Ndivyo maendeleo ya mwanadamu yalivyo…

Ndivyo maisha yako yanavyokwenda.

Unapiga hatua mbili kwenda mbele, halafu unapiga hatua moja kurudi nyuma.

Mambo yanaonekana kuwa mazuri, kila kitu kinakuwa sawa, halafu inatokea changamoto na kukurudisha nyuma.

Unakuwa unaona kila kitu kiko sawa na maisha ni mazuri, lakini inatokea changamoto au kikwazo ambacho kinakurudisha tena nyuma.

Inawezekana umesababisha changamoto hiyo moja kwa moja au sio wewe moja kwa moja.

Kikubwa ni usiumie sana, usianze kujilaumu kwamba ulikuwa pazuri na sasa umeharibu, jua maisha ndivyo yanavyokwenda, hivyo jifunze na songa mbele.

Ikiwa utakuwa unajilaumu na kujikosoa kila unapopiga hatua moja nyuma, utafanya mambo kuwa mabaya zaidi, badala ya hatua mbili mbele na hatua moja nyuma, utakuwa unapiga hatua moja mbele na hatua mbili nyuma, hivyo utakuwa unapotea kabisa.

Uko wapi sasa? Kwenye hatua mbili mbele au kwenye hatua moja nyuma? Hakikisha popote ulipo unajifunza ipi njia nzuri ya kuwa na maisha bora.

Na unahitaji kuwa na maisha bora kwenye hatua zote za maisha.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Hakuna Kisichokuwa Na Changamoto.

TAMKO LANGU;

Ninajua ya kwamba maisha sio njia ya moja kwa moja, kwamba sio mbele kwa mbele. Maisha ni hatua mbili mbele, na hatua moja nyuma. Mambo yanaweza kuwa mazuri sana lakini ikatokea changamoto na kunirudisha nyuma. Mimi nimeamua kuwa na maisha bora wakati wote, na hivyo nitajifunza jinsi ya kuendelea kuwa na maisha bora iwe naenda mbele au narudi nyuma.

NENO LA LEO.

Develop an attitude of gratitude, and give thanks for everything that happens to you, knowing that every step forward is a step toward achieving something bigger and better than your current situation.

Brian Tracy

Tengeneza tabia ya shukrani, na shukuru kwa kila kitu kinachotokea kwako. Jua ya kwamba kila hatua unayopiga mbele ni hatua ya kufikia kitu kikubwa na kizuri kuliko ulichonacho sasa.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.