Watoto wanajua sana, pengine vizuri zaidi kuliko hata wewe.
Kudhibitisha hili muulize mtoto yeyote mwenye umri katia ya miaka mitano mpaka kumi swali hili; ukiwa mkubwa unataka kuwa nani?
Niambie kama utasikia jibu kama hili;
Nikiwa mkubwa nataka niwe makamu wa raisi…
Nikiwa mkubwa nataka niwe napanga mafaili kwenye ofisi….
Nikiwa mkubwa nataka niwe naokota makopo…
Je umepeta jibu ambalo linaendana na hayo?
Jibu ni hapana, majibu utakayopata ni nataka niwe raisi, niwe rubani, niwe daktari, niwe mwalimu na mengine kama hayo.
Hivyo watoto wanajua, ya kwamba kwenye maisha unatakiwa kupata kile kilicho bora. Makamu wa raisi ni nafasi kubwa, lakini kuna bora zaidi, raisi, hivyo mtoto yeyote atataka kuwa rahisi.
Sasa cha kushangaza hapa ni kwamba kwa nini wewe umekataa kupigania kile ambacho unajua ni bora zaidi kwako? Kwa nini umekubali kuridhika na pale ambapo ulipo sasa?
Na sio kwamba tunadharau baadhi ya kazi, ila kama kuna ambacho ni bora zaidi kwa pale ulipo, ni vyema kuendea kile kilicho bora zaidi.
Labda tuseme kwa uwezo wako na mazingira uliyonayo, kazi pekee unayoweza kufanya ni kuokota makopo. Vizuri sana, sasa anzia hapo lakini usiridhike na kubaki hapo. Anza kuokota huku ukiwa na malengo baada ya muda fulani utakuwa huokoti tena wewe, bali utanunua kwa wale wanaookota, na unaendelea kukuza hivyo mpaka siku moja na wewe unamiliki kiwanda chako cha kutengeneza makopo, hii ni bora zaidi.
Labda kwa sasa umeweza kupata kazi ya kupanga mafaili, au kufagia ofisi, vizuri sana, sasa anzia hapo kuifikia ile ndoto kubwa uliyokuwa nayo wakati ambapo ulikuwa na ubunifu mkubwa sana.
Watoto wanajua kilicho bora, lakini kadiri wanavyokwenda na kukua wanasahau na kuridhika na kile wanachopata, hii ni sumu kubwa sana kwa mafanikio makubwa. Usikubali kabisa kuizika ndoto yako kubwa.
SOMA; Maisha Yako Yanaweza Kuwa Bora Zaidi, Anza Hivi….
TAMKO LANGU;
Najua watoto wanajua kile kilicho bora, na hata mimi nilikuwa najua kilichokuwa bora kwenye maisha yangu. Lakini baadae nilijikuta nasahau kile kilicho bora na kuridhika na kile nilichopata. Kuanzia sasa nafufua ndoto zangu zote kubwa na naanza kuzifanyia kazi. Najua kuishi tu maisha ya kuziendea ndoto zangu ni sehemu ya mafanikio makubwa.
NENO LA LEO.
Don’t settle for what life gives you; make life better and build something.
Ashton Kutcher
Usiridhike na kile ambacho maisha yanakupatia; fanya maisha yako kuwa bora zaidi na tengeneza kile unachotaka.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.