Karibu mwanafalsafa mwenzangu katika makala zetu hizi za falsafa mpya ya maisha. Kupitia kipengele hiki cha falsafa mpya ya maisha, tunatengeneza ukweli ambao tunaenda nao katika safari yetu ya kufikia mafanikio makubwa.

Kama ilivyo kwa kila mmoja wetu, tunataka tuwe na maisha bora zaidi, tunataka tuwe na mchango mkubwa kwa wanaotuzunguka na tunataka kuwa muhimu kwetu na kwa wale wanaotuzunguka. Kujijengea falsafa hii kutatuwezesha kuwa na maisha bora sana.

Pia kupitia falsafa hii tunajijengea uhuru mkubwa sana wa maisha yetu. Kwa kuishi maisha ya mazoea, maisha ambayo kila mtu amezoa kuishi, ni gereza kubwa sana ambalo linatuzuia kuwa bora zaidi. Lakini kupitia falsafa hii tunavunja gereza hili na kuanza kuona mwanga wa kuwa na maisha ambayo tunayafurahia.

Leo kupitia falsafa hii mpya ya maisha tunaangalia jambo moja ambalo lipo wazi sana, lakini wengi tumekuwa hatulipi uzito. Tumekuwa tunalipuuza na hii imekuwa inatugharimu sana baadae. Leo kupitia makala hii tutakumbushana jambo hili muhimu, ili tuanze kulifanyia kazi na maisha yetu yaendelee kuwa bora.

Kuna gharama ya kulipa.

Tangu kuanza kwa dunia, na mpaka tulipo sasa, na hata miaka mingi ijayo, kuna gharama ya kulipa kwa kila jambo. Sisi tunataka kuwa na maisha bora na ya mafanikio, lakini maisha haya hayaji tu kwa sababu umeyataka, bali kuna gharama ambayo ni lazima uilipe ili uweze kupata maisha hayo.

Katika kila jambo kwenye maisha yako, kuna gharama ambayo ni lazima uilipe, hata ungefanya nini, huwezi kuacha kuilipa gharama hiyo.

Na maisha yako hapo yalipo sasa, yapo hivyo yalivyo kutokana na mambo haya mawili;

Jambo la kwanza ni huenda umelipa gharama na ndio maana sasa hivi unaishi maisha ambayo unayafurahia, maisha ambayo kuna wengine wengi ambao wanatamani wangekuwa nayo lakini hawawezi.

Jambo la pili huenda ulikwepa kulipa gharama na sasa unaishi maisha ambayo unajutia, maisha ambayo sio mazuri na unatamani kama ingewezekana ubadili maisha hayo.

Kwenye kile jambo kuna gharama ya kulipa, na ndio maana katika kila aina ya maisha, kuna watu ambao wamefanikiwa na kuna ambao hawajafanikiwa. Tofauti hii inaletwa na mambo mengi, na mojawapo muhimu ni kuwa tayari kulipa gharama au kutokulipa gharama.

Huwezi kukimbia kulipa gharama.

Unakumbuka kwenye moja ya makala hizi za falsafa mpya ya maisha, tumewahi kujifunza kwamba huwezi kuidanganya dunia, yaani fanya ufanyavyo, kuna mahali dunia itakushika tu. Huwezi kamwe kuidanganya dunia, ina akili kukushinda wewe. Imekuwepo hapa muda mrefu kuliko wewe na yote unayoyafanya kuna wengi walishajaribu kuyafanya.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa gharama, huwezi kukwepa kulipa gharama, lazima utalipa tu. Dunia imejipanga vyema sana kuhakikisha kila mtu analipa gharama, isingekuwa hivi basi sisi tusingeikuta dunia, waliotutangulia wangeshaimaliza zamani sana.

Na dunia kuhakikisha kwamba wewe unalipa gharama, inakupa machaguo, uchague kulipa sasa au uchague kulipa baadae. Unaweza kuona hulipi gharama sasa, ukawacheka wale ambao wanalipa, ukajiona wewe ni mjanja, lakini dunia inakusubiri, utakuja kulipa baadae, dunia haina haraka na wewe, inajua utakuja tu kulipa. Ni sawa na kuchukua mkopo benki, wanajihakikishia kwamba utawalipa mkopo wao.

Mifano ya kulipa sasa au kulipa baadaye.

Kama labda hatujaelewana vyema kwenye kulipa sasa au kulipa baadae, wacha tuangalie mifano hii ambayo itatupa mwanga zaidi;

1. Labda huna muda wa kupika chakula kizuri kwa afya yako sasa, na hivyo unalazimika kula vyakula vya haraka, (fast food). Lakini nini kinatokea baada ya muda? Utapata uzito uliozidi kiasi, na hivyo kuanz akupata matatizo ya kiafya, na hivyo ule muda na gharama ulizoepuka sasa kupika chakula kizuri, utaulipa kwa kufanya mazoezi mazito na kujitibu ili uweze kurudi kwenye afya yako. na ukigoma kulipa hivyo ni nini kinafuata? Najua unajua benki inafanya nini pale unaposhindwa kulipa deni, inakufilisi. Na hiki ndio kitakachotokea kwenye maisha yako, yatafilisiwa kabisa, yaani utakufa kabla hata ya muda wako.

2. Mfano mwingine upo kwenye kazi na unaona wenzako wanakwenda kuongeza masomo, wewe unawashangaa, unaona wanahangaika nini, kwa nini wajitese wakati tayari wanayo ajira ya uhakika. Wenzako wanarudi masomoni, wakiwa na ujuzi zaidi na hivyo kufanya kazi zao kwa ubora zaidi na hatimaye kupata fursa za juu zaidi huku wakikuacha wewe chini. Wao walichagua kulipa gharama ya kusoma mapema, labda ilikuwa vigumu sana kufanya hivyo, na baada ya kumaliza wanafurahia matunda ya kile walichofanya. Wewe uligoma kulipa gharama na sasa unailipa kwenye maisha yako yote.

3. Mfano mwingine umeingia kwenye biashara, na unafikiria kupata faida tu, kwa namna yoyote ile. Na hivyo kukwepa taratibu zinazohitajika kwenye biashara, kuwalaghai wateja na mengine mengi. Ni kweli unaopata faida kubwa na unawashangaa wale ambao wanajifanya kuendesha biashara zao kwa utaratibu na kwenda vizuri na wateja japo wanapata faida kidogo. Lakini wewe huchukui muda kwenye njia hiyo uliyochagua, utajikuta umeingia kwenye matatizo ya kisheria, wateja nao wanakukimbia na biashara inakufa kabisa. Hapa ulichagua kutokulipa gharama ya kujenga biashara inayoaminika na hatimaye unalipa gharama kubwa zaidi ya kuondoka kwenye biashara kabisa.

4. Unashindwa kujinyima sasa hivi, ili sehemu kubwa ya kipato chako uweke akiba na kuwekeza kwenye maeneo ambayo yatakuzalishia baadae. Badala yake unatumia kipato chote unachopata, na baadae unajikuta hujawekeza chochote na uwezo wa kutengeneza kipato umepungua au kuisha kabisa. Umeshindwa kulipa gharama kwa sasa, na hivyo maisha yako yote ya baadae unayatumia kulipa gharama.

Ukichagua kulipa gharama baadae, utalipa na riba.

Yaani kama benki zinavyofanya kazi, ndivyo dunia nayo inafanya kazi. Ukichukua mkopo benki kwa muda mfupi, labda miezi sita watakupa kwa riba ndogo na hivyo unaweza kukazana na kulipa kisha ukawa umemalizana nao.

Ila unapochukua mkopo wa muda mrefu, labda miaka mitano au kumi, na riba utakayolipa ni kubwa pia.

Hivi pia ndivyo ilivyo kwa gharama tunayotakiwa kulipa kwenye maisha ili tuwe na maisha bora na yenye mafanikio. Ukiamua kulipa gharama hiyo sasa, kwa kufanya kile ambacho ni muhimu kufanya ili uwe na maisha bora utalipa kwa urahisi sana, sio kwa urahisi kwamba itakuwa rahisi, ila ni rahisi ukilinganisha na unapokuja kulipa baadae.

Unapoacha kulipa sasa, maana yake umeamua utalipa baadae, unalipa gharama kubwa sana. Yaani unaweza kutumia maisha yako yote yaliyobaki kulipa gharama hii, na hivyo kuwa na maisha magumu sana.

Ni sawa na kushindwa kujenga afya yako sasa, na baadae ukatumia muda wako wote kujitibu kwa afya mbovu. Au kushindwa kuweka akiba na kuwekeza sasa wakati bado una nguvu, baadae ukaja kuishi maisha ya kimasikini mpaka unapokufa, na hapo huna tena nguvu kama sasa.

Anza kulipa gharama sasa, hujachelewa.

Kama unasoma hapa, kwanza nikuhakikishie jambo moja, bado hujachelewa kulipa gharama, unaweza kuanza kuilipa gharama unayotakiwa kulipa sasa.

Kaa chini na angalia kutokana na maisha unayoyataka wewe ni gharama gani unahitaji kulipa.

Je unahitaji kuongeza elimu zaidi?

Je unahitaji kujenga mtandao mkubwa zaidi?

Je unahitaji kufuata taratibu zilizowekwa?

Je unahitaji kujali afya yako zaidi?

Andika ni gharama zipi unazotakiwa kulipa ili uwe na yale maisha ya ndoto yako.

Ukishajua ni gharama zipi unazotakiwa kulipa, anza kulipa leo hii, wala usichelewe. Kwa sababu miaka kumi ijayo, ukija kusoma tena hapa, utajilaumu sana kwa kutokuchukua hatua haraka.

Je ni elimu unahitaji kuongeza, anza kuangalia unaipataje. Je ni juhudi unahitaji kuweka kwenye kazi yako? anza kufikiri na kufanyia kazi.

Je ni akiba unahitaji kuanza kuweka, ili uwekeze na baadae upate uhuru wa kifedha? Anza sasa kuweka pembeni kila sehemu ya mapato yako.

Kadiri unavyokubali kulipa gharama zako mapema, ndivyo utakavyolipa kwa riba kidogo na ndivyo utakavyokuwa na maisha bora.

Muhimu sana kukumbuka.

Ni lazima utalipa gharama, hata kama utaona umepata njia ya shotikati kiasi gani, gharama zinakusubiri mbele uje ulipe, usipoteze muda wako kukwepa kulipa, ni bora ukalipa sasa ili baadae ufurahie matunda ya kulipa gharama zako mapema.

Mfano wa kuchekesha kidogo.

Nimewahi kusoma mahali kwamba kuna mtu alipita kwenye mgahawa na akakuta tangazo limeandikwa KULA BURE, GHARAMA ATALIPA MJUKUU WAKO. Mtu huyu alifurahi sana, akaona hapa amepata, akaingia kwenye mgahawa na akaagiza vyakula vizuri. Alipomaliza kula, mhudumu akamletea gharama, jamaa akasimama kwa hasira, mbona tangazo linasema tunakula bure na gharama atalipa mjukuu wangu? Si msubiri aje awalipe? Mhudumu akamjibu kwa unyenyekevu sana, hii sio gharama yako, bali ni ya babu yako…. jamaa kuangalia kweli gharama iliyoandikwa pale ni tofauti na alichotumia, na ilimbidi alipe ili asije kuaibika.

Kila unapojiona umekwepa kulipa gharama, kabla hujafurahia, jiulize swali hili makini sana. Nitakuja kuilipa lini hii? Na nitailipa kwa riba kiasi gani?

Fanyia kazi kile ambacho umejifunza hapa, muda ndio huu, kama ni gharama anza kulipa sasa.

Rafiki na kocha wako,

Makirita Amani.