufanye nini?
Fanya kile unachotaka kufanya, pigania kile unachoamini, na ikitokea umeshindwa na watu wanakusema, jua hata ungeshinda bado wangesema. Pia ikitokea umeshinda na watu wanakupongeza, jua kama ungeshindwa wangekusema.
Chochote unachofanya, fanya kwa sababu ndio unachoamini na ndio hasa unachotaka, usifanye kwa kuangalia watu wanasema nini. Watakupotosha na utashindwa kuwa na maisha bora kwako.
SOMA; Mambo Matano Yatakayokuwezesha Kushirikiana Vizuri Na Watu Kwenye Kazi Na Kufikia Mafanikio Makubwa.
TAMKO LANGU;
Najua ya kwamba watu tayari wanazo sababu za mimi kushinda au kushindwa. Lakini mimi ndio mwamuzi mkuu wa maisha yangu. Iwe nitashinda au nitashindwa, nitaendelea na safari yangu ya kupigania kile ninachotaka. Maneno ya watu hayana nafasi kubwa kwangu, najua nini ninataka na nitakipigania mpaka nikipate.
NENO LA LEO.
People will always have an opinion of you. Don’t let people’s opinion build your future instead let their opinions motivate your success…
– Vikas Runwal
Watu mara zote watakuwa na maoni juu yako. usikubali maoni yao ndio yajenge maisha yako, badala yake yafanye maoni yao kukuhamasisha ili ufikie mafanikio zaidi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.