Sipendi kukuambia nini usifanye, kwa sababu ni hasi. Napenda kukuambia ni nini ufanye, ili iwe rahisi kwako kufuata vizuri.

Lakini kuba wakati ambapo msisitizo unahitajika zaidi ili kuhakikisha kwamba tunakwenda sawa. Yaani tunaelewana vizuri na unafanya maamuzi yako ukiwa unajua vizuri ni kipi unakwenda kupata.

Kuna sababu nyingi sana za kwa nini wewe usiingie kwenye biashara, ila hapa leo tutajadili sababu moja muhimu.

Kama haupo tayari kujifunza kila siku, basi usiingie kwenye biashara, endelea na mambo mengine, ambayo yanaweza kuwa muhimu zaidi kwako.

Watu wengi wanapofikiria biashara huona kama ni sehemu wao wanakuwa mabosi na kusimamia wengine. Lakini ukweli ni kwamba biashara ina changamoto nyingi kuliko picha hiyo unayojitengenezea. Na njia ya kuvuka changamoto hizi ili uweze kufikia mafanikio ni kuwa na maarifa sahihi. Na maarifa haya utayapata kama unajifunza kila siku kuhusu biashara.

Unapoingia kwenye biashara ni lazima biashara yako iwe muhimu sana kwako kiasi kwamba una shauku ya kujua vizuri na kwa undani. Ni shauku hii ndio inayokusukuma kujifunza zaidi na hivyo kubobea zaidi kwenye biashara hiyo.

Hivyo sababu ya kwanza kabisa kwa nini usiingie kwenye biashara ni kama hujawa tayari kujifunza kila siku.

Sababu nyingine muhimu sana, (hapa nakuibia) ni kama huna muda wa kutosha kusimamia biashara yako, wewe mwenyewe. Tutaijadili hii vizuri siku nyingine.

SOMA; Hii Ndio sababu halisi kwa nini biashara nyingi zinashindwa.

TAMKO LANGU;

Kama sipo tayari kujifunza kila siku, sitaingia kwenye biashara. Kwa sababu najua biashara inahitaji sana maarifa niliyonayo ili iweze kufanikiwa. Nitahakikisha najifunza kila siku ili niweze kuboresha biashara yangu na hatimaye kufikia mafanikio makubwa.

NENO LA LEO.

“If a person will spend one hour a day on the same subject for five years, that person will be an expert on that subject.”
– Earl Nightingale

Kama mtu atatenga saa moja kila siku kujifunza kitu fulani kwa miaka mitano, mtu huyo atakuwa mtaalamu aliyebobea kwenye kitu hiko.

Anza leo kutenga saa moja kila siku kujifunza kuhusu biashara yako, na miaka mitano ijayo utakuwa mbali sana kimafanikio.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.