Mara nyingi watu wanaotaka kuingia kwenye biashara huwa wanaangalia biashara zinazofanyika sasa, na kama wakiona wanaofanya wana wateja, basi na wao huingia na kufanya biashara hiyo. Ni njia rahisi ya kuingia kwenye biashara, ila pia inaweza kumfanya mfanyabiashara ajikute kwenye changamoto kubwa sana hasa pale biashara zinapobadilika, na mara zote biashara huwa zinabadilika.
Wale wanaoingia kwenye biashara kwa kujua vizuri biashara wanazofanya na wateja wao, huendelea kudumu hata pale ambapo biashara zinabadilika. Ila wale wanaoingia kwenye biashara kwa kuiga, hujikuta kwenye wakati mgumu pale biashara zinapobadilika.
Leo kupitia kona hii ya mjasiriamali tutajadili njia nne muhimu ya kuzingatia kwenye biashara yako ambazo zitakuwezesha kujua kama biashara unayokwenda kufanya itakuwa na wateja. Na hata pale ambapo kutakuwa na mabadiliko ya kibiashara basi utaweza kwenda na mabadiliko hayo kwa sababu unaijua biashara yako vizuri na pia unawajua wateja wako vizuri.
Karibu sana ujifunze njia hizi nne muhimu kwa ukuaji wa biashara yako.
Njia hizi nne utakazojifunza hapa zitamhusisha moja kwa moja mteja na biashara yako. na hivyo ni muhimu sana kabla hujayafanyia kazi mambo haya manne uijue biashara yako vizuri na kisha uwajue ni wateja gani unaowalenga;
Njia ya kwanza; Je biashara yako inatoa ahueni kwa maumivu ambayo mteja anayo sasa.
Njia ya kwanza kabisa ni kuangalia ni maumivu gani ambayo wateja wanayapata sasa na kisha kuangalia kama kupitia biashara yako unaweza kuwaletea ahueni kwenye maumivu waliyonayo. Angalia kupitia biashara yako ni jinsi gani mtu anaweza kutuliza maumivu anayoyapata sasa.
Kumbuka kila mtu ana maumivu yake, na hivyo unapochagua maumivu makali sana na kuyapatia dawa ya uhakika, utakuwa na wateja wengi sana kwenye biashara yako. unapojua maumivu unayotuliza ni rahisi pia kuwajua wateja wenye maumivu hayo wanapatikana wapi ili uweze kufanya nao biashara zaidi.
Njia ya pili; je biashara yako inatoa suluhisho kwa matatizo aliyonayo mteja?
Watu wana matatizo yao, ambayo wangefurahi sana kama kuna mtu angewawezesha kuyatatua. Kwa njia hii unaweza kujenga biashara kubwa na yenye mafanikio kwa kuangalia ni matatizo gani ambayo watu wanayo sasa na ukayatatua. Kama ukiweza kuona tatizo kubwa na ambalo linawasumbua watu wengi, na ukaja na suluhisho bora la tatizo hilo, ni lazima utapata wateja wa biashara yako.
Angalia vizuri kwa biashara uliyonayo wewe, ni matatizo gani ya watu ambayo unaweza kuyatatua. Na ukishayajua angalia ni jinsi gani unaweza kuwafikia watu wenye matatizo yao, na wao wakajua ya kwamba wewe unaweza kuwatatulia matatizo yao.
Njia ya tatu; je biashara yako inakidhi mahitaji ya wateja.
Sio lazima kila mteja awe na maumivu, au awe na matatizo ya kutatua. Kuna wateja ambao wana mahitaji yao ya msingi, sio matatizo, bali mahitaji ya msingi ambayo wanahitaji mtu wa kuwawezesha kuyapata mahitaji hayo. Kwa biashara uliyonayo, je kuna watu wana mahitaji ya msingi sana ambayo wewe unaweza kuwapatia?
Fikiria vizuri juu ya biashara yako na fikiria vizuri juu ya mahitaji ya watu, kisha angalia ni jinsi gani unaweza kuwatambua wale wenye mahitaji unayokidhi na jinsi ya kuwafikia. Kulingana na biashara unayofanya, kuna watu wengi ambao wana mahitaji ya kile unachotoa. Ni wewe kuwatambua na kuwafikia.
Njia ya nne; je kuna lengo ambalo wateja wanalo na wewe unaweza kuwasaidia kulifikia?
Watu wana malengo mbalimbali kwenye maisha yako. na ili waweze kufikia malengo hayo, wanahitaji mchango wa watu wengine. Je biashara yako inaweza kumsaidia mteja kutimiza malengo yake ambayo amejiwekea? Kama ndio ni malengo gani hayo ambayo unaweza kumsaidia mtu kuyafikia? Kwa kujua malengo unayoweza kumsaidia mtu kufikia, na kisha kumjua mwenye malengo yale ni rahisi kufanya biashara na watu hawa.
Kwa nini ni muhimu kupitia njia hizi nne?
Ni muhimu sana kila mfanyabiashara kupitia njia hizi nne ili kujua ni njia ipi kati ya hizi anaitumia kuwahudumia wateja. Kwa kuijua njia anayotumia na kuwajua wateja wake, inakuwa rahisi kuikuza biashara yake. Na hata pale unapoitangaza biashara yako, huitangazi tu kwa kila mtu, bali unaitangaza kwa kulenga kile unachotoa kwa wale wanaokihitaji zaidi.
Fanya tathmini ya biashara yako au biashara unayotaka kuanzisha na ujue ipo katika njia ipi kati ya hizo. Biashara inaweza kuwa kwenye njia moja au hata zaidi ya moja. Ukishajua ulipo na ukawajua wateja wako, weka juhudi kuhakikisha unawapatia kilicho bora sana. Na wao wataiwezesha biashara yako kukua zaidi. Kila la kheri.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani