Kitabu SPEAK TO WIN kimeandikwa na mwandishi maarufu sana wa vitabu anayejulikana kama Brian Tracy. Brian ameandika vitabu vingi na pia amekuwa akitoa mafunzo mbalimbali ya biashara na mafanikio.

Katika kitabu hiki Brian anatushirikisha mbinu za kuweza kuongea vizuri mbele ya watu na kuweza kuwashawishi watu kuchukua hatua ambayo unataka wachukue?

Kila mmoja wetu kuna wakati atahitaji kuwashawishi watu wengine, au hata kutoa taarifa. Inaweza kuwa mbele ya watu wengi au hata mbele ya watu wachache. Inawezekana pia ikawa unaongea kuhusu kazi, biashara au hata kwenye sherehe.

Kuna mbinu ambazo ukizijua utaweza kuongea vizuri mbele za watu, na watu wakawa na shauku kubwa ya kukusikiliza badala ya kusinzia.

Hapa nimekuandalia mambo 20 muhimu sana niliyojifunza kupitia kitabu hiki SPEAK TO WIN.

1. Rasilimali kubwa sana unayomiliki ni akili yako. uwezo wako wa kufikiri vyema na ukaweza kuziwasilisha fikra zako vizuri mbele ya watu wengine kutakuwezesha wewe kupata chochote ambacho unakitaka. Wote tunajua ya kwamba chochote unachotaka utakipata kutoka kwa wengine. Jinsi unavyoweza kuwashawishi vizuri wengine, ndivyo watakavyokuwa tayari kukupa kile unachotaka. Hivyo kuongea vizuri kunaanza na kufikiri vizuri.

2. Akili yako ni kama msuli wa mwili, kadiri unavyoitumia ndivyo inavyokua zaidi. Hivyo unavyoitumia akili yako kujiandaa kabla ya kuzungumza mbele ya wengine, ndivyo akili yako itakuwezesha kufanya mazungumzo mazuri sana. Fikiria kwa kina na fanya maandalizi ya kutosha kabla hujazungumza mbele ya watu wengine. Hata kama hujawahi kufanya hivyo, fanya maandalizi na akili yako itakuwezesha kufanya vizuri.

3. Ili kuwa mzungumzaji mzuri unahitaji kuwa na vitu vinne muhimu.

Kwanza unahitaji kuwa na shauku kubwa ya kutaka kuzungumza vizuri. Kama shauku yako ni kubwa na unataka kuwa vizuri kwenye uzungumzaji, hakuna kinachoweza kukuzuia.

Pili unahitaji kufanya maamuzi kwamba unataka kuwa mzungumzaji mzuri. Unafanya maamuzi kwamba kila siku unakwenda kuchukua hatua ili kuwa mzungumzaji bora zaidi.

Tatu unahitaji kuwa na nidhamu ya kuweza kujiandaa na kutoa mazungumzo yako mbele ya watu. Unahitaji kuwa na nidhamu kwa sababu sio kazi ndogo.

Nne unahitaji kujitoa na kutokukata tamaa hata kama mwanzoni hutafanya vizuri.

4. Mafanikio ya mtu yeyote yanatokana na uwezo wake wa kuwashawishi watu wengine. Historia yote ya dunia inaonesha wale waliofanikiwa sana kwenye uongozi na hata biashara, walikuwa na wamekuwa ni watu wenye ushawishi mkubwa. Na wamekuwa wakionesha ushawishi huo kupitia mazungumzo wanayotoa kwa wale wanaowazunguka.

5. Kuna viungo vitatu muhimu sana vya ushawishi.

Kiungo cha kwanza ni mantiki(logic) ni lazima kile unachozungumza mbele ya watu kiwe na mantiki kwao.

Kiungo cha pili na maadili(ethic) ni muhimu sana unachowaambia watu kiwe kinaendana na maadili yao ndio wataweza kushawishika.

Na kiungo cha tatu ni hisia(emotion) kama unataka watu wahamasike na kuchukua hatua mara moja, hakikisha unachozungumza kinagusa hisia zao.

6. Njia pekee na ya uhakika kujifunza kuongea vizuri mbele za watu ni kuongea, kuongea, kuongea na kuongea tena. Kadiri unavyoongea zaidi na zaidi ndivyo unavyopata mbinu nzuri za kuweza kuongea vizuri zaidi.

7. Watu watasahau kile ambacho umeongea, ila hawatasahau jinsi ambavyo umeongea. Hivyo ni muhimu sana kuyaandaa mazungumzo yako vizuri kiasi kwamba watu wataendelea kukumbuka jinsi ulivyowapatia mazungumzo hayo. Na kwa njia hii watu watakusikiliza kwa makini sana na hivyo kuweza kushawishika kuchukua hatua.

8. Kabla ya kufanya mazungumzo kwenye nafasi yoyote au kwa jambo lolote unalopewa nafasi ya kuzungumza, ni vyema ukafanya utafiti wa kutosha, kujua vizuri kile unachokwenda kuzungumza ili unaposimama mbele ya watu ujiamini na wao waweze kukuamini, unapofanya utafiti na kujua mengi utajiamini sana.

9. Maandalizi yako kabla ya kuzungumza yanachangia asilimia 90 ya mafanikio yako kwenye kile unachokwenda kuzungumza. Dakika chache tu baada ya kuanza kuongea, wale wanaokusikiliza wanakuwa wameshajua kama kweli umejiandaa vizuri na unajua kile unachoongea au unaongea tu kwa sababu umepewa nafasi ya kuongea. Jiandae vizuri sana kabla hujatoa mazungumzo yako mbele ya wengine.

10. Kuongea mbele ya watu ni kitu ambacho watu wengi sana wanahofia. Watu wengi wapo radhi kuzikwa hai lakini sio kuongea mbele ya kundi kubwa la watu. Unaweza kuiondoa hofu hii kwa kuanza kuzungumza na watu wachache na kisha kuongeza wingi. Baada ya muda utajikuta unazungumza na kundi kubwa la watu bila ya kuwa na hofu.

11. Unaposimama mbele ya kundi kubwa la watu kwa ajili ya kuzungumza, simama kwa kujiamini, simama wima huku ukiwatazama wale ambao unakwenda kuongea nao. Na njia bora ni kumtazama mtu mmoja kwenye macho yake na kuchukulia kama unazungumza na mtu huyu mmoja tu. Kwa njia hii hofu ya kuongea mbele ya watu itaisha na utaongea kwa kujiamini.

12. Ili watu wakusikilize kwa kile unachoongea ni lazima wakupende na kukubali kwanza. Na ili watu wa kukubali na kukupenda, unahitaji kuwa na vitu viwili, kuwa halisi na pia unahitaji kuwa mnyenyekevu. Unakuwa halisi kwa kuwa muwazi na kusema ukweli. Ni lazima watu wajisikie salama kwako ndio waweze kuchukua hatua kwenye kile unachowashawishi, hivyo kuwa mwaminifu na ongea na watu katika hali ya unyenyekevu na kusikiliza.

13. Dini moja ambayo watu wote wanakubaliana nayo duniani ni MATUMAINI. Unapozungumza vizuri unawapa watu matumaini. Na watu wanapopata matumaini wanakuwa tayari kuchukua hatua. Hivyo ili uweze kuwashawishi watu, wape matumaini, watashawishika na kuhamasika kuchukua hatua.

14. Njia nzuri ya kuhakikisha watu wanakufuatilia kwa kile unachozungumza ni kuuliza maswali mara kwa mara. Binadamu tumezoeshwa kwamba unapoulizwa swali ni lazima ujibu, hivyo unapouliza maswali hata kama mtu hatajibu wazi wazi lakini atajipatia jibu ndani ya nafsi yake. Hivyo unapouliza maswali, watu wanafikiri juu ya kile unachozungumza.

15. Kuna aina nne za mikutano ya kibiashara, na aina hizi zina ajenda tofauti.

Aina ya kwanza ni mikutano ya kutatua matatizo au changamoto. Hapa kunakuwa na tatizo ambalo linatafutiwa ufumbuzi.

Aina ya pili ni mkutano wa kutoa taarifa, hapa kunakuwa na taarifa muhimu ambayo watu wanatakiwa kujua.

Aina ya tatu ni mkutano wa kutoa bidhaa mpya, mkutano huu unakuwa na lengo la kutambulisha bidhaa au huduma mpya.

Na mkutano wa aina ya nne ni mkutano wa kujenga timu, hapa watu mbalimbali wanaohusika na biashara wanakutana pamoja kujadili juu ya kile wanachofanya. Unapopewa nafasi ya kuzungumza ni muhimu sana ujue ni aina gani ya mkutano unaokwenda kuzungumza.

16. Unaposhiriki kwenye mkutano wowote, hata kama wewe sio mzungumzaji mkuu, uliza maswali, changia mawazo na fanya chochote ambacho kitakutofautisha na wengine. Na unapofanya hivi hakikisha umejiandaa vyema. Kwa njia hii utajifunza sana na pia utapata fursa nyingi zaidi kuliko wale ambao wamekaa kimya tu.

17. Kuna vitu viwili vinavyowasukuma watu kufanya maamuzi ya kununua kitu chochote. Vitu hivi ni hofu na tamaa. Watu wanapokuwa na hofu kwamba wanakosa kitu fulani wanafanya maamuzi ya kununua haraka sana. Na pia watu wanapokuwa wanatamani sana kitu wanafanya maamuzi ya kununua haraka. Mbinu hii imekuwa ikitumika na wafanyabiashara kuwashawishi wateja kununua zaidi.

18. Unapotaka kushawishi watu wakubaliane na kitu ambacho hawakubaliani nacho, usianze kwa kuwaambia kitu hiko, bali anza kwa kuwaambia kitu ambacho unajua wanakubaliana nacho, wakishakubali sasa tumia kile wanachokubaliana nacho kuunganisha na kile ambacho hawakubaliani nacho, kwa njia hii watakubaliana na wewe.

19. Unapozungumza mbele ya watu, zungumza kwa sauti kubwa ambayo watu wote wanasikia na pia zungumza kwa kasi ndogo. Unapozungumza taratibu(kwa kasi ndogo) unachukua umiliki mkubwa wa mazungumzo hayo na pia unawapa watu nafasi ya kutafakari vizuri kile unachowaambia. Lakini ukizungumza kwa haraka, unawaacha watu na hivyo kushindwa kuwashawishi au kufikisha ujumbe wako.

20. Kila mtu yupo kwenye biashara ya kuuza, swali ni je wewe unauza nini na je unauza kwa uzuri kiasi gani? Kama unafikiri wewe sio muuzaji unakosea sana, wewe ni muuzaji na kuna kitu ambacho unauza kwa wengine. Inawezekana ni bidhaa au huduma, inawezekana ni muda wako, inawezekana ni ujuzi wako, inawezekana ni taarifa ulizonazo. Katika njia zote, kadiri unavyoweza kuongea vizuri na kumshawishi yule unayemuuzia, ndivyo utakavyokuwa na kipato kizuri.

Anza sasa kuchukua hatua ya kujiandaa kuwa mzungumzaji bora. Na popote unapopata nafasi ya kuongea na mtu mmoja, kikundi cha watu au hata kadamnasi kubwa, hakikisha unatoa mazungumzo ambayo yatamfanya mtu ashawishike na awe na hamasa ya kuchukua hatua mara moja.

Hata kama sasa hivi huwezi kuzungumza mbele ya watu wachache, anza taratibu na kama hutakata tamaa utakuwa mzungumzaji mzuri sana.

Nakutakia kila la kheri.

Rafiki na kocha wako,

Makirita Amani.